Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi |
RAIS Pierre Nkurunziza wa Burundi amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa hali ya Burundi ni shwari na kwamba tangu juzi nchi hiyo imepokea ugeni mkubwa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na inatarajia kupokea marais watano kutoka nchi za Umoja wa Afrika kesho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, ujumbe wa Rais Nkurunziza umewasilishwa na Mjumbe Maalumu ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Leontina Nzeyimana Ikulu Dar es Salaam jana, alipokutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo.
Pamoja na kumpa taarifa kuwa Burundi inaendelea vizuri, Nzeyimana pia alimueleza Rais Magufuli kuwa Burundi ipo tayari kupokea nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Rwanda, ikiwa ni kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaoelekeza kuwa nchi inayofuata kutoa Katibu Mkuu baada ya Katibu Mkuu wa sasa kumaliza muda wake, ni Burundi.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao nchini.
Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frederiks aliwasilisha salamu za Mfalme wa Uholanzi, Mtukufu Willem- Alexander ambaye amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizoonesha katika mwanzo wa utawala wake katika kusimamia uadilifu serikalini na katika biashara na pia kuisaidia Mahakama.
Alisema Uholanzi inaamini kuwa maeneo hayo ndio yamekuwa yakileta vikwazo vya maendeleo, biashara na uwekezaji, na alimhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ilivyofanya katika miaka 45 iliyopita huku akitaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano kuwa ni kilimo na nishati.
Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliwasilisha salamu za Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambaye pamoja na kuitaja Tanzania kuwa lango muhimu katika mpango wake wa ushirikiano na Afrika, alimhakikishia kuwa India itaendeleza uhusiano wake na Tanzania hususani katika biashara na uwekezaji ikiwemo kuunga mkono mpango wa ujenzi wa viwanda Tanzania.
Kwa upande wake, Rais Magufuli aliwahakikishia mabalozi hawa kuwa serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na nchi hizo.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment