*Ni wa makampuni yaliyochota Sh bil 300 za CIS
*Zitto kabwe aibuka, aanika madudu ya Hazina
SHABANI MATUTU NA FLORIAN MASINDE
SIKU moja baada ya Serikali kuzitaka kampuni 980 zinazodaiwa fedha
zilizotolewa na wahisani chini ya Mpango Maalumu wa Kuagiza Bidhaa na
Malighafi kutoka Nje (CIS), baadhi ya vigogo wameanza kujisalimisha kwa
Serikali ya Rais John Magufuli.
Hatua hiyo imetokana na mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na
Mipango, kuwataka wafanyabiashara wakubwa waliochota mabilioni hayo
kuyarudisha kwa mujibu wa sheria.
Inaelezwa kupitia mpango huo, zaidi ya makampuni 900 yaliyokopeshwa
fedha hizo zinazofikia Sh bilioni 349, yalishindwa kuzirudisha fedha
hizo, huku wengine kuona kama zawadi kwao.
Kampuni hizo zilizokopeshwa fedha hizo chini ya mpango huo, zimekuwa
zikirudisha kwa kusuasua na nyingine zikionyesha nia ya kutorejesha
mikopo hiyo, huku Serikali ikilazimika kutoa miezi sita kwa kampuni zote
kutakiwa kulipa madeni hayo.
HISTORIA YA FEDHA ZA CIS
Fedha hizo za kigeni zilitoka kwa wahisani kuanzia
mwaka 1980 -1992/93 kwa lengo la kuipa serikali uwezo wa kuimarisha
uchumi wake.
Fedha hizo zililengwa kwa taasisi, kampuni, viwanda na biashara
mbalimbali ili kuzipa uwezo wa kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje,
kwa kuwa wakati ule nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.
Fedha za CIS zilitolewa kama mikopo yenye masharti nafuu, ambapo
wakopaji walitakiwa kulipa deni bila kutozwa riba, lakini mkopaji
akichelewa kulipa katika kipindi cha miezi 18, mkopo huo huwa na riba ya
asilimia 17.
Fedha zilizokusanywa kutokana na malipo ya deni zilikuwa zinachangia
mapato ya Serikali (bajeti) pamoja na miradi maalumu ya maendeleo, baada
ya makubaliano na wahisani husika.
ZITTO AIBUA MADUDU
MTANZANIA ilimtafuta aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye alionesha
wasiwasi wa kufanikiwa kwa kazi hiyo chini ya Kampuni ya Msolopa
Investment Ltd, iliyopewa kazi ya kukusanya madeni hayo .
Alisema mwaka 2013, PAC ilipowaita viongozi wa Hazina kuelezea kuhusu
makusanyo hayo ya madeni walieleza kuwa makampuni mengi yamekufa hali
iliyowafanya wapate ugumu katika kukusanya fedha zote.
“Kati ya madeni yaliyokuwa yakidaiwa ni Sh bilioni 379 na
zilizokusanywa ni Sh bilioni 142 pekee na Kampuni ya Msolopa na kiasi
kilichobaki jibu lao Hazina walisema makampuni yaliyokuwa yanadaiwa
yalikuwa feki,” alisema Zitto.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), alisema
kampuni nyingi ambazo hazijalipa fedha hizo za CIS zimeshafungwa.
“Baada ya kubainika kwa hayo ilibidi Kamati ya PAC, kuagiza Hazina
waunde kikosi kazi kufuatilia suala hilo, lakini tangu mwaka huo 2013
sikusikia chochote hadi juzi niliposikia Serikali imetangaza kumpatia
kazi ya ukusanyaji madeni Kampuni ya Msolopa ambayo mwaka 2013
tulielezwa kuwa ilishindwa kazi hiyo,” alisema Zitto.
Ametaka jambo hilo kufanyiwa kazi hadi mwisho kwa sababu imekuwa ni
kawaida kuibuka na kuzama kila wakati ambapo kwa upande wa PAC ilifanya
kazi kwa kiwango chake, hivyo kwa sasa Serikali inatakiwa kufanyia kazi
kwa uwazi na kuzingatia haki.
“Orodha ya wadaiwa iko wazi na Kamati ya PAC ilipewa na Kampuni ya
Msolopa ilipewa orodha hiyo na inapaswa kuwekwa wazi na wapo
wafanyabiashara na mashirika ya umma yaliyobinafsishwa,” alisema Zitto.
KAULI YA WIZARA YA FEDHA
Kutokana na tangazo la Wizara ya Fedha na Mipango,
ambalo lililosaini na Katibu Mkuu, Dk. Servacius Likwelile, MTANZANIA
ilifika wizarani hapo na kuzungumza na Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi
Mduma, ambaye aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi cha
miezi sita kilichotolewa na Serikali kwa wadaiwa hao.
Alisema kutokana na agizo hilo la kutakiwa kulipa ni vema wadaiwa wa
makampuni hayo kutumia muda huo kurejesha fedha hizo kabla
hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo majina yao kutangazwa
hadharani.
Alisema ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa, Serikali imeingia
mkataba na Kampuni ya Msolopa Investment ya jijini Dar es Salaam
kuwafuatilia wadaiwa wote na kuhakikisha wanalipa ndani ya kipindi
hicho.
Mduma alisema katika juhudi hizo mpya wadaiwa waliokuwa
wanafuatiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanapaswa kuwasiliana
na mamlaka hiyo waweze kupata kumbukumbu za madeni yao, vivyo hivyo kwa
wadaiwa waliopata mikopo yao kupitia Benki ya Rasilimali (TIB),
wanatakiwa kuwasiliana na benki hiyo kuwasilisha madeni yao haraka.
Pamoja na hali hiyo mmoja wa maofisa wa juu wizarani hapo aliiambia
MTANZANIA kwamba tangu lilipotolewa tangazo hilo na Wizara ya Fedha
baadhi ya viongozi wa makampuni kadhaa yanayodaiwa walikweda
kujisalimisha kwa Rais Magufuli na wengine kuahidi kuzilipa ndani ya
kipindi kilichopangwa.
Chanzo Mtanzania
Wednesday, 6 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment