Monday, 8 February 2016

Tagged Under:

Magufuli atimiza ahadi Mahakama

By: Unknown On: 21:25
  • Share The Gag
  • Rais Dk John Magufuli.

    RAIS John Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kuipatia Mahakama ya Tanzania Sh bilioni 12.3 kwa lengo la kuiwezesha Mahakama kuimarisha utendaji kazi na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
    Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Sheria wiki iliyopita Dar es Salaam, Dk Magufuli aliagiza Mahakama kupewa fedha hizo ambazo zilitokana na fungu lake katika bajeti ya mwaka 2015/2016.
    Jaji Mkuu Mohammed Chande Othman alisema Idara ya Mahakama, inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha kwani kuanzia mwaka wa fedha wa 2014 na 2015 walipatiwa fedha takribani Sh bilioni 40, lakini wakati mwaka wa fedha unaoishia zilipunguzwa na kufikia Sh bilioni 12.3 ambazo zilikuwa hazijatolewa.
    Kutokana na hilo, Rais Magufuli alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ndani ya siku mbili iwe imeipatia Idara hiyo ya Mahakama kiasi cha Sh bilioni 12.3 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya idara hiyo ili ifanikishe na kutekeleza majukumu yake.
    Akikabidhi fedha hizo mbele ya waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema fedha zilizokabidhiwa kwa Mahakama ni mwitikio wa kutekeleza ahadi ya Rais aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, mwaka huu.
    “Ni matumaini ya Serikali fedha hizo zitatumika vizuri na zitatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa,” alisema Dk Mpango. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju alimshukuru Rais kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ndani ya siku nne na kuudhihirishia umma kuwa kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” anaisimamia kwa vitendo.
    Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga alisema fedha walizokabidhiwa zitasaidia ujenzi wa mahakama nchini na zipo ndani ya bajeti ya mwaka 2015/2016 na watazitumia kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
    Mwanasiasa aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Said Amour Arfi alisema Rais Magufuli tangu alipoapishwa kushika madaraka ya juu ya nchi, ameishi kwa ahadi, kauli na dhamira yake kuleta mabadiliko ya dhati ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
    Akizungumza na gazeti hili akitoa tathmini na mtazamo wake wa utendaji wa Rais Magufuli kuelekea siku zake 100 tangu alipoapishwa na kushika madaraka hayo, Arfi alisema hatua alizoanza kuzichukua kwa kauli na matendo yamefufua matumaini ya Watanzania wakiwa na matarajio makubwa kwa kasi yake hiyo aliyoanza nayo.
    “Licha ya kuwa siku 100 ni muda mfupi lakini utendaji na kasi ya Rais (Magufuli) umetoa dira ya kiuongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa tathmini na mtazamo wangu, leo Rais (Magufuli) anakubalika zaidi kuliko kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana hata wale waliokuwa na mashaka naye na hawakumpa kura, kati yao leo wanajutia maamuzi yao,” alieleza Arfi.
    Arfi aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini (Chadema) mkoani Katavi kwa vipindi viwili mfululizo na baadaye kukihama na kujiunga na CCM, alisema Watanzania wameshuhudia Rais Magufuli akitimiza kauli na ahadi zake. Ahadi na kauli zake hizo, zimetekelezwa kwa kuunda baraza dogo la mawaziri, limewajibika kuondoa kero, ambazo zilikuwa zimewakabili wananchi ndani ya siku 100.
    “Pia tumeshuhudia mawaziri na watendaji wakuu serikalini wakifanya kazi kwa kasi na kuwafikia wananchi kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi au kutoa maelekezo ya kiungozi,” alieleza.
    Alisema pia Rais amejielekeza katika kubana mianya ya upotevu na ubadhirifu serikalini na kuboresha ukusanyaji wa mapato na ukwepaji wa kulipa kodi. “Naamini ataendeleza mapambano haya na kuimarisha makusanyo ya Serikali na kubana matumizi ni hatua sahihi katika kuimarisha nidhamu ya fedha,” alisema na kuongeza:
    “Katika hizi siku 100 tunaona mabadiliko makubwa katika utendaji na uwajibikaji wa watumishi wa umma hawafanyi tena kazi kwa mazoea nidhamu ya utendaji kwa watumishi hao wa umma ndani ya siku hizi 100 unatupa faraja na matumaini makubwa.”

    Chanzo HabariLeo.


    0 comments:

    Post a Comment