Mchungaji Christofa Mtikila enzi za uhai wake.
MWILI wa mwanasiasa machachari na mwenye misimamo mikali katika
ufuatiliaji wa mambo, Mchungaji Christopher Mtikila (65) unatarajiwa
kuagwa kesho, Dar es Salaam. Aidha, baada ya shughuli ya kuuaga mwili wa
Mtikila, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa chama cha siasa cha DP,
utasafirishwa kwenda kijijini kwao Milo wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe
kwa ajili ya maziko.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Mikocheni jijini Dar es Salaam,
kaka wa marehemu, Stanley Mtikila alisema kwa sasa mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo hadi kesho, ambapo utaagwa
na kusafirishwa.
“Bado tuna majonzi makubwa kutokana na msiba wa ndugu yetu na kaka
yetu mpendwa, lakini hatuna budi kuupokea kwani umeshatokea na hivi sasa
mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya jeshi Lugalo, tunatarajia
kuuaga kesho na kuusafirisha hadi kijijini,” alisema. Aliongeza kuwa
siku ya maziko haijajulikana, huku akisema kama watawahi kufika kijijini
kwao, basi maziko yatafanyika siku hiyohiyo.
“Maziko yatategemeana na muda tutakaofika, kama tukiwahi basi kesho
hiyo hiyo tutazika lakini tukichelewa hadi siku inayofuata ndiyo
tutamzika,” aliongeza. Kwa upande wake, kaka yake mwingine ajulikanaye
kwa jina la Charles Mtikila, alisema wao kama familia wameupokea msiba
huu kwa majonzi makubwa, lakini haina budi kukubali mipango ya Mungu,
licha ya watu wanaozungumza mengi kufuatia msiba huo.
“Msiba umetokea na sisi tumeupokea kama familia, mengine
yanayozungumzwa kuhusu msiba huu ni mambo ya kawaida kwani mimi mwenyewe
nimekwenda eneo la tukio na kaka yetu amefariki kwa ajali ya gari na
hio ndio taarifa kamili,” alisisitiza. Mtikila alifikwa na mauti baada
ya gari lake aina ya Toyota Corolla, lenye namba za usajili T189 AGM,
alilokuwa anasafiria kuacha njia na kupinduka eneo la Msolwa wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani katika barabara kuu ya Dar es Salaam- Morogoro.
Mtikila alikuwa akitokea mkoani Njombe, alikopita akitokea Rungwe
mkoani Mbeya ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa kampeni wa kumnadi
mgombea ubunge wa chama chake cha DP Jimbo la Rungwe, Nicodemus Atuswege
Ngwale, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mchungaji Mtikila alizaliwa mwaka 1950 huko Ludewa na hadi mauti
yanamfika, kama si kuenguliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwa
sasa angekuwa miongoni mwa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mtikila ambaye maisha yake ya kila siku yalitawaliwa na
harakati za kisiasa, haki za binadamu na mengine mengine, alienguliwa na
NEC kwa kuwa hakuwa na mgombea mwenza.
Akijitetea mbele ya NEC Agosti 21, mwaka huu, Mtikila alisema:
“Nimeshindwa kuja na mgombea mwenza kwa sababu mke wake ameugua presha
ghafla. Jambo hilo lilimfanya ashindwe kufika hapa.”
Mtikila alidai alifika mapema NEC, lakini alilazimika kwenda Mahakama
Kuu kwa ajili ya kuapa. Alidai kuwa mahakamani alitumia zaidi ya saa
mbili kumsubiri mgombea mwenza, Juma Metu Juma ambaye hakutokea.
“Nilipotaka kumuona Mkurugenzi (Kailima Kombwey) nilijibiwa kuwa
anashughulikia tatizo langu. Lengo lilikuwa kutaka kumueleza tatizo
nililonalo. Kwanza taratibu na kanuni za NEC hazisemi chochote iwapo
mgombea mwenza anapata dharura,” alisema Mtikila, ambaye alikiri kuwa
hakulipa Sh milioni moja, licha ya kuwa nayo mfukoni.
Baada ya maelezo yake kutoishawishi NEC, Mchungaji Mtikila alisema:
“Mimi kugombea si tatizo, ila nataka kuweka mambo sawa. Hata
nisipogombea hiyo hainizuii kwenda mbinguni. Kwanza mtu mwenye uchu wa
madaraka ya kwenda Ikulu anatakiwa kuepukwa kama ukoma.”
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Mtikila kushindwa kutekeleza masharti
na hivyo kupoteza sifa za kuteuliwa na NEC kugombea urais. Mara ya
kwanza ilikuwa mwaka 2010. Alishiriki mwaka 2005 na kupata asilimia 0.27
ya kura zote, huku Rais Jakaya Kikwete akiibuka mshindi kwa asilimia
80.28.
Nje ya siasa Pamoja na shughuli za siasa, pia alikuwa mwanzilishi na
Mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Full Salvation. Lakini pia kwa muda
mwingi wa maisha yake, alijihusisha na harakati za haki za binadamu kwa
kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo, kiitwacho Liberty
Desk.
Kanisa lake ni moja ya makanisa machache nchini yenye vitengo vya
namna hiyo. Umaarufu wa Mtikila ulikua mwanzoni mwa miaka ya 1990
kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuongea.
Upinzani wake dhidi ya muundo wa Muungano kati ya Tanganyika na
Zanzibar, madai yake kuhusu kile anachokiita “Uhujumu wa uchumi
unaofanywa na watu ambao aliwaita magabacholi” na kesi mbalimbali za
kikatiba, alizokuwa akifungua katika Mahakama za Tanzania, ni kati ya
mambo machache yaliyomfanya asikike kila kona ya nchi.
Kwa muda mrefu, chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa
kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar. Alikuwa akisisitiza
kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo Tanzania.
Hata hivyo, ilimpasa abadili msimamo wake katika miaka ya hivi
karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inavyotaka) ndipo kikapata usajili wa kudumu.
Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa
kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala. Kwa
ujumla maisha yake yamekuwa ni ya harakati muda wote, akipambana
awezavyo, akisimama kidete inavyowezekana na akijikuta matatani kila
uchwao.
Mchungaji Mtikila ameacha mjane, Georgia na watoto. Ubunge, urais na
kesi za kikatiba Itakumbukwa kwamba, kabla ya kujaribu kuwania Urais,
mara kadhaa alijaribu kuusaka ubunge wa Ludewa, kwa mfano mwaka 1997,
aliwania kwa tiketi ya Chadema kwa kuwa DP hakikuwa na usajili wa
kudumu.
Hata hivyo, baada ya uchaguzi mdogo, uliompa ushindi Crispin Haule wa
CCM, Mtikila aliachana na Chadema na kurejea kukiimairisha chama chake.
Mtikila aliyekuwa maarufu kwa watu wa rika zote, alikuwa na sifa
kadhaa, mojawapo ikiwa ni kuwa kiongozi anayejishughulisha na mambo
mengi mno na harakati zilizopitiliza, akiwa na ufahamu wa vitu vingi
pia.
Aidha, alipambana kisheria na serikali kwa kufungua kesi za masuala
mbalimbali dhidi ya serikali, zikiwemo za kikatiba. Aliwahi kufungua
kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi wa Tanzania,
wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila hati za
kusafirioa na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba
kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya na polisi na nyinginezo.
Na juu ya yote, Mtikila aliyekuwa hajali kupanda pikipiki au bajaji
kuwahi harakati zake, zikiwemo za mahakamani, alikuwa mtu mwenye
misimamo ya kipekee. Alipokuwa na ajenda zake, bila kujali hatimaye
yake, alizisimamia kwa nguvu zake zote.
Mtikila ameaga dunia akiwa mwanasiasa mashuhuri nchini, akiwa na
uwezo wa kuongoza kanisa (uchungaji), kuongoza chama cha siasa na
kushinda mahakamani kupambana na Serikali kwenye kesi kubwa na ambazo
nyingine alishinda.
Chanzo Gazeti la HabariLeo
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment