Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MTANDAO wa Wanawake wa Katiba na Uchaguzi, umemwomba Rais Dk. John
Magufuli, kusimamia kikamilifu utekelezwaji wa mikataba mbalimbali
iliyosainiwa na Tanzania hasa ile ya usawa wa kijinsia ili
kupunguza pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50 katika nafasi
za uongozi.
Mikataba hiyo ni pamoja na Mpango Kazi wa Beijing (1995),
Mkataba wa Maputo, Mkataba wa Nyongeza wa Jinsia na Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC Gender Protocol) na Tamko la Umoja wa
Mataifa la Haki za Binaadamu la mwaka 1948.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji
wa TGNP-Mtandao, Lilian Liundi katika taarifa yake aliyotumwa kwa vyombo
vya habari, ambapo alisema hiyo ni kwa sababu kumekuwapo na idadi ndogo
ya wanawake wanaoteuliwa kuliko ile ya wanaume katika ngazi ya maamuzi.
“Tumefuatilia tangu wakati wa uchaguzi na wakati wa uteuzi wa
mawaziri, makatibu wakuu, manaibu na wakuu wa idara na taasisi
mbalimbali uliofanywa hivi karibuni na Rais Magufuli.
“Katika uteuzi huo kuna jumla ya makatibu wakuu na manaibu
katibu wakuu 50 idadi ambayo ni pungufu kidogo ikilinganishwa na
mwaka 2014 ambapo walikuwa 53,” alisema.
Alisema idadi ya makatibu wakuu imeongezeka kutoka 23 mwaka
2014 hadi 29 wakati manaibu katibu wakuu imepungua kutoka 30
mwaka 2014 hadi 21 mwaka huu.
Alisema hata hivyo kati ya nafasi zote 50 za walioteuliwa
wanawake wapo 10 tu idadi ambayo ni sawa na asilimia 20 ikilinganishwa
na wanaume ambao ni asilimia 80.
Alisema idadi ya makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu
wanawake imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo takwimu za mwaka
2014 zinaonesha walikuwa 20 sawa na asilimia 37.7 huku wanaume
wakiwa 33 sawa na asilimia 62.3.
Created by GAzeti la Mtanzania
Wednesday, 6 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment