UJAMBAZI wa kutumia vifaa vya kivita umeibuka jijini Dar es Salaam,
ukiwemo uliofanyika katika uporaji wa Benki ya Access juzi, ambako
majambazi walitumia bunduki za kivita aina ya SMG na mabomu ya kurusha
kwa mkono.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Simon Sirro, alisema mbali na uvamizi huo, pia Polisi imebaini na
kukamata askari bandia, waliokuwa na sare rasmi za Jeshi la Polisi zenye
vyeo na redio call, zenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya askari
Polisi.
Akizungumzia matukio hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwanga alisema atakutana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk Hussein Mwinyi, ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na
Jeshi la Polisi, waanzishe msako wa pamoja dhidi ya wahalifu hao.
Uvamizi, mauaji Mbagala
Akisimulia ujambazi uliofanyika katika Benki ya Access Tawi la
Mbagala, Kamanda Sirro alisema majambazi hao walikuwa 12, wakiwa
wamepakizana kwenye pikipiki sita na walifika kwenye benki hiyo saa 8:30
mchana.
Baada ya kufika, moja kwa moja waliingia kwenye chumba cha askari
wanaolinda benki na kumpiga risasi kichwani askari mwenye namba H7739
Konstebo Harid na kufa papo hapo.
Mbali na mauaji hayo, Kamanda Sirro alisema walimshambulia askari
mwingine, Konstebo Shaban miguuni na kupora silaha zao na kuingia nazo
ndani ya benki, ambako walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya
ulinzi na raia wengine wawili na kufa papo hapo, huku wengine watano
wakijeruhiwa.
Baada ya hapo kwa mujibu wa Kamanda Sirro, majambazi hao walikimbilia
chumba kinachohifadhi fedha nyingi (strong room) na kukipiga risasi
katika jitihada ya kutaka kuingia ndani, lakini hawakuweza kuvunja.
Kutokana na ugumu wa kuvunja chumba hicho, Kamanda Sirro alisema
haraka haraka wakahamia katika kaunta za watoa fedha na kupora fedha
zilizokuwepo kati ya Sh milioni 20 mpaka Sh milioni 30 na kuondoka na
silaha za polisi aina ya SMG mbili na ile yao moja pamoja na pikipiki
zao.
Polisi waua watatu
Kamanda Sirro alisema taarifa zilisambazwa katika vikosi vya ulinzi, ambavyo vilijiimarisha.
Alitaja Kikosi cha Mbwa na Farasi eneo la Mkuranga, ambao walijiandaa
na majambazi hao walipofika kijiji cha Chui wilayani Mkuranga mkoani
Pwani, walipambana na polisi na askari wakafanikiwa kuua majambazi
watatu.
Mbali na kuua watatu, silaha tatu zilikamatwa ambazo ndio zile SMG
mbili za Polisi, walizochukua pamoja na ile yao moja, lakini wakakutwa
pia na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezwa Urusi.
“Hawa majambazi walikuwa wamejiandaa, kwa maana walikuwa na mabomu ya
kutupwa kwa mkono matatu aina ya RGD 01 ambayo ni mbinu ya kujilinda
wanaposhambulia,” alisema Kamanda Sirro.
Tisa watoroka
Pamoja na kujiimarisha kwa polisi, majambazi tisa walikimbia wakaacha
pikipiki zote sita za aina tofauti, ambazo ni Haojue mbili zenye namba
MC 560 AED na MC 207 BAN, San LG yenye namba MC 784 BDJ, Boxer yenye
namba MC 248 AXE na King Lion mbili zenye namba MC 653 BDQ na MC 853
BDR.
Kamanda Siro alisema baada ya hapo, waliendelea kuwakimbiza majambazi
hao hadi wakatokomea katika Msitu wa Kongowe, ambako juhudi za
kuwatafuta zilianza mara moja.
“Nawahakikishia wananchi mtandao wote wa ujambazi kwenye mabenki na
maeneo mengine, tutausafisha wote kwa maana hawa wanafanya uhalifu
maeneo ya Dar es Salaam na Pwani na wana ndugu zao, tutawakamata wote,”
alisisitiza Kamanda Sirro.
Alisema hawawezi kuona Watanzania wakiumia na kufa kwa tamaa za wachache, wenye kupenda utajiri wa haraka.
JWTZ kazini
Akizungumza kuhusu ujambazi huo, Waziri Kitwanga alisema Polisi
inajipanga upya na atazungumza na Waziri mwenzake, Dk Mwinyi kuangalia
jinsi ya majeshi hayo mawili, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), watakavyofanya kazi pamoja ya msako katika misitu yote
inayozunguka mikoa ya Pwani, kuanzia Bagamoyo hadi Kisarawe.
Alionya kama kuna kambi za uhalifu ndani ya misitu hiyo, zitasambaratishwa na kuomba raia wema watoe taarifa za uhalifu.
“Tutafanya operesheni kubwa na tutaifanya haraka, tunaomba wananchi
watoe ushirikiano hasa waendesha bodaboda kwa maana zinatumika sana
kwenye matukio haya. Mtandao wa majambazi ufahamu kwamba vyombo vya
usalama havijalala, tutawamaliza wote, tutatumia nguvu zetu zote
kuwamaliza na tutafanikiwa,” alisisitiza Kitwanga.
Kuhusu waendesha bodaboda, Kitwanga alisema ukaguzi wa kina unafanywa
na kuwataka waendesha bodaboda hao wanaposimamishwa, wakubali na kutoa
ushirikiano na wasione kama wanabughudhiwa, bali ni kuwakagua kwa sababu
wahalifu hutumia vyombo hivyo zaidi kufanya matukio mabaya.
Polisi feki
Katika tukio jingine, Kamanda Sirro alisema polisi feki wanne
wamekamatwa na wanashikilia kwa mahojiano, ili kubaini mtandao huo ambao
unatumia sare za Polisi, redio za upepo na pingu kufanya matukio ya
uhalifu.
Alisema walipata taarifa kutoka kwa raia wema ya kuwepo kwa mtandao
wa askari bandia, ambao hutumia sare za jeshi hilo kufanya matukio ya
uhalifu, ndipo walipowakamata hao wanne. Kwa mujibu wa Kamanda Sirro,
polisi feki watatu walikamatwa Februari 24, asubuhi saa mbili eneo la
Upanga karibu na Daraja la Selander.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kuhojiwa, walikiri kufanya matukio ya
ujambazi kwa kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja
anayeishi Kinyerezi. Kamanda Siro alisema Polisi walimfuata mtuhumiwa
huyo nyumbani kwake Kinyerezi na walipofanya upekuzi, walimkuta na sare
halisi ya Polisi, redio ya upepo na pingu.
Kamanda Sirro alisema baada ya uchunguzi, imebainika kwamba
watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia sare na vifaa hivyo vya Polisi,
kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi kwa kujiaminisha kuwa wao ni
askari Polisi.
Alisema watuhumiwa hao wamekiri kufanya matukio mbalimbali, ikiwemo
kuweka vizuizi katika barabara za mikoani na kufanya uporaji.
“Watuhumiwa hao wote wanahojiwa ili waeleze jinsi walivyopata sare na
vifaa hivyo ya Polisi, wamekiri kufanya uhalifu maeneo mbalimbali,
lakini wakati mwingine tunashindwa kukamata wahalifu kwa sababu redio
call wanayotumia zinaingiliana na zetu, hivyo wanakuwa wamepata
taarifa,” alisema Kamanda Sirro.
Katika tukio lingine, Februari 18 mwaka huu, watuhumiwa watatu wa
ujambazi, walikamatwa eneo la Kiwalani Kwa Mkude jijini Dar es Salaam
wakiwa na bastola moja.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 27 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment