Tuesday, 23 February 2016

Tagged Under:

Kampuni Ya Kichina Matatani Kwa Kutengeneza Vibao Vya Namba Za Magari Kinyume Cha Sheria

By: Unknown On: 22:36
  • Share The Gag

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya msako wa kushtukiza katika kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development Ltd iliyoko Barabara ya Nyerere Dar es salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema na kukamata vifaa pamoja na malighafi za kutengeneza na kutoa vibao vya namba za pikipiki kinyume na sheria.

    Katika msako huo uliofanyika tarehe 19 Februari 2016 katika kampuni hiyo, Maofisa wa TRA waliweza kukamata na kutaifisha vibao vyenye namba za pikipiki 2,500 na vibao 5,600 ambavyo havikuwa na namba. Pia maofisa wa TRA walikamata malighafi za rangi ya vibao katoni tatu, pamoja na mashine ya kupaka vibao rangi yenye uzito wa kilo 155.

    Mashine nyingine iliyokamatwa katika msako huo ni ya kutengeneza namba za magari yenye uzito wa kilo 902 ambayo imezuiwa isihamishwe kutoka katika kampuni hiyo pamoja na kompyuta mpakato ambayo imepelekwa katika maabara ya uchunguzi TRA kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    Taarifa za kuwepo kwa utengenezaji wa vibao vya magari kinyume na taratibu na sheria zilitolewa na msamaria mwema ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni husika Donglinh Guo, Meneja wa Kiwanda Yong Qing Cheng na Meneja wa ghala Peng Zhan walikamatwa baada ya kutokea fujo wakati wa msako na kufikishwa katika kituo cha Polisi Changombe.

    Kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development LTd ndio waingizaji pekee wa pikipiki za Falcon tangu mwaka 2008 ambapo inatuhumiwa kutoa vibao vya namba za pikipiki kwa wateja wake kwa shilingi 5,000 kinyume na sheria.Uchunguzi wa thamani ya kodi iliyopotea bado unaendelea.
     
    Vibao vya magari na pikipiki hutolewa na kampuni ambazo zinatambuliwa na TRA baada ya kupewa idhini. Kampuni hizo ni Masasi Sign, Auto Zone, Sign Industry, Kiboko, Budda Auto works, Parkinson Ltd na Next Telecom.

    Ili kujiridhisha kuwa kadi za pikipiki zinazotolewa kwa wateja wa kampuni hiyo ni halali, TRA ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa kadi hizo zinatolewa kihalali.

    TRA inawatahadharisha wananchi kufuata taratibu na sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea endapo watagundulika kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    0 comments:

    Post a Comment