Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa onyo kwa wadaiwa sugu
ambao hawajajitokeza kuanza kulipa madeni yao, kwamba hatua mbalimbali
dhidi yao zinatafuata kokote waliko.
Miongoni mwa hatua hizo, bodi hiyo imetaja kuwa ni kuwatoza wadaiwa
hao sugu riba ya asilimia kumi katika deni lao na kutumia taarifa zao
kuwazuia kufanya safari za nje ya nchi.
Taarifa ya hivi karibuni ya bodi hiyo ambayo gazeti hili inayo,
imeeleza kuwa wadaiwa hao wa tangu mwaka wa masomo wa 1994/95, wataanza
kusakwa kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ambaye anawajibika kukagua mali zote za Serikali.
Mbali na CAG, ambaye ana mkono mrefu wa kuwasaka katika ofisi zote za
Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na katika miradi
ambayo Serikali ina ubia na sekta binafsi, pia kampuni binafsi za
ukaguzi wa hesabu, zenye mkono mrefu katika sekta binafsi, zitatumika
kuwasaka katika kampuni binafsi na asasi za kiraia.
“Jukumu la CAG na kampuni zingine binafsi za ukaguzi wa mahesabu, ni
kulazimisha waajiri kuwasilisha taarifa za wafanyakazi wao ambao ni
wahitimu wa elimu ya juu na makato ya mkopo waliopewa,” imeeleza taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo imefanya marejeo ya Sheria ya Bodi namba 9 ya 2004 na
marekebisho yake, inayomtaka kila mwajiri kutoa maelezo kwa maandishi
kwa bodi, kuhusu mwajiriwa ambaye ni mnufaika wa mkopo huo, ndani ya
siku 28 tangu mdaiwa alipoajiriwa.
Hatua
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mdaiwa yeyote wa bodi hiyo atakayeshindwa
kulipa deni lake bila sababu za msingi, kwanza atakuwa akikabiliwa na
kesi ya madai chini ya kifungu cha 6 C na H cha Sheria ya Bodi ya Mikopo
namba 9 ya mwaka 2004.
Mbali na kukabiliwa na kesi hiyo, pia mkopo wake kwa namna
unavyochelewa kuanza kulipwa, utakuwa ukijilimbikizia riba ya asilimia
10.
Taarifa hiyo ya bodi imeeleza kuwa mdaiwa huyo taarifa zake
zitapelekwa katika taasisi za kumbukumbu ya mikopo zilizo chini ya Benki
Kuu (BoT), ambazo zitazuia wadaiwa hao kupata mikopo katika mabenki na
asasi zote za fedha.
Mdaiwa huyo pia atazuiwa kupata udhamini wa Serikali katika
muendelezo wa masomo yake, lakini pia atazuiwa kujiunga na chuo chochote
cha elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Aidha kwa mujibu wa taarifa hiyo, taarifa zao pia zitawasilishwa
katika Idara ya Uhamiaji iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
na katika ofisi zote za kibalozi, ili wakose kibali cha kusafiri nje ya
nchi.
Hasara nyingine watakayokabiliwa nayo wadaiwa hao, ni Tozo ya Kulinda
Thamani ya Mkopo (VRF) ya asilimia sita kila mwaka, itakayotozwa kwa
kila mkopo, ili wadaiwa watakapoanza kulipa mkopo waliochukua, walipe
kwa thamani ya sasa.
Tozo hiyo imelenga kuepuka athari ya mfumuko wa bei tangu mdaiwa
aliponufaika, lakini pia kuwezesha urejeshwaji wa deni, uwe na thamani
ya kumhudumia mwanafunzi mwingine mwenye mahitaji kwa sasa na baadaye.
Ambao hawajaajiriwa
Taarifa hiyo pia imeonya wadaiwa wanaodhani kuwa kutokuajiriwa ni
sababu ya kutolipa mkopo huo, kwamba mkopo huo unatakiwa kulipwa baada
ya kumalizika kwa mwaka mmoja tangu mdaiwa alipofanikiwa kuhitimu masomo
yake, au mwaka mmoja tangu mhusika alipokatisha masomo yake kwa sababu
yoyote.
Aidha, taarifa hiyo imeelekeza watakaojitokeza, kama wameajiriwa,
asilimia nane ya mshahara wao wa kila mwezi, itatakiwa kukatwa na
kuwasilishwa kwenye Bodi ili kulipa deni husika.
Lakini pia Bodi hiyo imetengeneza utaratibu kwa ambao hawajaajiriwa,
kwamba wanaweza kulipa kiasi cha chini cha Sh laki moja kila mwezi
katika akaunti za Bodi zilizopo Benki ya Posta yenye namba
CCA0240000032; Benki ya NMB namba 2011100205 na Benki ya CRDB namba
01J1028467503.
Deni lenyewe
Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, hadi Juni 2014, bodi hiyo ilikuwa
imewakopesha wanafunzi Sh trilioni 1.8 kuanzia mwaka wa masomo 1994/95
na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 51 zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya
Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Taarifa hiyo ya HESLB imetolewa siku chache kabla ya Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ya kusitisha
ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatega kwa tuhuma za
udhaifu katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.
Miongoni mwa waliosimamishwa pamoja na Nyatega ni Mkurugenzi wa Fedha
na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma
Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 20 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment