TUNU NASSOR NA FROLIAN MASINDE, DAR ES SALAAM
WAKATI Watanzania wakiingia katika juma jipya kwa ajili ya majukumu
ya ujenzi wa taifa, mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli, wameendelea
kutumbua majipu bila ganzi kwa watendaji wa Serikali.
Jana kwa nyakati tofauti Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Angella Kairuki, ametangaza kutumbua watendaji watatu,
huku mwenzake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,
akitumbua watendaji wawili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN).
Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri Kairuki alitangaza
kumsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Chuo cha Utumishi wa
Umma, Said Nassoro kutokana na utendaji usioridhisha.
Pia amewasimamisha kazi Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la
Tabora, Silvanus Ngata na Dk. Joseph Mbwiro wa tawi la Dar es Salaam
kutokana na ubadhirifu wa fedha.
Waziri Kairuki aliwaambia waandishi wa habari kuwa Nassoro ameshindwa
kuwasimamia watumishi na kusababisha matumizi mabaya ya fedha.
Alisema kutokana na makosa ya kiutendaji, Nassoro aliotoa mwanya kwa
viongozi wa matawi kufanya ubadhirifu wa mali za umma kwa masilahi
binafsi.
“Kwa mfano aliyekuwa mkuu wa tawi la Mtwara, Silvanus Ngata alizidisha fedha za gharama za ujenzi tofauti na zilizoainishwa.
“Pamoja na tuhuma hizo, Nassoro hakuchukua hatua yoyote zaidi ya
kumbadilisha kituo cha kazi na kumpeleka mkoani Tabora,” alisema
Kairuki.
Kuhusu Dk. Mbwiro, alisema kuwa alitumia vibaya fedha za ada na
kusababisha hasara ya shilingi bilioni moja alipokuwa anakaimu kitengo
cha fedha.
“Pamoja na tuhuma hizi, bado aliteuliwa kuwa mkuu wa chuo wa tawi la
Dar es Salaam nafasi ambayo alikuwa akiitumikia hadi sasa,” alisema
Waziri Kairuki.
Alisema ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG)
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilionyesha
kuwapo ubadhirifu huo.
NAPE NA JIPU TSN
Nayo Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN),
imemsimamisha kazi Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo, Gabrieli
Nderumaki, kupisha uchunguzi kutokana na utendaji usioridhisha ndani ya
kampuni hiyo.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Profesa Moses Warioba,
alisema hatua ya kumsimamisha kazi Nderumaki imetokana na kuwapo kwa
malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na nafasi yake
itachukuliwa na Naibu Mhariri, Tumma Abdallah.
“Kumekuwa na mambo mengi yanayofanyika bila kufuata utaratibu ndani
ya kampuni hii ikiwamo wafanyakazi kutoelewana na menejimenti katika
kulipwa stahili zao, pamoja na wafanyakazi kupewa majukumu ambayo
hawana uwezo wa kuyatekeleza,” alisema Prof. Warioba.
Alisema pamoja na hayo, pia bodi imetengua uteuzi wa Felix Mushi,
ambaye alikuwa Meneja Mauzo na Masoko katika kiwanda cha uzalishaji kwa
kukosa sifa na utendaji mbovu uliosababisha kampuni kushuka katika
uzalishaji.
Hatua hiyo ya kuwawajibisha watendaji hao imetokana na ziara
iliyofanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye katika kampuni hiyo, ambapo pia hakuridhiswa na utendaji mbovu
uliosababisha wafanyakazi 21 kuacha kazi.
“Nataka bodi itafakari juu ya malalamiko yaliyopo kwa wafanyakazi na
wachukue hatua kabla mimi sijakutana na wafanyakazi hao wiki ijayo ili
kujua mapungufu yako wapi,” alisema Nape.
Hata hivyo, bodi hiyo ya wakurugenzi inaendelea kutafuta namna ya
kuboresha utendaji ndani ya kampuni hiyo ili iendane na kasi iliyopo
katika uzalishaji wa magazeti kwa kiwango kikubwa.
MAJIPU YALIYOTUMBULIWA
Katika siku zaidi ya 100 za uongozi wa Rais Magufuli, watendaji zaidi
ya 150 wamefukuzwa kazi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.
Katika mpango wake huo Rais Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa
Mamkala ya Bandari (TPA) pamoja na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya
mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa makontena.
Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk.
Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati
na Maji (Ewura), Haruna Masebu.
Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia
vyema TPA, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa katika Bandari
ya Dar es Salaam bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya
mabilioni ya shilingi.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya
Rais Magufuli ambaye pia alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh bilioni 16
ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).
JIPU LA RAHCO
Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi
ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.
Uamuzi huo umelenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji
mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa
zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
JIPU LA TAKUKURU
Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16,
mwaka jana.
Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na
namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana
na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika Bandari
ya Dar es Salaam.
JIPU LA NIDA
Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza pia kumsimamisha kazi
ili kupisha uchunguzi dhidi yake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.
Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,
Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria,
Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Balozi Sefue alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonyesha kuwa NIDA
hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh. bilioni 179.6 kiasi ambacho ni
kikubwa.
WALIOKIUKA AMRI YA KUSAFIRI NJE
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza kusimamishwa kazi mara
moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya
nchi licha ya Serikali kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa
umma.
Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia
Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari
kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 22 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment