Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa Uchaguzi nchini Jaji Mstaafu Damian
Lubuva, ameeleza kushangazwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya vyama
vya siasa wakiwahamasisha wafuasi wao hasa kundi la vijana kubaki
vituoni ili kulinda kura.
Kauli hiyo ya Lubuva ambayo aliitoa Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari inaonekana kumjibu Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Akihutubia mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam juzi katika
viwanja wa Kawe, Mbowe aliwataka wanachama na wafuasi wao kubaki vituoni
siku ambayo watapiga kura ili kuzilinda zisiibiwe.
Hata hivyo, Jaji Lubuva alisema kauli hiyo inajenga mazingira ya kuleta fujo nchini.
“Nashangazwa na kauli hizo kwa sababu Tume tulishasema kwamba mfumo
tulioandaa ni mzuri na umeboreshwa kwa kuzingatia maoni yao… inakuwaje
tena wanaendelea kuwahamasisha wafuasi wao hasa vijana wabaki vituoni
kulinda kura kwanini… mawakala wapo kwa ajili gani,” alihoji.
Jaji Lubuva alisema NEC inasisitiza watu watakaokuwa wamekwisha
kupiga kura kuondoka vituoni kwani endapo vijana watabaki kuna uwezekano
wengine wakapata hofu ya kwenda kupiga kura.
“Ndio maana tunawataka waondoke lakini hawa wanasiasa wanaosema
wabaki kulinda kura huenda wana ajenda yao maana wasiwasi wa nini,”
alihoji Jaji Lubuva.
Aliwataka watazamaji wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu katika kipindi chote cha usimamizi bila
kufungamana na upande wa chama chochote cha siasa.
Aliwataka wanawake nchini kuhimiza amani kipindi hiki cha uchaguzi
kwani wana nguvu kubwa ya ushawishi ambayo inaweza kuzuia vurugu
zisitokee.
Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa mada katika semina
iliyowakutanisha NEC na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake
nchini Kaimu Mkurugenzi wa Sheria NEC, Emmanuel Kawishe, alisema NEC
imejipanga kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu kwa kuhakikisha unakuwa huru
na haki.
“Tumeandaa mfumo mbadala ujulikanao kama ‘Spreadsheet Excel RMS’
ambao utatumika kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yatakayojitokeza
katika zoezi la ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi,” alisema.
Kawishe alisema mfumo huo utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo ulioandaliwa.
“Tume imeandaa mfumo wa menejimenti ya matokeo (Result Management
System) ambao utatumika kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu
yanayoweza kutokea kwa bahati mbaya katika ujumlishaji wa matokeo.
“Kasoro au makosa hayo ni kama ujumlishaji wa kituo kimoja mara
mbili, kukosea uandikaji wa 7 badala ya 1, usahihi wa ujumlishaji na
mengineyo, mfumo huu si mgeni kwani ulitumika katika uchaguzi wa 2005 na
2010.
“Kwa uchaguzi wa mwaka huu, tumefanya uboreshaji na kuondoa mapungufu
katika maeneo yote yaliyokuwa na changamoto 2010 na tumeandaa mfumo huu
mbadala ambao utatumika kama huu uliopo utakuwa na changamoto,”
alisema.
Alisema katika usimamizi wa zoezi la uchaguzi tume imepata changamoto
ikiwamo ya kufariki kwa baadhi ya wagombea pamoja na kuongezwa kwa
mipaka ya kiutawala ambayo imeanzishwa baada ya kutangazwa kwa majimbo
mapya.
“Kuna baadhi ya kata mpya zimeanzishwa ambazo ni Ifakara, Bariadi,
Kishapu na Bulyanhulu wakati Tume ikiwa tayari imetangaza majimbo, hivyo
zipo katika tishio la kutopiga kura lakini suala hilo
linashughulikiwa,” alisema.
Chanzo Gazeti la Mtanzania
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment