CHAMA cha Democtratic Party (DP) kimesema kimesikitishwa na mazingira
yaliyosababisha kifo cha Mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji
Chrisopher Mtikila. Taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwenye vyombo vya
habari na Naibu Katibu Mkuu wa DP upande wa Tanganyika, Abdul Mluya
ilidai kuwa kifo cha kiongozi huyo kinaonesha mazingira ya utata.
“Tumeshitushwa sana na msiba huu ambao mazingira yake yana utata
mkubwa na sisi kama chama hatuelewi kilichotokea lakini tuna imani kuna
mipango ya watu waliohusika,” alidai Mluya. Alisema chama hicho
kinaiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina, hata ikiwezekana vyombo
vingine vya usalama vya kimataifa, kusaidia katika kubaini nini
kilichosababisha kifo hicho.
Mluya alisema vitu vinavyofanya wasiamini mazingira ya kifo hicho ni
pamoja na picha zilizopigwa na kuwekwa kwenye mtandao, mara tu baada ya
tukio la ajali kutokea kuwa zinatia shaka kuwa kuna mtu alikuwa
amejiandaa eneo, ambapo walipanga ajali itokee.
“Ajali ni ya kupangwa, haiwezekani picha za ajali zinaonesha kama
marehemu tayari alishapatiwa huduma ya kwanza wakati waliokuwa naye
wamesema wao ndio waliomhudumia na hakuna aliyempiga picha kati yao,”
alihoji Mluya.
Aidha, alisema kutokana na ushujaa wa kiongozi wao, wataendeleza kazi
zote ambazo Mchungaji Mtikila alikuwa akizifanya na hivyo yale ambayo
alitarajia kuyatekeleza, yatatimia kama ndoto zake zilivyokuwa.
Kwa upande wake, Mchungaji Patrick Mgaya ambaye ni miongoni mwa
abiria waliokuwemo ndani ya gari lililopata ajali, alisema kifo cha
ajali hii kina utata mkubwa huku akieleza namna ambavyo mazingira yake
yalivyokuwa.
Alisema wakati wanaendelea na mkutano wa kampeni huko Njombe,
pikipiki iliyokuwa na bendera mbili za vyama tofauti vya siasa,
ilikatisha mbele ya mkutano na kuondoka. Mara baada ya kuondoka,
waliendelea na mkutano hadi ulipoisha, kisha wakaondoka na kwenda kupata
chakula eneo jirani na walipokuwa wakifanyia mkutano, ambapo walipita
wafuasi wa vyama vingine vya siasa na kuwauliza, ni muda gani wataondoka
kuelekea Dar es Salaam.
“Hiki kifo mimi sikielewi hata kidogo kwasababu kinaonesha dhahiri
kuna watu walipanga na kuamua kutekeleza ajali hii kwa mbinu zao wenyewe
ikiwemo za kishirikina,” alidai Mgaya. Mgaya aliendelea kueleza kuwa,
walipomaliza kupata chakula, waliondoka na kuanza safari ya kurejea
jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya muda mfupi, walipata ajali na
kuligonga gari lililokuwa mbele yao kutokana na ukungu mkubwa, uliokuwa
mbele yao na taa za gari lao zilizimika.
Mara baada ya ajali hiyo, walikwenda Kituo cha Polisi kilichokuwa
jirani yake na kufanikiwa kutatua tatizo hilo, kisha kuendelea na safari
yao ya kurudi jijini Dar es Salaam. Alidai walipoanza kuondoka maeneo
ya Njombe, kwa nyuma waliona gari lililokuwa likiwafuata kwa nyuma
ambalo lilikuwa aina ya Toyota Land Cruiser ya rangi ya kijivu, ambalo
hakuweza kuzishika namba zake za usajili.
Alidai gari hilo lilikuwa linakuja kwa kasi nyuma yao hadi likawapita
kwa mbele, lakini hatua chache baadaye na gari yao pia ilifanikiwa
kulipita na kutangulia mbele. Mgaya alidai kuwa magari hayo mawili
yaliendelea kukimbizana kwa kasi huku Mchungaji Mtikila akimwambia
dereva apunguze mwendo, kwani kasi anayoendesha sio nzuri.
Mgaya alisema walipofika njiani maeneo ya Mikumi, walishuka kuchimba
dawa na yeye Mgaya kumshauri Mchungaji kuwa wasubiri kama nusu saa hivi
ili gari ile ambayo wana shaka nayo iweze kutangulia zaidi na wasiifikie
kwa haraka au wasiikute. Baada ya muda wa nusa saa kupita, walianza
safari huku wakimsihi dereva apunguze mwendo.
Alidai kuwa walipokuwa wakiendelea na safari, ghafla lile gari
walilokuwa wakifukuzana nalo, waliliona likiwa nyuma yao huku likija kwa
kasi kubwa na kuamua kupisha lipite, hivyo likawa mbele yao. Alisema
safari liliendelea huku magari yote yakiwa kwenye mwendo wa kasi na
walipofika karibu na kituo cha mafuta gari lao, lilipita na kuongeza
mafuta kisha kuendelea na safari.
Walipofika mbele kidogo, waliliona hilo gari likiwafuata tena na
kuamua kuongozana nalo hadi walipofika mbele na kukuta gari aina ya lori
likiwa limepaki pembezoni mwa barabara. Katika kulipita hilo gari,
Mgaya alidai gari lililokuwa mbele yao aina ya Land Cruiser, ambalo
lilitokea awali lilikuwa mbele ndio ilipaswa kugongana na lori hilo,
lakini lilifanikiwa kupita ndio dereva wao aliamua kupeleka gari porini
na kuanguka.
Mgaya alidai mara baada ya ajali hiyo, alipozinduka alimuuliza dereva
Mchungaji yupo wapi. Alidai Mchungaji alikandamizwa na gari kifuani na
walipata msaada kutoka kwa wasamaria, kulisukuma gari lililopata ajali
na kumuondoa huku akiwa tayari amefariki.
Maziko Mwili wa marehemu utaagwa leo katika viwanja vya Karimjee
kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba na kisha kusafirishwa hadi
kijijini kwao Milo wilayani Ludewa mkoa wa Njombe kwa ajili ya maziko
siku ya leo au kesho.
Mtikila alifariki kwa ajali ya gari maeneo ya Msolwa wilayani
Bagamoyo kwa ajali ya gari aina ya Toyota Corolla, lenye namba za
usajili T 189 AGM, akitokea Njombe kuelekea jijini Dar es Salaam.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment