Na Ahmed Makongo, Mwibara
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Mwibara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Kangi Lugola, amemshambulia kwa maneno makali mgombea urais wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kuwa umati
wa watu wanaofurika kwenye mikutano yake haumaanishi kumkubali isipokuwa
una sababu zaidi ya hiyo.
Lugola aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea
mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Uwanja wa Kata
ya Kisorya katika Jimbo la Mwibara, mpakani mwa wilaya ya Bunda na
Ukerewe iliyoko Mkoa wa Mwanza.
Lugola alisema watu wasishangae umati mkubwa anaoupata Lowassa kwenye
mikutano yake ya kampeni kwa sababu wananchi wengi sio kwamba
wanamkubali bali wanakwenda kuangalia na kushangaa mambo mengine.
Alisema wakati wa mchakato wa kuomba ridhaa ya kugombea urais ndani
ya CCM alishawishiwa na aliowaita wapiga debe wa stendi kumuunga mkono
Lowassa na kupanda basi lake ambalo lilikuwa bovu.
“Watu watasema kwamba mbona nilikuwa kwake, unajua wapiga debe hao ni
watu hatari sana, ni kama hao wa kwenye hiace, ukifika hapo stendi
watakuvuta huku na huku wakisema gari zuri ni hili…..sasa nilipanda basi
la Lowassa, kufika njiani likaharibika nikapanda basi zima la Dk. John
Pombe Magufuli na sasa ninakwenda nalo mbele kwa mbele,” alisema Lugola.
Lugola alisema kiongozi anayefaa kuwa rais kati ya wagombea wote
wanane wa nafasi hiyo ni Dk. Magufuli, kwa sababu afya yake ni imara na
pia anao uwezo mkubwa wa kuwa kiongozi mkuu wa nchi hii.
Chanzo Gazeti la Mtanzania.
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment