TAMKO LA JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR (JUMAZA) KWA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA KIISLAM ZANZIBAR KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MGOGORO WA KISIASA ZANZIBAR TAREHE 6-1-2016 KATIKA UKUMBI WA UMOJA WA WALEMAVU
*****
Awali tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kukutana katika hafla
hii hali ya kuwa ni wazima; sala na salamu zimfikie Mtume wetu Mtukufu
Muhammad (S.A.W), jamaa zake, maswahaba zake na wote wanaowafuata kwa
wema hadi Siku ya Malipo.
Ndugu waandishi wa habari, tunawashukuru sana kwa kuitikia wito wetu wa
kuhudhuria katika mkutano huu muhimu wenye lengo la kutafuta maslahi na
mustakbali mwema wa nchi yetu.
Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislamu Zanzibar tunawashukuru sana
Wazanzibari wote kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu katika nchi
yetu pamoja na kukabiliwa na mtafaruku mkubwa wa kisiasa ambao haujawahi
kushuhudiwa katika historia ya Zanzibar uliotokana na hatua ya
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha kuufuta
Uchaguzi wote uliofanyika tarehe 25 Octoba, 2015 na matokeo yake katika
tangazo lake la tarehe 28-10-2015.
Kitendo hicho cha kuufuta Uchaguzi huo, kimepelekea nchi yetu kuingia
katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa. Wananchi wa kawaida ambao
ndio wapiga kura wanaathirika kisaikolojia kwa kushindwa kujua khatima
ya kura walizozipiga.
Kwa upande mwengine kumekuwa na ongezeko la ugumu
wa maisha visiwani Zanzibar unaotokana na mfumuko wa bei kwa bidhaa
muhimu na mzunguuko wa pesa kuwa mdogo kutokana na baadhi ya Wafanya
biashara kuwa na khofu ya kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa khofu
ya kutokea vurugu.
Ndugu waandishi wa habari, sisi tukiwa viongozi wa jamii
tumeshughulishwa sana na mtafaruku huu wa kisiasa unaotukabili ambapo
hadi sasa tumechukua hatua zifuatazo kusaidia kufikia ufumbuzi:-
Tuliwaandikia barua za nasaha viongozi wote wakuu wa kisiasa
wanaoshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo huu wa
kisiasa.
- Tuliwaandikia barua Mabalozi wa nchi sita waliopo Tanzania kuomba wasaidie katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro huu katika kuhakikisha kuwa demokrasia inachukua mkondo wake. Mabalozi wahusika ni kutoka nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Norway na Sweeden.
- Tulimwandikia barua Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kumkumbusha dhima yake ya kuingilia kati mgogoro huu ili kupatikana ufumbuzi wa haraka.
- Kupitia khutuba za Ijumaa katika misikiti mbali tumekuwa tukiwanasihi wananchi wawe na subra ili watoe fursa kwa viongozi wa kisiasa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu kwa njia za amani.
Ndugu waandishi wa habari,
Wananchi wa Zanzibar tulipata matumaini
tulipoona kuwa viongozi wakuu wa kisiasa wanakutana kuzungumzia hali ya
kisiasa nchini, tuliamini kuwa katika vikao hivyo Viongozi hawa wenye
kuheshimika wakitawaliwa na busara, hekima, uadilifu na wakiweka mbele
maslahi ya taifa badala ya vyama vyao basi muda si mrefu tungepata
ufumbuzi wa mgogoro huu.
Bahati mbaya tunaambiwa ni vikao 8 sasa
vimeshafanyika tokea kikao cha mwanzo cha tarehe 9 Novemba, 2015
hakuonekani kuwa matumanini yale wananchi waliyoyajenga kwao kuwa
yatatimia.
Tunasema hivi kwa sababu kwanza vinaendeshwa kwa usiri mkubwa
mno na hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwa umma.
Hali hii
inawafanya wananchi kutoelewa kinachoendelea na hivyo kuishi maisha ya
wasi wasi na kukosa utulivu hata wa kufanya shughuli zao za kimaisha.
Kasoro nyengine ni kuwa vikao hivi vimechukua muda mrefu sana na hivyo
kuibua maswali mengi na shaka kwa wananchi.
Pia tabia iliyojitokeza ya
baadhi ya wajumbe wanaoshiriki mazungumzo hayo kutoa kauli
zinazoshabikia msimamo wa upande mmoja kunawatoa imani wananchi juu ya
kuwepo kwa nia njema katika mazungumzo hayo na kwamba mazungumzo hayo
yanaweza kuivusha nchi yetu katika mkwamo huu wa kisiasa unaohatarisha
usalama wa nchi yetu.
Kutokana hali hii sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar tunatamka kwamba:-
- JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar zinawataka Viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki katika mazungumzo kuwajibika kwa kuweka mbele maslahi mapana ya nchi, kuhitimisha mazungumzo yao haraka iwezekanavyo na kutoa maamuzi rasmi ikiwa ni muongozo wa kutukwamua hapa tulipo kwa njia ya amani na salama. Tunawatanabahisha kuwa jamii yetu kwa sasa ni mfano wa bomu linaloweza kuripuka wakati wowote ule.
- Ukimya na uvumilivu wa Wazanzibari uliopo kamwe usichukuliwe kuwa wao ni Malaika bali ni binaadamu kama walivyo wengine ambao wanaweza kufikia hatua ya kushindwa na uvumilivu na kutoa maamuzi magumu yanayoweza kutufikisha pahala pabaya na kuigharimu sana nchi yetu. Hatuombi jambo hili kutokea lakini likitokea viongozi wakuu wa kisiasa watabeba dhima mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo basi, tunawaomba Viongozi wakuu wa kisiasa wanaoshiriki katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi, ni wakati muwafaka sasa watoke hadharani na watoe taarifa kwa umma juu ya hatua iliyofikiwa na ikiwezekana lini mazungumzo hayo yatakamilika na Wazanzibari watarajie nini kutokana na mazungumzo hayo.
- Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar, tunapinga kwa nguvu zetu zote kauli za uchochezi zinazoendelea kutolewa na wanasisa ambazo zinazidi kujenga khofu, hamasa na chuki miongoni mwa wananchi. Aidha, tunasikitika kuona kuwa kauli hizo zinatolewa bila ya kujali mazungumzo yanayoendelea ya viongozi wakuu ya kutafuta ufumbuzi.
- Sisi Viongozi wa Dini ya Kiislam Zanzibar, kwa heshima kubwa tunamuomba sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. John Pombe Magufuli ambaye ameonesha dalili njema za uadilifu na uwajibikaji mkubwa achukue hatua za wazi na za haraka katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu kabla nchi yetu haijatumbukia pahala pabaya. Aidha, tunamuomba kusimamia kwa udhati na ujasiri kuona haki inachukua mkondo wake na maamuzi ya Wazanzibari walio wengi yanaheshimiwa.
- Katika Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 JUMAZA ilikuwa na waangalizi katika majimbo yote ya Unguja na Pemba, kasoro zilizoripotiwa katika Uchaguzi huu ni kasoro ndogo ndogo mno na kwa hakika ni afadhali kuliko chaguzi zote zilizopita huko nyuma tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vyangi. JUMAZA inashangazwa sana na hatua ya kufuta Uchaguzi huu iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salim Jecha. JUMAZA inauliza kwanini wakati tulipokuwa na kasoro kubwa zaidi katika chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 Uchaguzi haukufutwa na kutakiwa kurejewa tena iwe Uchaguzi wa mwaka 2015 tu? Na jee kama uchaguzi utakaorejewa nao ukawa na kasoro zitakazolalamikiwa, utafutwa tena? Tutafanya chaguzi ngapi kwa mtindo huu?
- Taasisi za Kiislam Zanzibar zinawaomba Waislamu wote kuendeleza dua ili kuitakia mema nchi yetu na kumkabidhi Mwenyezi Mungu kwa wale wote wanaokusudia shari. Aidha, zinawaomba Maimamu na Makhatibu kukemea kauli zinazohatarisha amani na mshikamano wa jamii.
- JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar zina khofu kubwa juu ya kurejewa kwa Uchaguzi, uzoefu unaonesha kuwa nchi zilizorejea uchaguzi katika Bara la Afrika kama vile Nigeria, Zimbwabwe, Malawi na kwengineko hatimaye zilitumbikia katika machafuko makubwa. Kama hilo halitoshi Zanzibar tuna historia mbaya ya kurejea Uchaguzi. Wengi tunakumbuka katika historia ya Zanzibar kile kinachoitwa ‘vita au machafuko ya Juni ‘. Uchaguzi wa Januari mwaka 1961 ulilazimika kurejewa mwezi wa Juni 1961, ambapo ulipelekea machafuko makubwa ikiwemo vifo vya watu 68, maelfu kujeruhiwa, nyumba kuvunjwa na kuchomwa moto. Kwa historia hii JUMAZA na Taasisi za Kiislam Zanzibar hazioni kuwa ni busara kurejewa kwa Uchaguzi uliofanyika kwa ufanisi na kukamilika. Penye nia njema na utashi wa kisiasa basi njia ya uadilifu iliyo wazi ya kutukwamua hapa tulipo ni kwa Viongozi wakuu wa kisiasa kufikia ufumbuzi na makubaliano haraka iwezekanavyo.
Mola wetu Mtukufu tunakuomba kwa rehma zako utuwezeshe kufikia ufumbuzi
unaofaa juu ya tatizo linalotukabili na uziunganishe nyoyo za
Wazanzibari kuwa pamoja, kupendana na kuweka mbele maslahi ya nchi yao.
Amiin.
AHSANTENI
………………………………..
MUHIDDIN Z. MUHIDDIN
KATIBU MTENDAJI
JUMUIYA YA MAIMAMU ZANZIBAR
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment