Basili Mramba akishuka katika gari la polisi. |
JAJI Projest Rugazia wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
ameelezea kushangazwa na sheria za Tanzania, kwa kutoa adhabu ndogo kwa
mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, ikilinganishwa na kiasi
cha fedha walichosababisha hasara. Jaji Rugazia alisema hayo wakati akiwapunguzia adhabu mawaziri hao kutoka kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni tano hadi kifungo cha miaka miwili jela. “Nashangaa sheria zetu, mtu anaweza kusababisha hasara ya fedha nyingi, halafu anatoa faini ndogo na kuishia hapo...lakini nawaachia waheshimiwa wanaotunga sheria,” alisema wakati akifafanua adhabu zinazotakiwa kutolewa kutokana na kosa hilo. Aidha, aliwafutia shitaka moja la kuisababisha Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 na adhabu iliyotolewa kutokana na kosa hilo. Hata hivyo, kosa hilo limeonekana katika mashitaka mengine. Jaji Rugazia alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia na kuchambua hoja za pande zote katika rufaa mbili, zilizowasilishwa na mawaziri hao pamoja na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Katika rufani hizo, Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, waliwasilisha hoja tano kupinga hukumu iliyotolewa Julai 6, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na jopo la Mahakimu watatu, likiongozwa na John Utamwa. Aidha DPP alipinga adhabu waliyopewa mawaziri hao kwa madai ni ndogo, hakimu alikosea kumuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja na pia iliiomba mahakama iamuru washitakiwa walipe fidia ya fedha walizosababisha hasara. Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Rugazia alikubali hoja ya kina Mramba kuwa walipewa adhabu mbili kwa kosa moja. “Haikuwa sahihi kuwashitaki kwa kosa la kusababisha hasara wakati kosa hilo lilishakuwa kwenye makosa mengine ambayo ni la tano hadi la 10,” alisema. Aidha, alisema Yona aliunganishwa kimakosa katika shitaka hilo, hivyo alifuta shitaka hilo pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni tano iliyotokana na kosa hilo. “Ninaondoa shitaka la kusababisha hasara, ninafuta adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni tano, hivyo Yona na Mramba watatumikia kifungo cha miaka miwili kwa kila kosa,“ alisema. Adhabu hizo ni Kifungu cha 96 (1) cha Kanuni ya Adhabu, ambapo adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka miwili jela, au Kifungu cha 284 (c) ambacho adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni tano. Katika uamuzi huo, Jaji Rugazia alisema, “Nakubali Kifungu cha 6 cha Kanuni ya Adhabu kinachotaka mahakama itoe amri washitakiwa walipe fidia, lakini siwezi kutoa amri hiyo.” Aidha, alikataa hoja za kina Mramba kuwa hati ya mashitaka ni batili, pia alisema hakukuwa na njama zozote kwa upande wa Jamhuri kutoita mashahidi waliosaini mkataba huo ili kuathiri upatikanaji wa haki, kwa kuwa utetezi walikuwa na haki ya kuomba watu hao wawe mashahidi wao. Alisema wasitumie maelezo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuficha kosa kwa kuwa alitoa maelekezo kutokana na barua aliyoipata kutoka kwa Mramba na hakujua kama tayari Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilishatoa angalizo la kutokutoa msamaha huo. Kwa upande wa Mgonja, Jaji Rugazia alisema anahalalisha kuachiwa kwake huru baada ya kutopatikana na hatia. Alisema, “Siwezi kuilaumu mahakama kwa kumuachia huru”. Katika hukumu hiyo, mawaziri hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh milioni tano, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7. Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008, wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza. Created by Gazeti la HabariLeo |
0 comments:
Post a Comment