Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
imesema imebaini baadhi ya wakurugenzi watendaji na watendaji katika
Manispaa nne, kutoa rushwa kwa maofisa wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti
wa Hesabu za Serikali (CAG), kuficha kasoro walizozibaini na kubadili
hati chafu kuwa safi.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Halima
Mpita amevuliwa madaraka yake kutokana na matumizi mabaya ya madaraka na
upotevu wa fedha za ushuru wa magari.
Akizungumza jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene alisema madudu hayo, ameyabaini baada ya kufanya ukaguzi wa
kina.
“Tumebaini baadhi ya watumishi katika halmashauri zetu ambao wamekuwa
wakitoa rushwa kwa maofisa wa CAG ili kushawishi wakaguzi kuficha
kasoro walizoziona au waandikiwe hati safi pamoja na kuwa na kasoro
nyingi. Ripoti hizi zimekuwa zikipelekwa bungeni na kujadiliwa wakati
sio halisi,” alisema Simbachawene.
Misenyi mkoani Kagera
Simbachawene alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misenyi,
Elizabeth Kitundu alimwagiza Mweka Hazina wake, Majaliwa Bikwaso kutoa
Sh milioni tatu kwa maofisa wa CAG kwa nia ya kuwalainisha ili wafiche
kasoro walizozibaini.
Aliwataja maofisa hao wa CAG w a l i o p e w a fedha hizo kuwa ni Steven Guwawa, John Elias na Kilembi Mkole.
Nanyumbu, Mtwara
S i m b a c h a w e n e alisema Juni 29, mwaka jana, Mkurugenzi Ally
Mohamed Kasenge, Mweka Hazina Pascal Malowe na Mhasibu Emmanuel Mgesa,
walimpatia Sh milioni 3.5 Ofisa wa Ukaguzi wa CAG, F. Mwampashi ambaye
alipokea kwa niaba ya wenzake ili kuficha kasoro walizozibaini.
Mbogwe, Geita
Simbachawene alisema Novemba mwaka jana, Mkurugenzi Abdallah Mfaume
na Mweka Hazina, Lucas Elias Ndombele waliwapa rushwa maofisa wa CAG Sh
milioni 16 ili wafiche udhaifu walioubaini. Maofisa hao ni Mustafa Said,
A.M Chanja, A. Moha na D.S Ndulima.
Alisema pia katika halmashauri hiyo, wakaguzi wa CAG walibaini
matumizi ya zaidi ya Sh milioni 236.8 yalifanywa bila kuwapo nyaraka za
kuthibitisha na Sh milioni 144.2 zililipwa kwa mkandarasi, bila kazi
iliyokusudiwa kufanyika na wafanyakazi 82 walionekana katika orodha ya
wafanyakazi hivyo k u l i p w a mishahara hewa.
“ N o - vemba 30, mwaka jana, kilifanyika kikao kati ya wakaguzi na
uongozi wa halmashauri a m b a c h o k i l i h u d h u l i w a na Kaimu
Mkurugenzi Sebastiani Nasoro aliyesema ameagizwa Mkurugenzi Abdalla
Mfaume awapatie Sh milioni 12 ili kuficha kasoro na kupewa hati safi.”
Aliwataja maofisa wa CAG waliopewa fedha hizo kuwa ni Rejea Mataka, Abdallah Kisura, A.J Cheile, A. M. Chanja, Mustafa Said.
“Katika halmashauri hiyo pia, Felisia Shilembi ambaye ni mfamasia wa
wilaya na mhasibu wa afya Calistusi Nyoni walitoa shilingi milioni 3 kwa
A.J Chile mkaguzi wa mkoa wa Geita ili kuficha kasoro ya kupotea kwa
fedha Sh milioni 90 zilizokuwa zinunue dawa na vifaa tiba.
Kilolo mkoa wa Iringa
Simbachawene alisema; “Agosti 23 mwaka jana, Lacosoni Pila wa Idara
ya Fedha alimpa fedha Sh 245,000 Ofisa wa CAG ambaye hakumtaja jina ili
afumbie macho kasoro alizoziona. “Naagizwa mamlaka husika za nidhamu kwa
watu hawa kuwachukuliwa hatua na pia namuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha
anawashughulikia wakurugenzi waliohusika kwa kuwasimamisha ili kupisha
uchunguzi wa huhuma dhidi yao.
“Nakemea tabia ya kubadili hati chafu na kuwa hati safi, kwani
inakwamisha juhudi za serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Hatuwezi kuendelea na watu wasiotaka kubadilika ambao wanaathiri maisha
ya wananchi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za rushwa kwa wakaguzi kutoka kwenye ofisi
yake, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa
Assad alisema ni mapema sana kwa ofisi yake kulizungumzia hilo.
Kuhusu Mamlaka ya Mji wa Tunduma, Simbachawene alisema: “Kwa mamlaka
niliyonayo namvua madaraka Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma, Halima Mpita
kuanzia leo kutokana na matumizi mabaya ya madaraka, kwani waliweza hata
kuwatumia watoto wake kwenye shughuli za halmashauri na kuwalipa posho
na upotevu wa fedha za ushuru wa magari yanayopita mpakani.
Alisema nafasi ya Mpita sasa itashikiliwa na Eric Mapunda, ambaye
kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Idara ya Utawala jiji la Mbeya.
Chanzo HabariLeo.
Wednesday, 17 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment