*Amwita mtukanaji na mkwamishaji miradi ya maendeleo
*Diana Chilolo amgeuka Lowassa, asema hana washauri
Na Bakari Kimwanga, Ikungi
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Magufuli, jana aliwasili Jimbo la Singida Mashariki ambalo mwakilishi
wake bungeni aliyemaliza muda ni Tundu Lissu (Chadema) na kuwataka
wapiga kura wa jimbo hilo kutomchagua tena kwa sababu ana lugha chafu.
Dk. Magufuli, ambaye alifanya mkutano wake wa kwanza Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida uliohudhuriwa na umati mkubwa, alisema amekwenda kufanya
mkutano wa kampeni katika jimbo hilo kwa sababu anataka wapigakura
wamchague mgombea ubunge wa CCM aliyemtaja kwa jina la Jonathan Njau,
ambaye ni mkweli na ana uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli.
Alisema Lissu hapaswi kuchaguliwa tena kwa sababu ameshindwa
kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo kupata maendeleo ya kweli kwa
kushindwa kusimamia miradi mingi ya jimbo hilo kutokana na misimamo yake
iliyochangia kuwaumiza wapigakura wake.
“Ninasema wana Ikungi na Watanzania kwa ujumla tunahitaji kujenga
nchi kwa kutumia rasilimali zetu ambazo zitamnufaisha kila Mtanzania,
ila kwa hapa kwenu mmeteseka kwa sababu ya aina ya mbunge mliyemchagua.
Ni bora kukosea jambo lingine au hata kuoa lakini sio kuchagua, kwani
haya ndiyo yanawafanya mteseke. Mnachagua mbunge ambaye kazi yake ni
kuwatukana mawaziri na hata zinapojadiliwa bajeti wanatoka nje.
“Waziri naye ni binadamu, hana moyo wa chuma wa kuvumilia matusi, je,
kwa hali hii anaweza kuleta maendeleo kwenu. Hapana msifanye makosa kwa
kuchagua wabunge wa matusi na kutoka nje,” alisema Dk. Magufuli
Dk. Magufuli alijigamba mbele ya wapiga kura hao kuwa yeye ni
‘tingatinga’ la maendeleo na amedhamiria kujenga Tanzania mpya yenye
uchumi wa viwanda pamoja na kukuza ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, alisema
anazijua na ana mbinu za kupambana nazo, huku akitolea mfano changamoto
zinazowakabili wauguzi na madaktari, ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba.
“Kule Chato kuna daktari alilazimika kufanya upasuaji kwa kutumia
chemli na alifanikiwa kuokoa maisha ya watu wengi kweli, sasa ni wajibu
wa Serikali ya Awamu ya Tano kuyaangalia haya na kuyapatia ufumbuzi wa
uhakika,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha, Dk. Magufuli alisema anaijua mipango inayofanywa na baadhi ya
watu wanaotaka kujigawia maeneo muhimu ya uchumi na aliwaonya kuwa
wanapaswa kujiandaa kuondoka wenyewe.
Aliitaja baadhi ya miradi inayolengwa na wale aliowaita mafisadi kuwa ni reli, gesi na umeme.
Diana Chilolo
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa
Singida, Diana Chilolo, ambaye alipewa fursa ya kuzungumza kwenye
mkutano huo, alieleza kushangazwa na uamuzi wa mgombea urais wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na vyama vya
NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy
(NLD) vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa,
aliyeukamia urais kama maji.
Chilolo ni mmoja wa makada wa CCM ambao awali walikuwa katika kambi
ya Lowassa, lakini katika mkutano wa jana alieleza kumshangaa kwa
kuonyesha udhaifu pale alipokihama CCM na kujiunga na Chadema.
“Lowassa amekosa mshauri na kama angekuwa naye asingechukua fomu ya
urais, maana ukimwangalia unamuona hayuko sawa, lakini pia amekuwa
akitajwa katika kila udhaifu wa ufisadi na Lissu alikuwa ni moja wa watu
waliokuwa wakimsema, sijui leo amemsafisha na nini.
“Muogope kiongozi asiyekubali matokeo, mimi nilikuwa mgombea kura
zangu hazikutosha, bado nipo imara na ninatafuta kura za CCM kwa rais,
wabunge na madiwani na sijayumba,” alisema Chilolo.
Chanzo Gazeti la Mtanzania.
Sunday, 4 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment