Sunday, 4 October 2015

Tagged Under:

Mabadiliko ni ya uchapakazi-Mwigulu

By: Unknown On: 05:06
  • Share The Gag

  • Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mwigulu Nchemba.

    MJUMBE wa Kamati ya Ushindi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba ametaka Watanzania kutambua mabadiliko yanayohitajika si ya vyama vya siasa, bali ni uchapakazi huku akisisitiza kuwa mgombea wa CCM, hakupitishwa kujaza nafasi bali kwa utendaji wake.
    Mwigulu alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ya Ushindi, waliopewa nafasi kuzungumza katika mkutano wa kampeni mjini Singida, wakimtaja Dk Magufuli kuwa ni mtu wa aina yake ambaye Taifa litaandika historia ya mabadiliko kwa kumchagua.
    Katika mkutano huo, wajumbe wengine waliozungumza ni January Makamba na Lazaro Nyalandu, huku Mwigulu akihadharisha kuwa kuna vyama vinavyotaka mgombea urais wao aingie madarakani kwa kumchangia fedha, ili atakapoingia madarakani watafute namna ya kuziba pengo la fedha walizotoa.
    “Mabadiliko ya Watanzania si ya vyama vya siasa bali ni ya kufanya kazi…kwa Watanzania wote, hatujamleta Magufuli kwa ajili ya kujaza nafasi, wala hatujamleta kupokea kijiti tu,” alisema Mwigulu.
    Mwigulu alisema, ni kweli Mwalimu Julius Nyerere alisema mabadiliko yasipopatikana ndani ya CCM watayapata nje, ndiyo maana ameletwa Magufuli ili mabadiliko yatoke ndani ya chama hicho tawala. Akizungumzia malalamiko ya watu kuhusu kudhulumiwa haki zao wakiwamo wafanyakazi, Mwigulu alisema wanaohusika kufanya hivyo si wana CCM kwani watumishi hawaingii serikalini kwa kadi za chama.
    “Ukikuta kuna eneo watu wanalalamika kuhusu haki zao, ujue halijafanywa na wana CCM…hata serikalini hawaingii kwa kadi za CCM bali ni Watanzania. Tumewaletea Magufuli ni kiboko ya wazembe,” alisema Mwigulu. Mwigulu ambaye aliasa Watanzania kuacha kuchagua kwa ushabiki wasije kupeleka watu wenye ajenda tofauti, alisema Magufuli ni mgombea pekee anayeweza kusimama na kusema atapambana na rushwa.
    “Mtanzania anayetaka kuitendea haki nafasi yake na Taifa kwa ujumla, atampigia Magufuli…,” alisema na kusisitiza kuwa nia na madhumuni yake ni kutumikia Watanzania. Aliendelea kuhadharisha watu wanaochangishana ili kumweka rais madarakani akisema, kitakachofuata ni kujaza mashimo ya fedha zao.
    Kwa upande wake, Makamba alisema, ili kutendea haki Taifa na wananchi wake, Watanzania wanapaswa wamchague Magufuli. Aliwataka wanawake wasisikilize wala wasikubali vitisho kwamba siku ya uchaguzi kutakuwa na vurugu, ili washindwe kupigakura.
    Aliwahakikishia kwamba vyombo vya dola viko imara na hakuna wa kuizidi nguvu Serikali. Kwa mujibu wa Makamba, katika uchaguzi huu, vipo vibao viwili; kimoja kikiwa kimeandikwa amani, utulivu, maendeleo, mshikamano, umoja ambacho alisema ni cha CCM kinachopaswa kuchaguliwa.
    Alitaja kibao kingine kuwa ni kilichoandikwa vurugu, chuki, utengano, fujo, udini, ukanda ambacho alisema wanapaswa waepukwe wasichaguliwe. Mjumbe mwingine wa Kamati ya Ushindi, Nyalandu, alisema moyo wa mgombea wa CCM uko karibu na Watanzania wanyonge.
    Alisema Tanzania ya Magufuli anayoiona ni itakayojali watu wote wakiwamo wazee, vijana, wanawake na wanafunzi. “Magufuli ndiye mabadiliko ambayo yanahitajika,” alisisitiza.
    Akiwasihi wananchi kumpigia Magufuli kura, alisema “saa ya Tanzania kuona matumaini yake imefika…nauona moyo wa Magufuli uko karibu sana na Watanzania.” Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji, akimwombea kura Magufuli pamoja na mgombea ubunge, alisema dhamira yake ya kusaidia wana Singida ni ya kuzaliwa na si lazima awe kiongozi.
    Aliwaahidi kuwa atashirikiana bega kwa bega na mbunge wa CCM atakayechaguliwa kuendeleza maendeleo Singida Mjini. Alimwombea Magufuli kura na mgombea ubunge wa Singida Mjini, Musa Sima, akisema atashirikiana nao kujenga nchi.

    chanzo Gazeti la HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment