Na Esther Mbussi, Zanzibar
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali
Mohamed Shein, ameahidi kutoa kompyuta na kuongeza idadi ya walimu wa
masomo ya sayansi katika shule za sekondari Kusini Unguja.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni eneo la Paje, Kusini Unguja Dk.
Shein alisema kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya sayansi kutasaidia
kuongeza ufaulu wa masomo hayo.
“Serikali itaboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule na tayari
tunamalizia shule 22 tulizoanza kujenga mwaka jana. Tumefanikiwa
kutekeleza ahadi zetu tulizoahidi, tuliahidi maji tumefanikiwa lakini
hapa Paje kwa bahati mbaya wafadhili wetu hayajakamilisha ila jitihada
za kuleta maji Paje zinaendelea,” alisema Dk. Shein.
Kuhusu uchimbaji wa mafuta na gesi, Dk. Shein alisema wamekubaliana
na Rais Jakaya Kikwete kuwa Tanzania Bara iendelee kuchimba mafuta yake
na Zanzibar itachimba ya kwake.
“Aidha, tulikubaliana Zanzibar tutunge sheria yetu wenyewe, tayari
tumeshaandaa na rasimu iko tayari, nitakaporudi nitachimba mafuta ndani
ya miaka mitatu,” alisema Dk. Shein.
Awali, aliyekua Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Shamsi Vuai Nahodha, alisema anawashangaa viongozi wa Chama cha
Wananchi (CUF) kulalamika kuwa Serikali haitoi ajira wakati Wizara ya
Ajira ilikua chini ya uongozi wao.
Alisema katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Wizara za Ajira,
Biashara, Utalii, Viwanda, Viwanja vya Ndege na Barabara zilikuwa
zinasimamiwa na mawaziri wa CUF.
“Anapotokea mpinzani anayesema Serikali ya CCM haitoi ajira huyo
apimwe akili… ningekuwa mimi ndiye Maalim Seif ningewaita mawaziri wangu
nikawauliza kimetokea nini lakini wao kila mtu ni kulalamika tu,
haijulikani kiongozi nani.
“Ukiwauliza kwanini mnashindwa wanasema sera inayotekelezwa ni ya
CCM, lakini kazi ya upinzani ni kutoa mawazo na kutengeneza sera
mbadala, binafsi nilichokitegemea kwa wenzetu hao kimekuwa tofauti,”
alisema Vuai.
Created in Gazeti la Mtanzania
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment