Tuesday, 6 October 2015

Tagged Under:

Magufuli: Uadilifu wangu hauna shaka

By: Unknown On: 03:33
  • Share The Gag

  • Mgombea Urais kupitia CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa hadhara.

    MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema uadilifu wake ni wa kuaminika na ameamua kujitoa sadaka kwa ajili ya kutumikia Watanzania katika uhai wake. Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Katesh wilayani Babati mkoani Manyara, jana, Magufuli alisema anachotaka ni kufanya kazi na si siasa.
    “Inawezekana nikaonekana siyo mwanasiasa mzuri, mimi sifanyi siasa, nataka nifanye kazi na hiyo iwe sadaka yangu katika maisha yangu nikiwa duniani,” alisema Magufuli. Katika mkutano huo ambao baada ya kuhutubia, baadhi ya watu walianza kurusha kadi za Chadema, alisema anajiamini kwa uadilifu.
    Aliomba wananchi wazidi kumwombea atekeleze azma yake ya kujitoa sadaka kutumikia watanzania. Aliahidi kufanyia kazi kero mbalimbali katika wilaya hiyo, zikiwemo zilizotolewa na mgombea ubunge wa Jimbo la Hanang, Dk Mary Nagu. Dk Nagu aliomba Magufuli kuamuru shamba kubwa la Basuto, lirudi kwa wananchi.
    Magufuli aliwataka wananchi wapuuze wanaotoa ahadi wasizoweza kutimiza. Mafisadi Akihadharisha wananchi dhidi ya kununuliwa na mafisadi ili wawapigie kura, alisema fedha hizo ni walizoiba hivyo zinarudi taratibu kwa wananchi.
    “Wakiwagawia hela kuleni, hizo hela mliibiwa siku nyingi. Wanaanza kuzirudisha pole pole,” alisema. Akiwa katika eneo la Dongobash kwenye Jimbo la Mbulu Vijijini, ambalo Mbunge wake, alikuwa Mustapha Akonaay wa Chadema, Magufuli alimpigia chapuo mwanasiasa maarufu, Dk Willibrod Slaa.
    Akonaay sasa anagombea kupitia ACT-Wazalendo na mgombea wa CCM ni Frateu Massay na wa Chadema ni Paul Sulle. Akimnadi mgombea wa CCM, Magufuli alisema kama angekuta Dk Slaa ndiye mgombea wa ubunge, angewaambia wananchi wamchague bila kujali chama chake kwa kuwa ni mtu anayejali haki za Watanzania.
    Akisisitiza kuwa maendeleo hayana chama, aliwaasa wananchi kuepuka kuingiza mafisadi madarakani. Aliendelea kuhadharisha kuwa wakikubali kununuliwa kwa fedha, wafahamu pia watauzwa. Akiwa eneo hilo la Dongobash wananchi waliwasilisha kero mbalimbali kwa Magufuli kupitia mabango.
    Miongoni mwa mambo waliyolalamikia, ni kile walichodai mmoja wa wana Ukawa kuwa amewadhulumu shamba kwa kesi ya kuchongwa. Magufuli aliwataka wamwachie suala hilo, akisema mashamba yanasimamiwa na Sheria za Ardhi Namba 4 na 5 za mwaka 1999, ambazo zote ziko chini ya usimamizi wa rais.
    Magufuli aliomba akabidhiwe mabango hayo, aende nayo kwa ajili ya kwenda kufanyia kazi kero walizotaja. Akiwa mjini Haydom wilayani Mbulu, Magufuli alisema, “Tanzania tumechoka kuchezewa na mafisadi na mimi nimejitoa sadaka kupambana na mafisadi.”
    Mgombea huyo aliahidi barabara inayotoka Katesh kwenda Haydom, itajengwa kwa lami. Pia aliahidi serikali itaendelea kuwa karibu na Hospitali ya Haydom inayomilikiwa na KKKT kwa kutoa ruzuku, kulipa mishahara kwa wataalamu.
    Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kusisitiza kuwa kitashinda kwa zaidi ya asilimia 80 kutokana na namna ambavyo kimeweza kufikia wananchi wengi kwa usafiri wa nchi kavu tofauti na wanaotumia usafiri wa anga.
    Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulembo, alisema mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amefika kwenye vijiji 9,002 katika mikoa 20 na kufanya kampeni. Alisema hayo jana mjini Babati mkoani Manyara wakati akimkaribisha Magufuli kuhutubia mkutano wa kampeni.
    Bulembo ambaye amekuwa akiongozana na mgombea huyo, alisema kwa wanaofanya utafiti, inaonesha mgombea huyo atashinda kwa asilimia 81.9. Alisema kampeni za Magufuli ni za nchi kavu, jambo lililowawezesha kukutana na watu wengi tofauti na wengine wanaotumia usafiri wa anga.
    “Watanzania hawako angani, wako chini,” alisema. Hata hivyo, akihutubia mjini hapa, Magufuli alisema, “Mimi sitaki asilimia 81, nataka asilimia 99 ya urais au hata 100.” Alihoji wanaotaka ushindi huo na kuitikiwa kwa sauti ya juu na maelfu ya watu katika mkutano huo.
    Mkutano wa Karatu Akihutubia mkutano wa kampeni mjini Karatu, Dk Magufuli aliwaambia katika miaka ya nyuma, walipata kiongozi mzuri, ambaye ni Dk Willibrod Slaa. Magufuli ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu, alisema Dk Slaa ni kiongozi ambaye anamfagilia licha ya kwamba ni wa chama kingine.
    Akishangiliwa na umati wa watu uliohudhuria mkutano huo, Magufuli alisema, Dk Slaa ni mtu mwenye msimamo, mwadilifu na anayemtanguliza Mungu. Magufuli ambaye amekuwa akiomba kura kwa vyama vyote vya siasa huku akisisitiza kwamba maendeleo hayana vyama, alisema ni vyema kuonesha msimamo wa jambo lolote ambalo ni zuri bila kujali itikadi za vyama.
    Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya watu, Magufuli alisema, “Ndugu zangu wa Karatu mmefunika…mtu mwingine asingemsifu mtu wa chama kingine kama mimi nilivyomsifu Dk Slaa…tunatakiwa kuwa na msimamo kama wa Dk Slaa,” alisema.
    Wakati huo huo, Magufuli alisema miongoni mwa mambo atakayofanya kwa ajili ya jamii ya wafugaji, ni pamoja na kuhakikisha yanakuwapo malambo ya kutosha kwa ajili ya kunyweshea mifugo. Pia, alisema serikali yake itatoa ruzuku ya asilimia 60 kwa dawa za mifugo.
    Vile vile alisisitiza mkakati wake wa kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ambavyo miongoni mwake, vitakuwa ni vya mazao ya mifugo. Aliahidi pia atatoa kipaumbele kwa sekta ya utalii, kuhakikisha inaimarika.

    Chanzo Gazti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment