Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Seif Sharif Hamad akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana
kuhusu hatma ya uchaguzi wa Zanzibar. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa
Kamati ya muda ya Uongozi wa chama hicho.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, amesema ana
imani na jitihada za Rais John Magufuli katika kutafuta suluhu ya
mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Amemtaka Magufuli aingilie kati kutafuta mbinu muafaka, inayoendana na matakwa ya kisheria na kikatiba, kumaliza mgogoro huo.
Aidha Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waanchi (CUF) na
mgombea Urais Zanzibar, alisema chama hicho hakiko tayari kurudia
uchaguzi, kwa kuwa wanaamini kuwa uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka
jana, ulikuwa huru na haki na tamko la kuufuta lilikuwa batili.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema tangu
kufutwa kwa uchaguzi huo na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC) Jecha Salim Jecha, kumefanyika vikao takribani vinane
vinavyoshirikisha viongozi mbalimbali, wakiwemo marais wastaafu wa
Zanzibar, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein na Rais Magufuli.
“Kwa kuwa suala hili ni kubwa na limeathiri taswira ya nchi mbele ya
jamii ya kimataifa na kwa kuwa Rais Magufuli alipozungumza na waandishi
wa habari baada ya kukutana na mimi (Maalim Seif) Ikulu Dar es Salaam
alisisitiza haja ya kulipatia ufumbuzi wa haraka suala hili…” …”Tunaona
wakati umefika yeye mwenyewe aongeze juhudi zenye lengo la kufanikisha
hatua tulizopendekeza ambazo ni kuendelea kuhesabiwa kwa kura katika
majimbo tisa yaliyobaki na kutangazwa rasmi kwa mshindi kupitia uchaguzi
wa mwaka jana na si kurudia uchaguzi mpya,” alisema Seif.
Kuhusu Rais Magufuli
Alisema Rais Magufuli amefanya kazi kubwa ya kutia moyo ya
kuhakikisha mazungumzo kuhusu muafaka wa uchaguzi Zanzibar, yanakamilika
kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria.
“ Rais John Magufuli amefanya kazi kubwa ya kututia moyo ili
tukamilishe mazungumzo hayo kwa ufanisi na kwa kuzingatia matakwa ya
Katiba na Sheria. Alikutana na mimi na baadaye alikutana na Dk Ali
Mohamed Shein,” alisema Maalim Seif.
Alisema “Ukweli ni kwamba katika vikao hivyo vinane bado Dk Shein na
Balozi Ali Idd ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais wameendelea
kung’ang’ania kurudiwa kwa uchaguzi huku wakimtetea kwa nguvu Jecha,
mimi nasisitiza haja ya kuheshimu matakwa ya Kikatiba na Kisheria na
maamuzi ya wananchi wa Zanzibar” .
Alisema anaamini kuwa Rais Magufuli kupitia mazungumzo waliyowahi
kuyafanya, alionesha wazi kuwa anataka mzozo unaoendelea umalizike kwa
kuhakikisha kila upande unaridhika.
“Nadhani Dk Magufuli akiwa Amiri Jeshi Mkuu hayuko tayari kuunga
mkono misimamo ambayo hapo baadaye itabidi atumie majeshi yake kutuliza
ghasia. Nasisitiza I have confidence in him (nina imani naye) kwamba
anataka suala hili limazikike kwa pande zote kuridhika,” alisisitiza.
Alisema chama chake kinaamini kuwa uchaguzi visiwani humo kurudiwa si
suluhisho la mgogoro uliopo bali badala ya kutuliza mgogoro uliopo,
utaanzisha vurugu na fujo hasa pale wananchi watakapohisi hawatendewi
haki juu ya maamuzi yao.
Alisema uchaguzi huo haufai kurudiwa kwa sababu hakuna uhalali wa
msingi unaosababisha urejewe kutokana na kile alichodai ni kitendo cha
Mwenyekiti wa ZEC Jecha, kutokuwa na uhalali wa kufuta uchaguzi Kikatiba
na Kisheria.
Alisema Mwenyekiti huyo alifuta uchaguzi huo bila kushirikisha
wajumbe wake ambapo kwa mujibu wa Sheria ni kosa. Aidha alisema pia
chama hicho hakikubali uchaguzi huo kurudiwa kwa kuwa kiini cha mzozo
uliopo kwa sasa ni uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi.
“Uchaguzi ni wapigakura na si vyama au wagombea. Lazima wapigakura
waridhishwe kuwa uchaguzi ulikuwa na tatizo kiasi cha kuufanya
ufutwe…hadi sasa hakuna mwelekeo unaoonyesha kuna ukweli katika tuhuma
za kasoro za uchaguzi,” alisema.
Alipendekeza kuwa ili mzozo unaoendelea visiwani hapo umalizike ni
vyema Mwenyekiti wa ZEC Jecha akaondoka kwenye wadhifa huo au ajiuzulu
kutokana na kitendo cha kufuta uchaguzi bila kufuata taratibu.
Aidha alipendekeza ZEC chini ya Makamu Mwenyekiti na Makamishna
waliobaki kwa mujibu wa Sheria na Katiba, wamalizie kutangaza matokeo ya
Urais kwa majimbo tisa yaliyohakikiwa na kumaliza uhakiki wa matokeo ya
Urais kwa majimbo 14 yaliyobaki na kutangaza matokeo.
Aidha alimtaka Rais Magufuli aongeze juhudi zenye lengo la
kufanikisha mapendekezo hayo wakati uongozi wa CUF na CCM nao ufanye
mazungumzo ya kukamilisha utaratibu wa kuunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar nchini ya mshindi atakayetangazwa.
Akana kujitangaza Kuhusu madai kuwa alikiuka Sheria kwa kujitangaza
mshindi kabla ya Tume ya Uchaguzi, Maalimu Seif alisema, haoni kama
amefanya kosa kwani alichofanya ni kuchukua matokeo yaliyokwishatangazwa
na wasimamizi wa uchaguzi na kubandikwa kwenye vituo vya uchaguzi.
“Hakuna sehemu yoyote niliyojitangazia mimi Maalim Seif nimeshinda,
ila nimechukua matokeo yaliyokwishatangazwa yanayoonyesha kuwa
ninaongoza,” alisisitiza.
Oktoba mwaka jana, Tume ya Uchaguzi ZEC ilitangaza kufuta matokeo
yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani Zanzibar baada ya kubainika kujitokeza
kwa kasoro nyingi, zilizosababisha kukiukwa kwa sheria za uchaguzi na
haki kushindwa kutendeka.
Baadhi ya kasoro zilitajwa ni pamoja na baadhi ya vituo vya uchaguzi
vya Pemba kuwa na idadi kubwa ya kura zilizopigwa kuliko idadi ya watu
waliopo katika daftari la wapiga kura.
Mara baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo, vikao mbalimbali vilifanyika
vilivyoshirikisha wagombea wapinzani katika uchaguzi huo ambao ni Seif
na Dk Shein ili kuwezesha kupata suluhu.
Serikali ilibainisha kuwa inajipanga kutaja tarehe ya kurejewa kwa uchaguzi upya visiwani humo.
Chanzo Gazeti la HabariLeo.
Monday, 11 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment