NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya MTANZANIA,
RAI, Bingwa, Dimba na The African, imelaani vikali, uzushi, uongo na
upotoshaji wa hali ya juu unaofanywa na watu wasio na nia njema na
kampuni hiyo.
Watu hao juzi walitengeneza mfano wa gazeti la RAI lenye ujumbe
hasi na kulisambaza katika mitandao ya kijamii, likiwa na taarifa
mbalimbali za uongo na uzushi ambazo haziuhusu uongozi wa kampuni hiyo
na magazeti yake kwa ujumla wake.
Akizungumzia hali hiyo mjini Dar es Salaam jana, Mhariri Mtendaji
Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda
amesema ameshtushwa na hatua hiyo, lakini akawataka wasomaji na
wafuatiliaji wa gazeti halisi la RAI kulipuuza gazeti hilo feki.
Alisema gazeti hilo linalosambazwa katika mitandao ya kijamii
halina maana yoyote, kwani watu wanaofanya hivyo wamelenga kulichafua
gazeti halisi kwa maslahi binafsi.
Alisema hiyo ni mara ya pili kwa watu hao wenye nia ovu na gazeti
hilo, kutengeneza mfano wa gazeti la RAI na kulisambaza katika mitandao
ya kijamii.
“Tumeshtushwa na hatua hii ya kurudia uovu wao, tulipoona kwa
mara kwanza wametengeneza gazeti feki la RAI ambalo lina sura
inayofanana na gazeti letu halisi na kuliweka katika mitandao ili
kuwaaminisha watu kuwa gazeti linaloenda sokoni ndio lile ambalo
lilikuwa na habari ambazo ni potofu zenye mwelekeo wa
uchochezi, tulipuuza.
Hata hivyo wahusika wa uovu ule wa awali tuliwabaini.
“Watu hawa, wameurudia tena, sasa niseme inatosha, napenda kuwaambia
wasomaji wa gazeti la RAI ambalo huchapwa kila Alhamisi kuwa, gazeti
linalowekwa kwenye mitandao ya kijamii si gazeti halisi la RAI
wala habari zile hazijawahi kuandikwa na RAI hata mara moja.
“Na hata ukizisoma habari zilizomo kwenye gazeti
linalosambazwa mtandaoni zimetawaliwa na dhamira ya kulipaka matope
gazeti halisi la RAI, wahariri na waandishi wake kwa malengo ambayo
hatujayajua.
“Katika uchunguzi wetu tuliofanya baada ya gazeti feki
kuwekwa mitandaoni kwa mara ya kwanza, tuliona kazi hiyo haramu
inafanywa katika chumba kimoja cha habari ambacho watendaji na wahariri
wake wana mrengo fulani wa kihabari.
Tulikaa kimya wakati ule wa kwanza kwa maana tuliamini wangejifunza kutokana na upuuzi wao.
“Lakini baada ya kuona wamerudia, tumeona kuna wajibu wa
kuwajulisha wasomaji wetu ambao baadhi wanaingia kwenye mitandao
ya kijamii kabla ya kusoma magazeti, kwamba kile ambacho
wanakiona kwenye mitandao si gazeti halisi la RAI, gazeti la RAI
linatoka kila siku ya Alhamisi ya kila wiki hata habari zinazowekwa
kwenye gazeti hilo feki si za Alhamisi.
“Kutokana na hali hiyo tunaangalia namna bora ya kuwasiliana
na mamlaka husika za kiserikali ili kupata njia sahihi ya
kuwashughulikia hawa wanaokiuka sheria ya mitandao,” alisema.
Kibanda amewataka watu hao wenye nia ovu na kampuni ya New Habari
(2006) Ltd, kuachana na mikakati yao hiyo miovu kwani haitawasaidia
kufanikisha malengo yao.
Created by Gazeti la Mtanzania
Wednesday, 7 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment