Sunday, 4 October 2015

Tagged Under:

Aliyeua watu 77 atishia kususia chakula hadi afe

By: Unknown On: 07:24
  • Share The Gag
  • OSLO, Norway
    MWANAUME aliyeua watu 77 nchini Norway ametishia kususia chakula hadi afe, akilalamika kwamba anateswa gerezani.
    Vyombo vya habari vinasema, Anders Behring Breivik anadai kutengwa kutoka kwa wafungwa wengine tangu Septemba 2, na kwamba huwa anaruhusiwa kutoka nje ya seli yake saa moja tu kwa siku.
    Breivik aliua watu 77 mwaka 2011, alipolipua bomu katikati mwa Oslo kabla ya kufyatulia risasi mamia ya vijana waliokuwa wamekusanyika katika Kisiwa cha Utoya nchini humo.
    Alihukumiwa kifungo cha miaka 21 jela 2012.
    Madai yake kwamba anawekwa katika hali mbaya ameyatoa kwenye barua aliyoandika na kuituma kwa vyumba vya habari vya Norway na Sweden.
    Kwenye barua yake, Breivik (36), anasema hali ngumu gerezani imemlazimisha kuacha kozi yake ya sayansi ya siasa aliyokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Oslo.
    “Kusoma na kufanya mawasiliano ni jambo lisilowezekana chini ya mazingira kama haya,” alisema kwenye barua.
    Breivik alisema hali ikisalia ilivyo, atasusia chakula hadi afariki dunia, kwa mujibu wa vyombo vya habari Norway.
    Mkurugenzi wa gereza la Skien anakozuiliwa Breivik, Ole Kristoffer Borhaug, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwa sasa hakuna mtu anayesusia chakula gerezani humo.
    Kwa mujibu wa gazeti la Dagbladet, Waziri wa Haki wa Norway, Anders Anundsen alikataa kuzungumzia madai hayo ya Breivik.
    BBC

    0 comments:

    Post a Comment