Mgombea Urais wa CC, Dk John Magufuli. |
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC), limemrahisishia kazi ya kutoa fedha kwa Tanzania ya kusambaza umeme, hivyo hakutakuwa na ugumu katika usambazaji umeme.
Dk Magufuli mwenye historia ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya barabara nchi nzima, alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni, aliofanya mjini Bahi mkoani Dodoma.
Kauli hiyo ya Dk Magufuli na nyingine ambazo amekuwa akitoa katika kampeni zake, zinazoingia katika mkoa wa Singida ambao ni wa 17 sasa, zimeonesha tofauti ya ahadi anazotoa kwa wananchi na zile zinazotolewa na mgombea wa urais wa Chadema, aliye chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa.
Tofauti kubwa imejionesha katika ahadi za Dk Magufuli, kwa kutambua na kuahidi kudumisha na kuendeleza kazi zilizofanywa na viongozi wa awamu zilizomtangulia na zinazoendelea kufanyika katika Awamu ya Nne inayoishia ukingoni.
Kwa upande wa Lowassa, yeye na wapigadebe wake wamekuwa wakionesha kwamba hakuna kilichofanyika katika miaka 54 iliyopita tangu nchi ilipopata Uhuru, wala kinachofanyika katika uongozi wa sasa.
Hata katika umeme, hawasemi kuwa kwa sasa Watanzania wanaopata nishati hiyo ni asilimia 46 kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005, kutokana na jitihada za Serikali kwa kutumia fedha za ndani na nje, ambazo sasa zimeongezewa nguvu na fedha za MCC.
Kazi ya JK
Kauli ya Dk Magufuli kushukuru MCC kwa kurahisishia kazi akichaguliwa na wananchi kuongoza Tanzania, imeonesha namna anavyokubaliana na kazi zinazoendelea kufanywa na Rais Jakaya Kikwete, ambaye Magufuli amekuwa akimuita mzee mtarajiwa.
Mwanzoni mwa wiki hii, Rais Kikwete akiwa nchini Marekani, kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika moja ya ziara ambayo vyama vya Ukawa vimekuwa vikiipinga, alikutana na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J.
Hyde na watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Makamu wa Rais wa Operesheni za Shirika hilo, Kamran Khan. Ni katika mkutano huo, ndipo MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka katika shirika hilo, ambapo kuanzia mwakani wakati Rais Kikwete akiwa ameshastaafu, Serikali itaanza kupokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi ya Sh trilioni moja za Tanzania.
“Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania, imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati kupambana na rushwa,” Hyde alimwambia Rais Kikwete na viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Yusuf Omar Mzee.
Matokeo yake
Katika awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya awamu ya kwanza ya fedha za MCC. Kutokana na hatua ya kukubaliwa kupata awamu ya pili ya fedha hizo, Tanzania itakuwa imepata jumla ya shilingi za Tanzania trilioni 2.45 za awamu zote mbili kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutoka nchi hiyo katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita.
Katika awamu ya kwanza, fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea- Mbinga. Fedha hizo pia ndizo zilizotumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro; na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani; na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
Kauli za Lowassa
Baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Lowassa ni pamoja na kufuta ada na michango ya wanafunzi shuleni, ambayo pia Dk Magufuli amekuwa akiitoa.
Tofauti yao iko katika kuonesha hali halisi ilivyo, ambapo Dk Magufuli amekuwa akionesha kuwa awamu za uongozi zilizopita zimefanya kazi, ikiwemo Awamu ya Nne, ambayo imeweka mazingira wezeshi katika Bajeti ya Serikali ya 2015/2016 ya elimu iliyopitishwa mwaka huu, kuwa huduma hiyo iwe bure kuanzia Januari mwaka 2016.
PAYE
Pia Lowassa amekuwa akitoa ahadi za kufuta au kupunguza kodi ya mshahara kwa wafanyakazi (Paye), ahadi ambayo pia Dk Magufuli amekuwa akiitoa, lakini tofauti ikiwa katika kuonesha kilichofanyika katika awamu zilizopita.
Kwa mfano katika Paye, Serikali ya Awamu ya Nne inayomaliza muda wake, mwaka 2005 ilikuta kodi hiyo ni asilimia 18, ikapambana kuishusha hadi kufikia asilimia 11 mwaka huu.
Mbali na kushusha kodi hiyo, pia Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani, ilikuwa mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000 na ndio uliokuwa ukikatwa kiwango hicho cha kodi, lakini kazi ikafanyika na kupandisha mshahara kima cha chini mpaka Sh 300,000 mwaka huu, huku kodi yake ikishushwa.
Afya
Katika afya, Lowassa amekuwa akiahidi kuwa atahakikisha kunakuwa na uhakika wa dawa na vifaa vya uzazi, huku Dk Magufuli akisisitiza kuwa itakuwa marufuku hospitali za Serikali kukosa dawa.
Tofauti imekuwa ikijionesha kwa Dk Magufuli, kwani amekuwa akionesha namna viongozi waliomtangulia walivyofanikisha huduma ya afya kuwa bora na kuahidi kuanzia hapo. Kwa mfano, Dk Magufuli amekuwa akiahidi kujenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata, hospitali ya wilaya kila wilaya na hospitali ya rufaa kila mkoa.
Ahadi hiyo ni katika maeneo yaliyokosa huduma hizo, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne, kati ya mwaka 2005 na 2014 ilijenga vituo vya kutolea huduma za afya 2,175, kati ya hivyo hospitali ni 19, vituo vya afya 168 na zahanati 1,883 nchi nzima.
Katika ubora wa vifaa anaouzungumzia Lowassa, Serikali ya Awamu ya Nne iliimarisha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali za rufaa za Kanda, mikoa na wilaya kwa kuzipatia vifaa vya tiba na uchunguzi (MRI, CT Scan, X ray, Ultra Sounds na vingine vya maabara.
Mbali na hivyo, pia Serikali imejenga Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ambayo inatumika kuwa Maabara ya Kimataifa ya Rufaa kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).
Matokeo ya jitihada hizo na zingine ni kupungua kwa maambukizi ya malaria, ugonjwa unaoua zaidi nchini kwa asilimia 51 na kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kwa asilimia 71.
Aidha, wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 49 mwaka 2005 hadi miaka 62 hivi sasa, huku vifo vya watoto wachanga vikipungua kutoka vifo 68 kwa kila vizazi hai 1,000 hadi vifo 21 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2014.
Wilaya mpya Katika hatua nyingine, Dk Magufuli akiwa Bahi, moja ya wilaya mpya alisema atakapoingia madarakani, watumishi na watendaji ambao wamepangiwa kazi katika wilaya mpya lakini hawaishi kwenye vituo vyao, watalazimika kuchagua ama kuishi mjini bila kazi au kuhamia na kuendelea na kazi.
Magufuli amesisitiza zaidi walio kwenye mamlaka ya rais ya uteuzi, akiwemo Mkuu wa Wilaya, lazima watii, vinginevyo wataachishwa kazi. “Haiwezekani ukawa na wilaya halafu viongozi wanalala Dodoma mjini,” alisema na kusisitiza kuwa ni lazima wakae hapo, hata kwa kupanga nyumba.
Akisisitiza viongozi na watendaji walio kwenye mamlaka yake ya uteuzi kutii, alisema, “najua viongozi mnanisikia.”
Created by Gazeti la HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment