Saturday, 27 February 2016

Tagged Under:

Morogoro waomba Ulanga kuwa mkoa

By: Unknown On: 22:10
  • Share The Gag

  • Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe

    WAJUMBE wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Morogoro (RCC) wamepitisha pendekezo la uanzishwaji mkoa mpya wa Ulanga, ambao utakuwa na wilaya tatu za Kilombero, Malinyi na Ulanga.
    Mkoa huo mpya, utatokana na kugawanywa mkoa mama wa Morogoro.
    Pendekezo hilo lilifikiwa baada ya kupitishwa na vikao vya ushauri vya halmashauri za wilaya (DCC) za mkoa wa Morogoro na kufikishwa kujadiliwa na kupitishwa katika kikao cha RCC, kilichofanyika juzi chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
    Kwa sasa mkoa wa Morogoro una wilaya saba za Morogoro, Kilosa, Mvomero, Gairo, Kilombero, Ulanga, Malinyi na una eneo la kilometa za mraba 73,039.
    Eneo hilo ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara.
    Katika kikao hicho cha RCC, Dk Rutengwe aliwaagiza watendaji wa serikali za wilaya, kukamilisha taratibu mbalimbali za kisheria na kuwashirikisha wananchi kabla ya kufikiwa hatua za mwisho za uwasilishaji rasmi wa pendekezo la kuanzishwa mkoa mpya kwa mamlaka zinazohusika.
    Alitumia pia kikao hicho, kuagiza maofisa mipango miji na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero kuandaa michoro ya mipango miji ya kisasa, itakayokidhi upatikanaji wa huduma zote muhimu za kiuchumi na kijamii.
    Awali, Mkuu wa Mkoa huyo aliliwasilisha pendekezo hilo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili kati ya Februari 22 na 23, mwaka huu mkoani Morogoro.
    Dk Rutengwe alisema mchakato huo, ulianza kufanyika tangu mwaka 2014 na sasa umefikia mahali pazuri, kwa kuwa suala hilo limefikishwa mezani kwake na kuwa limetokana na mazingira ya kijiografia na ukubwa wa mkoa huo, lengo likiwa ni kusogeza huduma za kijamii na kiutawala karibu na wananchi.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment