Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikari za mitaa (Tamisemi), George Simbachawene (kulia) akimhoji jambo Mkurugenzi Mtendendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Azimina Mbilinyi, wakati
wa kikao kilichowakutanisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya za
mkoa huo alipokuwa katika ziara mkoani Morogoro.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), George Simbachawene amesema kuwa wakurugenzi wa halmashauri
nchini, wakaoshindwa kutekeleza agizo la kujitosheleza kwa madawati
katika shule ya msingi na sekondari hadi Juni mwaka huu, wajitambue
wameshindwa kazi.
Pia wakurugenzi wa halmashauri watakaozalisha madeni ya watumishi
pamoja na ya wazabuni wa vyakula katika shule za serikali, watakuwemo
kwenye kundi la kuwajibishwa.
Waziri huyo wa Tamisemi alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na
Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro wakiwemo wakuu wa wilaya,
wakurugenzi watendaji wa halmashauri (Ma-DED), makatibu tawala wa
wilaya, na wakuu wa idara za halmashauri zote za mkoa huo chini ya Mkuu
wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
Hivyo alisema agizo lililotolewa na Rais John Magufuli la kutaka
kuona kila mwanafunzi anaketi kwenye madawati, halina mjadala na kwamba
ifikapo Juni mwaka huu pasiwepo na mwanafunzi anaketi sakafuni na
wakurugenzi watakaoshindwa, watakuwa wameshindwa kazi na watawajibishwa.
Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya, ambao ndiyo wasimamizi wa
rasilimali zilizopo katika maeneo yao hasa ya misitu, wasisite kutoa
vibali vya uvunaji wa miti ya kutengeneza madawati kwenye wilaya zao ili
watoto wote waliopo shuleni wawe wanakaa kwenye madawati.
“Tumieni vyema nafasi zenu za kuwa wenyeviti kamati za kutoa vibali
vya uvunaji rasilimali za misitu... ili madawati yaweze kupatikana na
utekelezaji wa matumizi ya vibali hivyo ufuatiliwe ili visitumiwe vibaya
na waliopewa kazi hizo,” alisema Waziri.
Alitoa mfano kuwa Mkoa wa Morogoro ambao una rasilimali nyingi za
misitu, umekuwa na upungufu wa madawati ni 73,972 katika shule za msingi
na 11,038 katika shule za sekondari za serikali.
Pia alisema mkoa una upungufu wa vyumba vya madarasa 4,508 kwa shule
za msingi na madarasa 352 kwa shule za sekondari za serikali wakati eneo
la afya lina upungufu wa zahanati 334.
“Kuna kazi kubwa katika sekta ya elimu ambapo kwa Mkoa wa Morogoro
pekee unakabiliwa idadi ya madawati mengi sembuse wilaya kama ya
Kibaha,” alisema.
Waziri Simbachawene pia alionya tabia ya uzalishaji wa madeni ya
watumishi wa halmashauri na wazabuni, wanaotoa huduma ya vyakula shule
za serikali unaofanywa na watumishi wa Idara ya Uhasibu na maofisa
utumishi kuwa siku zao, zinahesabika na wajiandae kutumbuliwa majipu.
Ili kutekeleza agizo la kukomesha uzalishaji wa madeni, alitoa
maelekezo kwa maandishi kwa wakurugenzi wa halmashauri zote 181 kwa
ajili ya utekelezaji wake.
Alisema halmashauri hizo, zina uwezo wa kulipa madai ya wafanyakazi
wake kama nauli ya likizo, gharama za matibabu na mambo mengine kwa
kutumia fedha za makusanyo yake ya ndani kwa kuwa fedha za mishahara na
mengine zinatolewa na Serikali Kuu.
“Serikali inalaumiwa kwa sababu wakurugenzi hawatekelezi wajibu wao
na matatizo mengi yapo katika Idara ya Uhasibu na Idara ya Utumishi,”
alisema na kuongeza: “Wahasibu ni chanzo cha matatizo yote haya wanakuwa
na mahusiano na wenye kutoa huduma, utakuta deni la shilingi bilioni 25
likihakikiwa linabakia shilingi bilioni tano, zimeongezwa tarakimu hapo
na haya yameshatokea.”
Aliongeza, “Hawa sasa wajiandae kutumbuliwa, tunaelekea ngazi ya
wakuu wa idara wa halmashauri, akitumbuliwa mkurugenzi naye mkuu wa
idara anayehusika na kashfa hiyo atawajibishwa si kwa mkurugenzi pekee.”
Aliwakumbusha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
nchini kutambua jukumu walilopewa la ukamilishaji wa vyumba vya maabara
na wasiokamilisha hicho ni mojawapo ya kigezo cha kupoteza nafasi zao.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 23 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment