Sunday, 27 December 2015

Tagged Under:

Amani yatawala Maulid, Krismasi

By: Unknown On: 00:17
  • Share The Gag

  • IGP Ernest Mangu.

    WAKAZI wa maeneo mbalimbali hapa nchini wamesherehekea sikukuu ya Maulid na Krismasi katika hali ya amani, bila kuwepo na matukio makubwa ya uvunjifu wa amani.
    Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, makamanda wa Polisi wa mikoa ya kipolisi ya Dar es Salaam na Pwani, wamesema kuwa hakuna matukio makubwa yaliyoripotiwa katika sikukuu hizo.
    Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ilala, Lucas Nkondya akizungumza na gazeti hili alisema kwa taarifa alizonazo mpaka jana mchana hakuna tukio lolote lililoripotiwa ambalo liliashiria uvunjifu wa amani.
    “Kwa taarifa nilizonazo mpaka sasa huku kuko shwari kabisa hakuna tukio lolote kubwa lililotokea la uvunjifu wa amani, watu wamesherehekea vizuri,” alisema Kamanda Nkondya.
    Aidha alisema katika matukio yaliyoripotiwa ni kukamatwa kwa pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda 80 katika maeneo mbalimbali, ambao walipatikana na matukio ya uvunjifu wa sheria ya usalama barabarani.
    Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema pia kuwa hali katika sikukuu hizo ilikuwa ni shwari bila kutokea vurugu zozote kwa upande wa Kinondoni. Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema pia kuwa hakukuwa na tukio kubwa la uvunjivu wa amani isipokuwa matukio ya kawaida.
    “Siwezi kusema kuwa hakukuwa na tukio lolote la uvunjifu wa amani lakini hakukuwa na tukio kubwa kwa upande wa Pwani, matukio kama ugomvi, matusi haviwezi kukosekana,” alisema Kamanda huyo.
    Makamanda hao wamewaomba wananchi waendelee kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya katika hali ya amani kama ambavyo imefanyika kwa Krismasi na Maulid, ili nchi iendelee kuwa na amani.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment