Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa akihutubia umati wa wananchi katika kampeni zake zinazoendelea. |
MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowassa amesema kwamba iwapo atapata ridhaa ya wananchi ya kuchaguliwa kuiongoza nchi ataunda serikali rafiki kwa waendesha bodaboda nchini ili kutetea na kuboresha maslahi yao.
Akihutubia wananchi wa wilayani Babati, mkoani Manyara juzi alisema anataka kuona bodaboda wanapata malipo sahihi pamoja na kufanya kazi zao kwa uhuru ili kuinua kipato chao na kuondokana na umasikini.
“ Naomba mnichague kuwa Rais nina uwezo na nimejiamini kuwa natosha, ninagombea kwa sababu nimechoka na umasikini, mtu anakula mlo mmoja kwa siku, ni wakati wa watu kuondokana na umasikini,” alisema.
Alifafanua kuwa kutokana na azma yake hiyo ataongoza taifa kwa spidi 120 kwa saa katika kuleta maendeleo yaliyokusudiwa kwa kuanza na kipaumbele cha kuboresha elimu ambapo alisisitiza kuwa atafuta ada ya shule kuanzia elimu ya chekechea hadi chuo kikuu na kuboresha maslahi ya walimu.
Lowassa alisema anaweka kipaumbele kwenye elimu kwa sababu dunia ya sasa inaongozwa na teknolojia ya kisasa ambayo ana imani ndio dira ya kumkomboa Mtanzania wa leo na hasa kizazi kipya.
Aliongeza kuwa endapo atapata ridhaa hiyo atakuwa mtetezi wa wakulima nchini kwa kuwajengea misingi mizuri ya kupata masoko ya kuuza mazao yao popote duniani pasipo kutozwa kodi ya aina yoyote.
Chanzo Gazeti la HabariLeo
0 comments:
Post a Comment