Sunday, 4 October 2015

Tagged Under:

Magufuli-Nitaongoza Serikali yenye utajiri

By: Unknown On: 05:12
  • Share The Gag

  • Mgombea wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia wananchi.

    MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema atarithi Serikali tajiri na kuwataka Watanzania kuwa makini kuchagua kiongozi muadilifu, akionya kuwa wasio waadilifu wameshaanza kujipanga kugawana rasilimali za Taifa, ikiwemo gesi asilia na bandari.
    Akizungumza juzi na jana mkoani Singida, Dk Magufuli mwenye historia ya kusimamia miradi ya miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni tisa, aliwaomba wananchi wamchague kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisema yeye hana mtu anayemdai fadhila.
    Alitoa mfano wa mchakato wa kuwania nafasi ya kuwa mgombea urais wa CCM, ambapo Dk Magufuli alisema wako baadhi ya wenzake walitumia fedha nyingi kupata nafasi hiyo, ambazo watapaswa kuzirejesha watakapoingia Ikulu.
    “Ukiwanunua watu, hutaogopa kuwauza...mimi nilichukua fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kimya kimya na nikarudisha kimya kimya na hata kuchaguliwa kwangu, kulikuwa kimya kimya kwa nguvu za Mungu.
    “Msichague watuhumiwa wa ufisadi nchi hii itauzwa...wameshaanza kugawana rasilimali za Taifa, wengine mafuta na wengine gesi na reli,” alisema Dk Magufuli bila kufafanua.
    Kwa mujibu wa Dk Magufuli, Tanzania ina Serikali tajiri ambayo alisema haipaswi kutegemea ushuru kutoka kwa watu wa maisha ya chini, ambao alisema wakati mwingine haufiki serikalini, bali unaishia kwenye matumbo ya watu wachache.
    “Tanzania ni tajiri, mazingira yamesharahisishwa na kazi yangu itakuwa rahisi,” alisema huku akishukuru waliomtangulia kwa kumrahisishia kazi kwa kusambaza nishati ya umeme, kujenga miundombinu ya barabara na kudumisha amani.
    *Misingi tajiri
    Ingawa hakufafanua zaidi, lakini tangu Agosti mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete ambaye anatarajiwa kustaafu hivi karibuni, alishatangaza kuwa kazi yake kabla ya kustaafu, ni kuweka misingi ya kitaasisi ya kumwezesha rais ajaye, aongoze nchi tajiri.
    Akiwa katika Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo mjini Washington D.C, Marekani Agosti 4 mwaka jana, Rais Kikwete alisema anataka na anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi ambayo ni masikini na hivyo atatumia muda wake uliobakia katika uongozi kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo wa Serikali tajiri.
    Akifafanua zaidi kuhusu msingi mkubwa wa Tanzania tajiri, Rais Kikwete alipokuwa akielezea Hali ya Baadaye ya Tanzania Baada ya Ugunduzi wa Gesi katika kituo hicho Marekani, alisema ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wananufaika na ugunduzi wa gesi asilia.
    “Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Watanzania na nchi yao wananufaika kutokana na mapato ya rasilimali ya gesi asilia... Rasilimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri.
    “Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye njia hiyo ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu,” alikaririwa Rais Kikwete.
    Pia katika mkutano na viongozi wa dini uliofanyika jijini Dar es Salaam mwaka jana, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia fursa za wazawa katika uchumi wa gesi, alieleza kuwa utaratibu kwa wawekezaji wote ni Serikali kupata mapato yake ya kati ya asilimia 65 na 70 na mwekezaji kati ya asilimia 30 na 35.
    “Tunataka kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lakini hata wao wakipewa leseni utaratibu utakuwa ule ule kama wengine na hili ni kwa kampuni zote. Serikali itapata kati ya asilimia 65- 70 na mwekezaji asilimia 30-35. Ndio maana tunapenda Serikali ilisimamie hili ili rasilimali hii inufaishe Watanzania wote,” alikaririwa akisema.
    *Mapato ya gesi
    Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kufanikisha lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali gesi, ni pamoja na kupitishwa na kusainiwa kwa Sheria ya Mafuta na Gesi; Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini; Mafuta na Gesi Asilia na Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi.
    Sheria hizo zimelenga kuhakikisha Serikali inapata fedha za mgawo unaotokana na kumiliki hisa na kodi katika vitalu vya rasilimali hiyo, kama ilivyofanyika katika nchi za Norway na Trindad na Tobago, badala ya kupeleka kwa watu binafsi.
    Aidha katika Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi, inayounda Mfuko wa Mafuta na Gesi, kumewekwa adhabu kali kwa mtu atakayetumia vibaya fedha za gesi, ikiwemo faini isiyopungua kiasi cha fedha ambacho mhusika amechukua, kifungo cha miaka 30 jela na kufilisiwa mali.
    *Mapato mengine
    Serikali ijayo pia itarithi uwezo wa kukusanya mapato ya Serikali wa Sh bilioni 850 kwa mwezi, kutoka makusanyo ya Sh bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi takribani Sh bilioni 850.
    Uwezo huo wa makusanyo umesaidia kupunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya Serikali mwaka 2005, hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015.
    Aidha Serikali ijayo pia imeachiwa fungu la fedha kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC), kwani kuanzia mwakani itapokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi ya Sh trilioni moja za Kitanzania kwa ajili ya kusambaza umeme, ambao kwa sasa asilimia 46 ya Watanzania wananufaika nao kutoka asilimia 10 tu ya Watanzania ilivyokuwa mwaka 2005.


    Chanzo Gazeti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment