MIPANGO miji ni sehemu muhimu katika kufanya mji kuwa na mandhari inayovutia na salama kwa ustawi wa wakazi wa eneo husika.
Miji iliyopangwa vizuri, mara nyingi huiokoa jamii isikumbwe na majanga
ambayo yanazuilika iwapo kuna miundombinu inayopitika kwa urahisi.
Tunashuhudia miji ya mataifa mengine duniani ikiwa kwenye ubora
unaotakiwa, kimsingi hiyo ni kutokana na kupangwa vizuri kupitia
wataalamu wa mipango miji wa nchi husika.
Lakini suala hilo kwa nchi yetu limekuwa tofauti ambapo makazi mengi yamejengwa holela, bila kufuata mpangilio wowote.
Kutokana na Watanzania kutozingatia suala la mipango miji juzi, Naibu
Waziri wa Nyumba na Makazi, Angela Kairuki amezungumzia suala hilo na
kueleza kuwa ramani za mipango miji (Master Plan) za Jiji la Dar es
Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Tanga imepitwa na wakati.
Kairuki anasema kuna kila sababu ya wataalam kuangalia upya njia ya
kubadilisha miji hiyo. Katika majiji hayo bado tunashuhudia kila kukicha
ujenzi unaendelea bila kufuata mipango miji hali ambayo inachangia
kutokea matatizo ambayo yangezuilika.
Tunaamini kuwa iwapo kauli ya naibu waziri itafanyiwa kazi changamoto zilizopo sasa nchini zitapungua kama si kumalizika kabisa.
Hivyo umefika wakati sasa kwa kila mtu atumie nafasi yake ipasavyo ni
dhahiri hakutakuwa na upungufu katika mipango miji kama inavyotokea kila
mara huku wataalamu wakiwa wapo maofisi.
Umefika wakati sasa kwa wahusika wote kuanzia ngazi ya chini kuangalia
upya suala hilo kwa kina ili kuepusha mambo ambayo yanaepukika kwani ni
hasara kubwa ambayo inapatikana kwa makosa ya wataalamu wetu.
Mfano jijini Dar es Salaam kila kunapotokea janga la moto wananchi au
mamlaka husika na uzimaji moto haifanikiwi kuzima kutokana na upungufu
wa mipango miji mbovu uliopo.
Ni vema sasa kutafakari kwa kina kuhakikisha kuwa miji yetu inakuwa
katika mpangilio ili kuepusha majanga kama mafuriko na ajali za moto
ambazo zikitokea ni vigumu kukabili janga hilo kwa urahisi.
Tunaamini kuwa miji iliyopangwa vizuri inasaidia kuondoa msongamano wa
magari barabarani hususan katika miji inayokua kwa kasi. Pia, husaidia
kuondokana na maradhi mbalimbali ikiwamo malaria na magonjwa ya mlipuko
kama kipindupindu.
Aidha, itawezesha magari ya zima moto kufika kwa urahisi katika eneo
ambalo limekumbwa na janga la moto. Hivyo ni vema sasa mipango miji
ikajipanga upya ili kuhakikisha majiji na vijiji vinakuwa na muonekano
mzuri.
Chanzo Habari mambalimbali
Tuesday, 6 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment