Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari.
WATU wawili, baba na mwanawe wamekufa baada ya kushambuliwa na
kujeruhiwa na simba mkoani Katavi. Tukio hilo lilijiri Januari 3, mwaka
huu, pale mkazi wa kijiji cha Sitalike wilayani Nsimbo Wilaya ya Mlele,
John Jeremiah (45) na mwanawe mwenye umri wa miaka mitano, walipouawa na
simba baada ya kuwavamia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher
Anjelo alisema kuwa kutokana na mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi
kutokuwa imara, simba huyo aliuparamia, akausukuma na kuingia ndani.
Inadaiwa kuwa simba huyo baada ya kumjeruhi vibaya na kumsababishia
kifo Jeremiah alimvamia mtoto wake na kula kiwiliwili chake ambapo
alibakiza kichwa kisha akaondoka na kutokomea porini. Kijiji cha
Sitalike kinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo wilayani
Mlele.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Anjelo alitoa taarifa kwa askari wa
wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo walianza kumsaka simba
huyo wakishirikiana na wananchi. Walifanikiwa kumuua simba huyo.
Inaelezwa kuwa baada ya kumuua simba huyo, baadhi ya wakazi wa kijiji
hicho walitaka wapewe mzoga wa mnyama huyo kwa ajili ya kitoweo huku
wengine wakidai viungo vyake ni tiba za kijadi na mazindiko, lakini
askari hao wa wanyama pori walikataa na kuondoka na mzoga wa mnyama huyo
kwa madai kuwa wanenda kuuteketeza kwa moto.
Wakati huo huo, watu wawili wameuawa kikatili kwa kuchinjwa shingo na
kukatwakatwa mapanga katika tukio lililotokea katika vijiji vya Bindi
na Mwamkulu mkoani Katavi. Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Katavi,
Focus Malengo alisema kwamba Januari 02 mwaka huu, saa saba usiku mtu
aliyefahamika kwa jina la Chalya Kishosha (60), mkazi wa Kijiji cha
Ibindi alikutwa akiwa ameuawa kikatili kwa kuchinjwa na watu
wasiojulikana.
Alisema watu hao walimvamia akiwa amelala chumbani kwake. Tukio
jingine lilitokea siku hiyo hiyo katika Kitongoji cha Center John katika
Kijiji cha Mwamkulu Wilaya ya Mpanda ambapo mtu mmoja aliyefahamika kwa
jina la Tiho Robart (40) alikutwa akiwa ameuawa kikatili kwa kuchinjwa
shingo.
Kaimu Kamanda Malengo alisema marehemu pia alivamiwa na wauaji hao
wakati akiwa amelala ndani ya nyumba yake. Alisema kuwa chanzo cha
mauaji katika matukio hayo mawili hakijajulikana na kwamba jeshi la
polisi kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vya Mwamkulu na Ibindi
wanaendelea kufanya msako ili kubaini waliohusika na mauaji ya watu hao
na kuwafukuisha kwenye mkondo wa sheria.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Wednesday, 6 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment