JANA katika gazeti hili ukurasa wake wa mbele tuliandika taarifa
iliyotolewa na Tume Ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyoonya vyama vya siasa
kuhusu ushawishi wa kuwataka wafuasi wao kubaki katika vituo vya kupiga
kura wakishamaliza kupiga kura.
Pamoja na kuipongeza NEC kwa kutoa tamko hilo mapema tunapenda kuunga
mkono hoja ya Tume kuhusiana na tabia inayoelekea kushika kasi ya
ushawishi wa uvunjaji sheria wa wazi wazi unaoandaliwa na vyama
vinavyoshiriki uchaguzi mkuu.
Tunapenda kuamini kama inavyoamini NEC lengo la madai ya kulinda kura
haliko kwa nia hiyo ni ajenda ya siri ambayo inaweza kabisa kudhuru
uhuru wa uchaguzi wenyewe. Ni kweli kabisa kitendo cha kujikusanya
kitasababisha hofu kwa wapigakura wengine watakaokuwa wanaenda vituoni
kwa kukuta makundi ya watu, na tunavyojua makundi ya vyama vingine
hugeuka kuwa kichochea cha uvunjifu wa amani.
Kuna sheria na kanuni zinazoendesha uchaguzi ambazo vyama
vimekubaliana, kitendo cha kushawishi watu wabaki katika maeneo ya
upigaji kura, kutaleta mhemko usiokuwa wa kawaida hasa ikizingatiwa
kwamba vyama vinavyoshiriki ni vingi na si kimoja au viwili.
Aidha kama ilivyoshangaa NEC kwa nini vyama vinang’ang’ania kubaki
katika vituo vya kupigia kura na kuleta hisia kwamba vina ajenda ya
siri, tunajiuliza kulikuwa na haja gani ya kukubaliana katika maadili na
ufuataji wa utaratibu kisha unandaa mazingira ya ghasia na uvunjifu wa
amani?
Tunaamini kwamba wananchi watapuuza maneno ya wanasiasa hao uchwara
ili uchaguzi usijawe na hofu na watu wakashindwa kutumia nafasi yao ya
uhuru kupiga kura. Ni vyema kila mtu kwa nafasi yake apinge kwa nguvu
zote kitendo cha kurundikana katika vituo vya kura baada ya kupiga kura
na sheria zinazohusu uchaguzi zikazingatiwa kwa kuwa zimetengenezwa
kanuni zilizokubalika na wote wanaoshiriki.
Hali ya sasa ya kuandaa hasa makundi ya vijana yana athari zake
kisiasa na kijamii na kwamba vurugu zitakapoibuka kutokana na kugongana
kwa makundi katika eneo husika, waathirika si wa eneo hilo tu bali
Tanzania nzima kwani tutakuwa tumetia dosari uchaguzi.
Ni vyema wananchi na hawa wapiga kura wasikubali kutumika vibaya
kusababisha fujo kwa maslahi ya wanasiasa wachache ambao maslahi ya
taifa ni adimu kwao. Ni vyema Watanzania wakasoma alama za nyakati na
kujiepusha na uvunjifu wa amani unaoshawishi mapema na wanasiasa wenye
uchu wa madaraka kwa kile wanachodai ulinzi wa kura.
Ni kweli hakuna ulinzi wa kura wa stahili hiyo hasa ikizingatiwa
kwamba kila kitu kinafanyika kituoni pale, kinafanyika kwa utaratibu wa
maridhiano ya pande zinazoshiriki katika uchaguzi. Tunatoa wito kwa
Watanzania wanaoitakia mema nchi hii kupuuza kwa makusudi kabisa miito
kama hii ya ulinzi wa kura kwa kubaki vituoni ili tuwe na uhakika
uchaguzi wetu unafanyika kwa namna inavyostahili.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment