Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Kidato cha
Nne 2015, yakionesha ufaulu wa watahiniwa wote umeshuka kwa asilimia
0.80, ikilinganishwa na mwaka 2014 huku zaidi ya asilimia 80 ya
watahiniwa waliofanya mtihani huo wakifeli somo la Hisabati.
Hata hivyo, asilimia 24 .7 ya watahiniwa wa shule 94.941 waliofaulu
wamepata Daraja la I hadi III, hivyo kuwa na nafasi ya kuendelea na
Kidato cha Tano na watahiniwa 113,489 sawa na asilimia 32 wamefeli
mtihani huo.
Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana Dar es Salaam, wasichana
wameshika nafasi ya kwanza na ya pili katika wanafunzi 10 bora kitaifa,
ambao ni Butogwa Shija wa Canossa ya Dar es Salaam aliyefuatiwa na
Congcong Wang wa Feza Girls pia ya Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde
alisema watahiniwa 272,947 kati ya watahiniwa 433,633 wa kujitegemea na
shule, wamefaulu mtihani huo ambao ni wasichana 131,913 na wavulana
141,034.
Akielezea kwa upande wa watahiniwa wa shule, Dk Msonde alisema
watahiniwa 240,996 (asilimia 67.91) ya watahiniwa 384,300 waliofanya
mtihani, wamefaulu mtihani huo. Mwaka 2014, watahiniwa wa shule
waliofaulu walikuwa ni 167,643 (asilimia 69.76). Hivyo kwa mwaka huu
ufaulu umeshuka kwa asilimia 1.85.
Alisema kwa watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni
31,951 sawa na asilimia 64.80. Mwaka 2014 watahiniwa waliofaulu walikuwa
ni 29,162 sawa na asilimia 61.12. Hata hiyo, watahiniwa wa shule 94,941
sawa na asilimia 24.73 wamepata Daraja la I hadi III huku zaidi ya nusu
ya waliofaulu kwa watahiniwa wa shule 146,055 wakipata Daraja la Nne.
Mwaka 2014 asilimia 30.72 (watahiniwa 73,832) walipata madaraja ya
Distinction, Merit na Credit kwa kutumia mfumo wa Wastani wa Alama
(GPA). Dk Msonde alisema watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa, waliofaulu ni
watahiniwa 7,536 kati ya 16,162.
Kwa mwaka 2014, watahiniwa 6,810 walifaulu. Akizungumzia ufaulu wa
masomo kwa watahiniwa wa shule, alisema masomo ya Civics, Historia,
Jiografia, Kiingereza, Kemia, Baiolojia, Commerce na Book-Keeping,
ufaulu wake umepanda kati ya asilimia 1.09 na 12.86 ikilinganishwa na
mwaka 2014.
“Ufaulu wa juu kabisa ni wa somo la Kiswahili unaoonesha asilimia
77.63 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu. Ufaulu
wa chini ni somo la Hisabati ambao ni asilimia 16.76. Mwaka 2014 ufaulu
ulikuwa ni asilimia 19.58.” alifafanua bosi huyo wa Necta.
Msonde aliongeza: “Ufaulu wa masomo mengi upo chini ya asilimia 50,
hata idadi ya watahiniwa waliopata Daraja la I, II na III ni takribani
robo ya watahiniwa waliofanya mtihani hivyo juhudi zinahitajika katika
kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo na kuimarika zaidi kwa ubora wa
elimu.”
Akizungumzia upangaji wa shule kwa ubora wa ufaulu, Dk Msonde
alizitaja shule 10 bora kuwa ni Kaizirege (Kagera), Alliance Girls
(Mwanza), St Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar
es Salaam), Marian Boys (Pwani), Alliance Rock Army (Mwanza), Feza
Girls na Feza Boys (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).
Alizitaja shule zilizofanya vibaya kuwa ni Pande (Lindi), Igawa
(Morogoro), Korona (Arusha), Sofi (Morogoro), Kurui (Pwani), Patema
(Tanga), Saviak (Dar es Salaam), Gubalk (Dodoma), Kichangani na Malinyi
(Morogoro).
Dk Msonde aliwataja watahiniwa waliofanya vizuri zaidi na shule
wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza
Girls), Innocent Lawrence (Feza Boys), Dominick Aidano (Msolwa,
Morogoro), Sang’udie Sang’udie (Ilboru), Asteria Chilambo na Belinda
Magere (Canossa), Humfrey Kimanya (Msolwa), Bright Mwang’onda na Erick
Mwang’ingo (Marian Boys).
Wasichana
Aliwataja wasichana 10 bora ni Butogwa (Canossa), Congcong (Feza
Girls), Asteria Chilambo na Belinda Magere (Canossa), Lilian Kiwone na
Marynas Duduye (St Francis Girls), Julieth Mbalilaki (Baobao), Vaileth
Lazaro (Kilakala), Nancy Shao (Canossa) na Emmy Shemdangiwa (St Marys
Mazinde Juu).
Wavulana
Aliwataja wavulana 10 bora ni Innocent Lawrence (Feza Boys), Dominick
Aidano (Morogoro), Sang’udie Sang’udie (Ilboru), Humfrey Kimanya
(Msolwa), Bright Mwang’onda na Erick Mwang’ingo (Marian Boys), Mohamed
Kigume (Marian Boys), David Joseph (Ilboru), Daniel Mabimbi (Alliance
Boys), William Kihanza (Mzumbe).
Aidha, Dk Msonde alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa
87 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani, kati ya hao 25 ni wa
kujitegemea na 52 ni wa shule na 10 ni watahiniwa na Mtihani wa
Maarifa.
Baraza pia limezuia kutoka matokeo ya watahiniwa 23 wa shule,
waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya baadhi ya masomo huku
watahiniwa 98 walioshindwa kufanya masomo yote, wote watapewa nafasi ya
kufanya mitihani hiyo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji huyo wa Necta alisema Baraza
katika Mkutano wa 109, wameamua kurejesha utunuku wa mfumo wa madaraja
wa Jumla ya Alama (Divisheni) kuanzia matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka
2015 kutokana na maoni ya wadau, ambao wameona mfumo wa Divisheni
unaeleweka ukilinganisha na ule wa Wastani wa Alama (GPA) uliokuwa
ukitumika awali.
Dk Msonde alisema kutokana na mabadiliko hayo, alama za ufaulu
zitakuwa kama ifuatavyo; A (alama 75-100), B (65-74), C (45-64), D
(30-44) na F (0-29) wakati wa Kidato cha Sita madaraja yatakuwa A
(80-100), B+ (70-79), B (60-69), C (50-59), D (40-49), S (35-39) na F
(0- 34).
Dk Msonde alisema madaraja ya ufaulu kwa Kidato cha Pili na Nne
yatakuwa ni Daraja la I (pointi 7-17), II (pointi 18-21), III (pointi
22- 25), IV (pointi 26-33) na Daraja 0 (pointi 34-35) huku wa Kidato cha
Sita itakuwa ni Daraja la I (pointi 3-9), II (pointi 10-12), III
(pointi 18-19) na Daraja 0 (pointi 20-21).
Chanzo HabariLeo.
Thursday, 18 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment