Mchekeshaji aliyeongeza kwa kuimba muziki
Stella Kessy
JINA la Kinyambe si geni kwa mashabiki wa filamu za kibongo hasa wale wanaopenda wachekeshaji.
Kinyambe amekuwa akifanya sanaa inayomtofautisha na wachekeshaji
wengine wa nchini, ana kipaji halisi cha kuzaliwa na kwa kipindi kifupi
tangu aanze kuuonekana kwenye runinga amejijengea jina kubwa miongoni
mwa waigizaji wa Tanzania.
Jina halisi la Kinyambe ni Mohammed Abdallah au James, mbali ya
kuigiza ana kipaji cha kuimba muziki wa kizazi kipya, pia amemgeukia pia
Mungu akiimba nyimbo za Injili.
Kinyambe anasifika kwa kuigiza kama ‘zoba’ akiwa na uwezo wa
kuyageuza macho yake kama kinyonga, anasema anaamini kuimba kwake muziki
wa Injili ni kama njia ya kumshukuru Mungu.
“Nimewatumikia wanadamu kwa muda mrefu, sasa ni zamu ya kumtukuza
Mungu na lengo langu ni kufika mbali katika fani zote zinazofanya
kuanzia kuigiza, kuchekesha na kuimba,” anasema.
Kinyambe aliyewahi kutamba katika kipindi cha ‘Vituko Show’ na
kupitia filamu mbalimbali za komedi anatamba na wimbo wa ‘Acha ya Dunia’
aliomshirikisha mwimbaji wa kwaya ya KKKT Makongolosi Chuya mkoani
Mbeya, Mederick Sanga.
Kinyambe anafichua mchanganyiko wa majina yake kwa maana ya Mohammed
na James inatokana na kuzaliwa na wazazi wenye dini mbili tofauti, “Baba
yangu ni Mwislamu na mama ni Mkristo, ndiyo maana unaona nina majina
mawili ya dini tofauti. Najiona niko kotekote tu kwa sababu
ninayemwabudu ni Mungu tu,” anasema.
Ubunifu
Kinyambe anasema alibuni staili ya kuzungumza kama ‘zuzu’ na
kuchezesha macho kwa namna ya ajabu kama njia ya kutaka kusaka mashabiki
na kujitofautisha na wachekeshaji wengine.
“Niliamini bila ubunifu ni vigumu kuhimili ushindani, hivyo nikaibuka
na staili hiyo, nashukuru nimepokelewa vyema kiasi cha kujivunia,”
anasema.
Kinyambe anadai pamoja na kujifanyisha makengeza na kuyageuza macho
kila mara kama kinyonga, ukweli hana ulemavu wowote na wala huwa haumii
kama watu wanavyofikiria kwa sababu alianza kujizoesha hivyo kitambo.
Msanii huyo aliyevutiwa kisanii mwigizaji N!xau Toma maarufu kama
‘Bushman’, mwigizaji nyota wa Namibia aliyecheza filamu za ‘Gods Must Be
Crazy’, anasema kipaji cha sanaa ni cha kuzaliwa nacho kwani alianza
kuvunja mbavu watu tangu akiwa kinda.
“Nilipokuwa mdogo, hasa shuleni nilikuwa kipenzi cha wanafunzi
wenzangu kutokana na tabia ya kuwachekesha, pia nilijishughulisha na
sanaa ya uimbaji na uchoraji fani ninazoendelea nazo hata sasa,”
anasema.
Mafanikio
Kinyambe anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa maji na juisi tu,
anasema hana mafanikio ya kujivunia katika sanaa hiyo, zaidi ya kuwa na
jina kubwa na kulifafanua jina lake lina maana ya mkoba kwa lugha yao ya
kabila lake la kihaji la mkoani Mbeya.
“Sina cha kujivunia, ila nashukuru sanaa ilinipatia ajira Al Riyamy
na kunikutanisha na mastaa kadhaa waliosaidia kuinua kipaji changu,”
anasema.
Anawataja baadhi ya wasanii aliokutana na kuigiza nao ni Mzee Magari, Steven Kanumba, Jackline Wolper na wengine.
Msanii huyo mwenye ndoto za kufika mbali kisanii pamoja na kimaisha,
amewahi kutoa kazi zake binafsi ikiwamo; ‘Nyumba’, ‘Chumba cha Maiti’,
‘Polisi Feki’, ‘Fundi Kinyambe’ na ‘Fumbafu Thana’. Jina la filamu hiyo
ni msemo maarufu anaopenda kuutumia msanii huyo akimaanisha Pumbavu
Sana, kila anakopokuwa akitaka kukosoa jambo.
Muziki
Kinyambe aliyezaliwa mwaka 1985 Uyole mjini Mbeya akiwa mtoto wa
pekee wa kiume na wa tatu kati ya watoto saba wa familia yao pia ni
mkali katika muziki.
Baadhi ya nyimbo zake ni ‘Maumivu’ alioimba na Baguje, ‘Maimuna’
alioimba na Leila Tot na Erick Ivyoivyo na ‘Kiduku Mpapaso’
aliomshirikisha Kesse.
Tofauti na vijana wengi, Kinyambe anayemzimikia mkali wa zamani wa
Daz Nundaz, Ferooz, hana mzuka kabisa na mambo ya soka, akidai hana timu
yoyote anayoishabikia wala kufuatilia mchezo huo.
Safari yake ya sanaa ilianzia katika makundi tofauti yakiwamo Ufunguo
Sanaa, Greenwood na Mbeya Films na filamu alizocheza awali alipoingia
kwenye fani hiyo ni ‘Msitu wa Maajabu’, ‘Kiapo Changu’, ‘God is Great’,
‘Leathal Weapon, iliyomkutanisha na marehemu Steven Kanumba.
Kinyambe analia na wezi wa kazi za wasanii na kuiomba Serikali
iwasaidie pamoja na kuiwekea miundombinu itakayowawezesha wasanii
kunufaika na kazi zao, anasema fani ya filamu Bongo imepiga hatua kubwa
kwa sasa tofauti na awali.
Amesema kuwa anatarajia kufika mbali sana katika sanaa na kufanana na mwigizaji Rowan Atkinson maarufu kama Mr.Been.
stella_kessy@yahoo.com
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment