NAIBU
Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amevitoza faini ya
zaidi ya Sh milioni 60 viwanda viwili vya Lodhia Plastic Industries
Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka taratibu za kazi na kudharau
mamlaka ya usalama mahali pa kazi (Osha).
Mavunde
alitoa adhabu hiyo jana jijini hapa wakati alipofanya ziara ya
kushtukiza kwenye viwanda hivyo huku akiongozana na wakuu wa idara ya
kazi, idara ya uhamiaji na viongozi kutoka Osha.
Awali
alipokuwa katika kiwanda cha Sunflag, alizungumza na baadhi ya
wafanyakazi na kugundua kuwa baadhi yao hawana mikataba ya ajira na
wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja lakini pia hawana vifaa vya kutosha
vya kuzuia pamba kuingia mwilini.
Pia
aliagiza menejimenti ya kiwanda hicho, kuhakikisha inalipa mishahara ya
wafanyakazi kwa kima cha Serikali na si kuwalipa Sh 4,424 kwa siku.
Aidha akiwa kiwandani hapo aligundua kuwa kuna wafanyakazi raia wa
kigeni 41 wanaofanya kazi katika idara mbalimbali zinazopaswa kusimamiwa
na raia wa Tanzania.
Akiwa
katika kiwanda cha Lodhia, Mavunde alifuta kibali cha mmoja wa wageni
kutoka nje ya nchi kutokana na kukiuka kibali cha kufanyakazi na
kumwagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Raju Sighn kupeleka vibali 38 vya
raia wa kigeni ili vikaguliwe.
Kutokana
na kasoro hizo Mavunde alitoza faini ya jumla ya Sh milioni 22.9 kwa
kiwanda cha Sunflag na kiwanda cha Lodhia Plastic kilitozwa Sh milioni
10 kutokana na kukiuka masharti ya uendeshaji viwanda na kutoa siku 14
faini hiyo iwe imelipwa.
“Ndani
ya siku saba muwe mmepeleka taarifa Osha na hivi vibali vya wageni
kutoka nje ya nchi kwa ofisi za kazi jijini Arusha. Maana mnasema mna
vibali lakini nilivyoviona havijaniridhisha, pelekeni ili waone na
ikithibitika mmekidhi viwango mtapunguziwa adhabu, ila heshimuni sheria
za nchi,” alisisitiza.
Credit; Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment