Rais Jakaya Kikwete.
RAIS Jakaya Kikwete ameagiza kero za madereva nchini, zianze
kutatuliwa na ripoti za hatua zitakazoanza kuchukuliwa kuanzia kesho,
zipelekwe kwake moja kwa moja. Amesema hayo jana alipokutana na
wanachama wa Chama kipya cha Madereva (TADWU), wakati alipokutana nao
jijini Dar es Salaam akiwa na maofisa wa Wizara ya Kazi na Ajira, Kikosi
cha Usalama Barabarani na Mdhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(Sumatra).
Akizungumza katika mkutano huo baada ya kupokea risala ya madereva
hao, Rais Kikwete aliagiza Sumatra kumpa taarifa ya namna walivyojipanga
kukagua madereva wenye mikataba na wasio na mikataba.
"Jumatatu lazima mnipe taarifa ya mkutano wenu, Sumatra kwenye hiyo
mikataba mnahakiki nini na nani ana mkataba na nani hana mkataba,"
alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete aliwataka Sumatra pia kusimamia
mazungumzo kati ya wamiliki wa magari na madereva na kupata muafaka
katika matatizo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na madereva hao kwa muda
mrefu bila ufumbuzi hasa katika masuala ya posho na mishahara.
"Mikataba ambayo inaonesha mtu analipwa kiasi gani na posho yake ni
kiasi gani hiyo ndiyo mikataba kamili, hata mimi nilipoingia, nilipewa
mkataba unaoeleza kwa miaka mitano Rais unastahili hiki na hiki,"
alisema Rais Kikwete. Rais Kikwete alisema hana mamlaka ya kupanga posho
lakini aliwataka Sumatra kukaa chini na wamiliki wa magari, madereva na
Wizara ya Kazi na Ajira kupanga namna ya kuwalipa madereva.
"Mnapotegemewa kusimamia na hamsimamii vizuri mnatengeneza
manung'uniko... tendeni haki, simamieni vizuri," alisema Rais Kikwete.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Giliad Ngewe aliwekwa katika wakati
mgumu na Rais Kikwete baada ya kuulizwa maswali ni lini wanapitia
mikataba ya madereva hao, ambapo alijibu kwa kusua sua jambo lililofanya
madereva waliojaa katika ukumbi huo kumzomea.
Rais Kikwete alibaini kuwa madereva wengi hawana mikataba jambo
lililosababisha wafanye kazi katika mazingira magumu ambapo aliwataka
Sumatra kuhakikisha madereva wote wana mikataba. Alisema sekta ya
usafirishaji inachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa
nchi na madereva ndio wanaoendesha uchumi wa nchi.
Kuhusu madai ya madereva kupigwa tochi na askari wa usalama
barabarani wawapo safarini, aliwataka madereva hao kutii sheria sambamba
na kuzingatia sheria za usalama barabarani. Alisema madereva nao
wamekuwa wakikiuka sheria za barabarani na kusababisha ajali nyingi
zinazotokea nchini na kusababisha maafa makubwa na upotevu wa mali. Rais
Kikwete alitoa mfano wa alama za barabarani zinazoonesha kuwa dereva
hapaswi kwenda kwa kasi ya zaidi ya kilometa 80 kwa saa, lakini unakuta
dereva ndio anakanyagia kasi ya kilometa 120 kwa saa.
Alisema kama madereva wangekuwa wakitii sheria na alama za
barabarani, kusingekuwa na haja ya hizo tochi, lakini vifaa hivyo
vinawekwa kutokana na madereva kutotii sheria. Mbali na hayo, Rais
Kikwete pia aligusia suala la kuzidisha mizigo katika magari na kusema
madereva wamekuwa wakipewa uzito maalumu wa mizigo yao, lakini
wanazidisha, hata hivyo madereva hao walipiga kelele kuwa ni tatizo la
wamiliki.
*Mpinga na Matrafiki
Hata hivyo, alimtaka Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani,
Mohamed Mpinga, kuondoa matrafiki wanaoomba rushwa barabarani. Alisema
madereva wa nje ya nchi wanaobeba mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam
kwenda katika nchi zao, wamewaeleza viongozi wao kuwa wamekuwa
wakilazimika kuwa na bajeti ya rushwa wanazoombwa na trafiki barabarani.
Aliwapongeza madereva kwa kuanzisha chama cha kuweka na kukopa na
kusema kuwa naye atawasaidia.
Kuhusu mafunzo, alimuagiza Kamanda Mpinga kutafuta namna ya
kuzungumza na wamiliki wa magari, ili mafunzo hayo ya kila baada ya
miaka mitatu, yafanyike kwa utaratibu utakaotunza ajira za madereva na
gharama zilipwe na wamiliki.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment