Monday, 8 February 2016

Tagged Under:

Tunu Pinda apata ajali, anusurika kifo

By: Unknown On: 21:37
  • Share The Gag

  • Gari ya Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu, Tunu Pinda baada ya kupinduka.
    MKE wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda (pichani) na wenzake watatu akiwemo dereva wa gari wamenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kupinduka kutokana na kumgonga mwendesha bodaboda eneo la Mkundi Manispaa ya Morogoro katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.
    Ajali hiyo ilitokea saa nane mchana jana katika eneo hilo wakati gari lenye namba za usajili STK 9442 aina ya Toyota Land Cruiser lilipomgonga mwendesha bodaboda akiwa na pikipiki yenye namba MC 647 BBA na kupinduka.
    Mke huyo wa Waziri Mkuu mstaafu na wenzake watatu walijeruhiwa na walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kupatiwa matibabu na kuchunguzwa afya zao. Jioni hiyo hiyo jana waliruhusiwa kuendelea na safari.
    Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alithibitisha kuwapokea majeruhi hao akiwemo Mama Tunu Pinda ambaye hakuumia sana licha ya kupata maumivu kifuani.
    Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, mbali na Mama Tunu, majeruhi wengine ni dereva Angelo Mwisa (50), Gilbert Sampa (40) pamoja na mlinzi wa mke huyo wa Pinda, Gaudencia Tembo.
    Alisema walipata majeraha madogo madogo kwenye mbavu na kifuani na baaada ya kupata matibabu wameruhusiwa kuendelea na safari ya kwenda Dar es Salaam. “Tumepokea majeruhi wanne akiwemo Mama Pinda hawakuumia sana, ni majeraha madogo ambapo dereva ameumia kidogo usoni na hali zao sio mbaya.
    Jioni hii wanaendelea na safari, mikanda waliokuwa wamejifunga imesaidia kutopata majeraha makubwa,” alisema Dk Lyamuya. Alisema hospitali hiyo pia ilipokea mwili wa dereva wa bodaboda ambaye aligongwa katika eneo la tukio hilo na jina lake hadi jana lilikuwa halijatambuliwa.
    Ajali hiyo ilitokana na mwendesha bodaboda aliyekatisha barabara kuu kutoka upande mmoja wa barabara kwenda mwingine bila kuchukua tahadhari na hivyo kusababisha kugongwa na gari hilo na kupinduka.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment