Sunday, 4 October 2015

Tagged Under:

Mashabiki Simba, Yanga hawaishi vituko uwanjani

By: Unknown On: 05:20
  • Share The Gag
  • Aina ya ushangiliaji wa mashabiki wa Yanga wakicheza na Simba.

    KAMA ilivyo kawaida. Tambo za mashabiki wa Simba na Yanga zilianzia nje ya milango ya kuingilia uwanjani, ambapo mashabiki kama kawaida yao walikuwa wanacheza kwa mbwembwe na utani mwingi.
    Simba ilibeba jeneza ambalo lilifunikwa kwa bendera yenye rangi za njano na kijani, ambazo ni za Yanga, ambalo lilisindikizwa na mashabiki wengi, kwa kuamini kuwa wanaenda kummaliza mtani wao Yanga. Aidha, kundi la mashabiki wa Yanga likisindikizwa na watu waliovaa mavazi kama ya kiganga na vibuyu lilikuwa likiingia ndani ya uwanja huku likicheza kwa mbwembwe wakitamba kuwa walikuwa wakienda kummaliza mtani wao Simba.
    Utani wa aina hiyo ni kawaida kwenye soka sio tu ndani ya Tanzania bali hata katika nchi nyingine za kiafrika. Ndani ya uwanja Kumbe mashabiki wa Yanga ni waoga. Rekodi zilizokuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari kuwa Simba wamekuwa wakiionea vilisababisha mashabiki kutokuwa na furaha. Uwanjani waliokuwa wakishangilia sana kabla ya mechi ni mashabiki wa Simba tena wakiamini kuwa wataendeleza rekodi yao ya kuwafunga watani zao.
    Lakini kwenye majukwaa ya Yanga mashabiki walikuwa watulivu, huku baadhi yao walikuwa wakionesha mbwembwe lakini asilimia kubwa walikuwa ni watulivu wakisikiliza ni nini kitatokea. Inaonekana kuwa mashabiki wengi wa Yanga walikuwa hawaamini kama siku hiyo timu yao ingeweza kuibuka na ushindi, huku baadhi yao ambao walikuwa wachache walijikaza kisabuni wakishangilia kujipa moyo.
    Ukilinganisha ni misimu mingine iliyopita tulizoea kuona mashabiki wakizomeana, wote wakishangilia timu zao kwa zamu lakini kwa Yanga kipindi cha kwanza dakika chache za mwanzo haikuwa hivyo. Haikuwa hivyo kwa sababu waliamini kuwa kuna uwezekano wa kufungwa tena. Wachezaji wenyewe Wakati wachezaji walipokuwa wakiingia uwanjani Hamis Kiiza alikwenda kwenye benchi la Yanga na kumkumbatia Kocha Hans Pluijm na kusalimiana naye.
    Huenda alikuwa akimkubali kocha huyo ambaye wakati anaifundisha Yanga kabla ya mchezaji huyo kuondoka walikuwa wakielewana na alikuwa akimwamini na kumpa nafasi. Mwanzo wa mchezo Kikosi cha Yanga kiliingia uwanjani kama hakijiamini kabisa, ambapo walianza kwa mchecheto huku wakipoteza mipira ovyo ovyo tu na kusababisha kipa wao Ally Mustapha kulalamika.
    Kuna wakati Nadir Haroub alikuwa akilalamika sana kwani wachezaji wenzake walikuwa hawajatulia ipasavyo. Pengine ni kutokana na kuonesha presha. Hali hii haikumfurahisha hata kidogo kocha msaidizi Charles Mkwasa, ambaye alisimama ghafla kwani alikuwa amekaa kwenye benchi, akimnyooshea kidole Haroub kwa kitendo cha kuwagombeza wenzake kwamba sio kizuri, kinawaharibu kisaikolojia na kuwatoa mchezoni.
    Jambo la kufurahisha ni kuona kuwa Simba walikuwa wakicheza kwa kujiamini hasa kipindi hicho cha kwanza, kwani mashambulizi waliyoingia nayo yaliwachanganya Yanga. Walikuwa wakipata nafasi lakini hawakuweza kutimiza kile ambacho walikikusudia cha kutumbukiza mpira ndani ya lango la Yanga. Kitendo cha Yanga kucheza vibaya dakika kama 15 za mwanzo hakika kilisababisha mashabiki wake kutulia tuli wakiona huenda mambo yatakuwa mabaya.
    Baada ya kutolewa Simon Msuva dakika 34 na kuingia Malimi Busungu mchezo ulibadilika kwa kiasi fulani na kusababisha Yanga kufanya mashambulizi ambayo baadaye yalizaa goli la kwanza. Mashabiki wa Yanga Walikuwa kimya, baada ya goli la kwanza lililofungwa na Donald Ngoma, ambapo jukwaa la Yanga lilianza kuchangamka na kuhamishia huzuni kwenye jukwaa la Simba. Utani wao ulianza rasmi, walianza kuchangamka, kuimba na hata kusimama kuishangilia timu yao huku wakiwakebehi watani zao.
    Mashabiki wa Simba Kwa jinsi ambavyo mchezo ulivyokuwa ukiendelea, mashabiki wa Simba walianza kumnyooshea kidole mwamuzi wa mchezo Israel Nkongo ambaye alikuwa akichezesha mchezo huo. Kila ilipokuwa ikipigwa filimbi waliona kuwa haiwatendei haki, na baada ya Yanga kufunga bao la pili lililofungwa na Malimi Busungu, hali ilikuwa mbaya zaidi kwa mashabiki wa Simba ambao matumaini yao yalianza kupungua.
    Hakika Simba waliamini kwa asilimia 100 kuwa lazima washinde mchezo ule kutokana na rekodi ya huko nyuma lakini mambo hayakuwa kama walivyotarajia. Aina ya ushangiliaji Kweli huu msimu mpya na mambo mapya. Ushangiliaji wa Hamis Kiiza na mashabiki wa Simba katika mechi ya Kagera Sugar ulikuwa ni salamu kwa Yanga. Baada ya kufunga ‘hat trick’ kwa maana ya mabao 3-1 peke yake katika mchezo huo wa Kagera, alitoa ishara kwa kushika kwenye mkono kwamba bado muda kidogo kuifunga Yanga.
    Ushangiliaji huo uliungwa mkono na Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba, Haji Manara na mashabiki wote. Kilichotokea katika mechi ya Simba na Yanga, baada ya Yanga kushinda, aina ile ya ushangiliaji wakawaonesha Simba kwamba huo muda uko wapi? Walikuwa wakishangilia mabao yao kwa kushika mikono yao wakiuliza huo muda uko wapi?
    Kwa kweli ilikuwa ni aina mpya ya ushangiliaji wa utani kwa timu hizo. Siasa za mashabiki Siku zote Simba wanapoona watani zao wanacheza vibaya huanza kuwatania kwa kuwaimbia CCM, CCM, CCM. Tena jambo la ajabu zaidi msimu huu siasa kuhusishwa na soka baada ya mashabiki wa Simba kuonesha ishara ya kuzungusha mikono kwamba wanahitaji mabadiliko.
    Awamu hii, Yanga walivyoshinda na wao, wakaimba CCM, CCM, CCM kisha wakawarudishia Simba ishara hiyo hiyo ya mabadiliko. Ishara ambazo wamekuwa wakizitumia, tumekuwa tukiziona mtaani hasa kwenye kampeni za siasa. Kitendo cha kutumika kwenye soka, inaonesha wazi ni jinsi gani mashabiki hao wametekwa na harakati za siasa zinazoendelea nchini kote.
    Ingawa kwa upande mwingine zinaweza kuleta matatizo baadae kwani sio wote wanaoshabikia Simba ni Ukawa au CCM au sio wote wanaoshabikia Yanga ni CCM au Ukawa. Mabadiliko ya mchezaji Mchezaji wa Senegal, Pape Ndaw aliingia dakika ya 84 kuchukua nafasi ya Ramadhan Kessy. Kubadilishwa kwake haikuwa tatizo, la kushangaza ni kiatu alichokuwa amevaa.
    Ilikuwa ni kama jambo la aibu kwa mchezaji huyo wa kimataifa kuingia na kiatu kibovu uwanjani, huku wengine wakielekeza katika imani za kishirikina kwani mchezaji wa kulipwa kama yule hakustahili kabisa kuvaa kiatu kibovu kama kile. Sio kwamba hana vingine, isipokuwa inadaiwa hicho ndicho kiatu alichokichagua kukichezea uwanjani. Kiatu chake hicho kilizua mjadala mkubwa na kuhusishwa na imani za kishirikina.
    Kadi za njano, nyekundu Ama kweli refa Israel Nkongo hakutaka masihara. Katika mchezo huu aligawa kadi nane kutokana na wachezaji kutendeana madhambi. Ngoma amewapa wachezaji wawili wa Simba kadi za njano. Juuko Murshid na Ramadhan Kessy waliomtendea madhambi.
    Aidha, Mussa Mgosi na Salum Telela walipewa kadi ya njano kila mmoja kutokana na kufanya madhambi kwa wakati tofauti Twite alipewa kadi mbili za njano kisha nyekundu kwa kumuangusha Mohamed Tshabalala, na Tshabalala akipewa kadi ya kumuangusha Busungu.

    Created by Gazeti la HabariLeo.


    0 comments:

    Post a Comment