Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers Ltd (TSN)
inayochapisha magazeti ya Serikali ya Daily News, Sunday News, HabariLeo
na SpotiLeo. Waziri alifanya ziara katika Ofisi TSN barabara ya Nandera jijini Dar es salaam.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaka
magazeti ya Serikali kumsaidia Rais John Magufuli, kutumbua majipu kwa
kuibua uozo serikalini.
Akizungumza katika kikao cha wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania
Standard (Newspapers) Ltd Dar es Salaam jana, inayochapisha magazeti ya
Daily News, HabariLeo na Spotileo, Nape ametaka magazeti hayo
yasimung’unye maneno kwa kuandika ukweli; kwenye nyeusi yaandike nyeusi
na kwenye nyeupe, yaandike nyeupe.
Alisema vyombo vya habari vya Serikali vina wajibu wa kumsaidia Rais
kutumbua majipu kwa kuandika habari bila woga, upendeleo wala kuomuonea
mtu, ili kama kuna dosari ziko mahali ziibuliwe kwa lengo la kupata
suluhu.
“Unajua vyombo vya habari vinaaminika na vinasomwa na wengi na hasa
wananchi wanapotaka ukweli wa jambo, wanaangalia kama limeandikwa, sasa
kama jambo litaandikwa kwa kufichwa fichwa haitaisaidia Serikali, kama
ni nyeusi sema nyeusi, kama ni nyeupe sema nyeupe na hiyo ndiyo suluhu,”
alisisitiza Nape.
Alisema majipu yanayoendelea kutumbuliwa na Rais, mengine yanaibuliwa
na vyombo vya habari na ili kumsaidia na kusaidia Taifa, vyombo vya
habari vya Serikali lazima viibue hayo, pia viaminiwe mpaka na watumishi
wa Serikali, wavitumie kuibua uozo.
Nape alisisitiza kwamba kuficha ukweli kwenye jambo ovu, ni kuendelea
kuharibu hivyo kuibuliwa kwa maovu kutaisaidia Serikali na watendaji
wake kuchukua hatua madhubuti. “Kuna hili jambo la baadhi ya watendaji
kusema mfumo hautaki hili, hakuna cha mfumo ni maneno yao wanayatumia
kama kichaka cha kufanya uchafu,” alisema Nape.
Nape alitoa onyo kwa watendaji wa serikali kuacha tabia ya kuzuia
habari zisitoke kwa maslahi yao na kutaka wenye pingamizi ya kutoka kwa
habari, wawasiliane naye na si kuingilia chombo cha habari.
Katika taarifa ya wafanyakazi wa TSN kwa Waziri huyo, walimuomba
kuangalia changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na maslahi duni, uhaba wa
vitendea kazi na baadhi ya viongozi kufanya uamuzi kwa kukiuka sheria na
utaratibu.
Akijibu hoja kuhusu Muundo wa Utumishi wa kampuni hiyo, ambao
umelalamikiwa na wafanyakazi kuwa umepitwa na wakati na umekuwa na
malalamiko mengi ya upendeleo, Nape alitoa mwezi mmoja kwa Menejimenti
ya TSN, kulifanyia kazi na kulimaliza.
“Sipendi kufukuza watu kazi, ila inapobidi itafanyika, natoa mwezi
mmoja menejimenti na mtu wa utumishi kaeni, pitieni muundo huo... kwanza
umeisha muda wake uletwe mpya na wafanyakazi walipwe malimbikizo ya
nyongeza ya mishahara kwa muda wote ambao hawajaongezwa,” alisisitiza
Nape.
Kuhusu Mkataba wa Hali Bora kwa Wafanyakazi, Waziri Nape alitoa siku
saba kwa Menejimenti ya TSN kupitia upya mkataba huo na kuhakikisha
unazingatia maslahi ya watumishi.
Akizungumzia dosari nyingine zilizopo katika kampuni, Nape alisema
ukaguzi mkubwa wa hesabu za kampuni utafanywa na ripoti yake itatumika
kuchukua hatua zaidi kwa wahusika.
Akizungumzia miradi ya kampuni ambayo kwa miaka mingi imekuwa
ikizungumzwa bila kutekelezwa, Nape aliagiza mikabata yote ya miradi
hiyo ipelekwe mezani kwake, ili ichunguzwe kuona wapi imekwama.
Nape alisema ni vyema watendaji wanapokubaliana na wafanyakazi,
utekelezaji ufanyike na wanapoona wameshindwa, ni vyema kurudi mezani
kuwaeleza watumishi, badala ya kukaa kimya.
“Tujenge utamaduni wa kuheshimu taratibu tunazojiwekea, kama
mlikubaliana mambo, mkashindwa kutekeleza ni vyema mkarudi mezani
kuzungumza na si kukaa kimya, jambo ambalo wafanyakazi wanatafsiri
wanavyojua wao,” alisema Nape.
Aliagiza menejimenti ya TSN, kuweka wazi kwa sifa na vigezo mambo
yanayowahusu watumishi ikiwa ni pamoja na muundo wa utumishi,
upandishwaji madaraja na mshahara ili watumishi wasinung’unike na kila
mmoja ajue kesho yake baada ya kujiendeleza.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu,
Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (Raawu) tawi la TSN, Oscar
Mbuza, alimkabidhi Waziri Nape orodha ya mambo ambayo wafanyakazi
wamekuwa wakiyadai kwa miaka mingi bila mafanikio na kusema ujio wa
Waziri huyo utaleta suluhu, kwani morali ya watumishi kazini ilishuka.
“Wafanyakazi pamoja na kuendelea kufanya kazi, lakini morali ya kazi
imeshuka kwa kiwango kikubwa sana, hii ni kwa sababu ya maslahi duni ya
wafanyakazi ya muda mrefu, ila ujio wako tunatumaini utaleta suluhu na
watumishi watapata ari mpya ya kufanya kazi,” alisema Mbuza.
Chanzo HabariLeo.
Friday, 26 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment