Friday, 12 February 2016

Tagged Under:

Ikulu yajitathmini siku 100 za JPM

By: Unknown On: 21:57
  • Share The Gag

  • Rais Dk John Magufuli.

    KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametoa tathimini ya Ikulu ya siku 100 za Rais John Magufuli, baada ya jamii ya Watanzania, wanasiasa na wasomi kutoa yao katika vyombo mbalimbali vya habari.
    Katika tathmini aliyoitoa jana, Balozi Sefue amesema japo siku 100 ni chache sana kufanya tathmini ya kina, zinatosha kuonesha mwelekeo wa Serikali na kupata kionjo cha uthabiti wa dhamira yake ya kutekeleza ahadi zake kwa wananchi. Mapato Akizungumzia tathmini ya ukusanyaji mapato, Balozi Sefue amesema katika siku 100 za kwanza, Serikali imefanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi na mapato yasiyo ya kodi.
    “Katika kipindi cha siku 100 za kwanza, mapato ya kodi yameongezeka hadi kufikia Sh trilioni 3.34, ikilinganishwa na makusanyo ya Sh trilioni 2.59 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2014/15. “Hilo ni ongezeko la Sh bilioni 746.31. Hali kadhalika, kwa mapato yasiyo na kodi, makusanyo yameongezeka hadi kufikia Sh bilioni 281.68, kutoka Sh bilioni 224.03 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2014/15, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 57.65,” amesema.
    Akitoa mfano wa makusanyo yasiyo ya kodi, Balozi Sefue amesema jamii imesikia, baada ya kashkashi pale Hospitali ya Taifa Muhimbili, mapato yake yameongezeka maradufu na kuwapa uwezo mkubwa zaidi wa kuhudumia wananchi na hali hiyo pia iko kwenye halmashauri. “Ukusanyaji huu wa mapato umeiwezesha Serikali kugharamia baadhi ya miradi yake kwa fedha za ndani, mathalan kuwalipa wakandarasi, kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, miundombinu, umeme, kilimo, uwezeshaji wa vijana na kadhalika.
    “Naamini kasi iliyopo sasa itaongezeka kwa siku zijazo na kutupatia uhuru zaidi wa utekelezaji wa mipango yetu. Kwa msingi huo nawasihi wananchi wadumishe uzalendo kwa kulipa kodi kwa kila bidhaa wanazonunua, kwani mapato hayo ni kwa ajili ya kuwahudumia. Pia msisite kutoa taarifa za wakwepa kodi, ambao watashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria,” alisema.
    Ubanaji matumizi Akizungumzia jitihada zilizochukuliwa katika kubana matumizi, Balozi Sefue amesema katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa kufuata vipaumbele muhimu, imefanikiwa kuokoa baadhi ya fedha zilizokuwa zitumike katika mahitaji yasiyo ya kipaumbele na kuyapeleka katika vipaumbele. Kwa mfano, katika safari za nje ambazo zilizuiwa, Balozi Sefue amesema fedha zilizookolewa zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.
    “Zaidi ya Sh bilioni saba ambazo zingeweza kutumika kwa safari za nje, zimeokolewa katika siku 100 na zitatumika kwenye miradi hiyo ya maendeleo,” alisema. Fedha zingine zilizookolewa katika mahitaji yasiyo ya kipaumbele na kupelekwa kwenye mahitaji ya kipaumbele ni pamoja na zile za kugharamia sherehe za Uhuru. “Badala ya sherehe za Uhuru, tumefanya usafi ili kupambana na kipindupindu, fedha zilizookolewa zinajenga sehemu ya barabara iliyokuwa kero kubwa kwa wananchi,” alisema.
    Zingine ni zile za wabunge kujipongeza kwa sherehe kubwa, ambazo zimetatua tatizo la vitanda kwa wagonjwa na za sherehe za siku ya Ukimwi, zilizokwenda kununua dawa za kupambana na makali ya Ukimwi. Pia zipo fedha za semina elekezi ya mawaziri, ambazo zitakwenda kutekeleza mradi wa kufunga vifaa vya kisasa vya kuchunguza magonjwa katika hospitali 37 kote nchini. “Hatua hizo na nyingine nyingi, zimevuta hisia za watu mbalimbali kote duniani.
    Mnaofuatilia mitandao ya kijamii mnajua hivyo na wapo wameonesha wazi kutamani tungewaazima Rais wetu kwa muda,” alisema. Safari za nje Akizungumzia Sera ya Mambo ya Nje, Balozi Sefue amesema Tanzania inajivunia msingi imara wa diplomasia na uhusiano mzuri wa kimataifa, uliowekwa na viongozi, kuanzia Awamu ya Kwanza iliyojikita katika ukombozi wa Mwafrika na jamii nyingine zinazotawaliwa duniani, hadi Awamu ya Nne iliyoendeleza diplomasia ya uchumi.
    Alifafanua kuwa Rais Magufuli, anatambua pia kwa nadharia ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa, inabainisha kuwa sera ya mambo ya nje, inaakisi sera za ndani ya nchi. “Tofauti na wanaomlaumu Rais kwa kutosafiri nje ya nchi, Rais wetu anafahamu na kushukuru sana kuwa marais waliomtangulia wamefanya kazi kubwa na nzuri sana ya kujenga uhusiano wetu na nchi za nje na kuimarisha diplomasia yetu.
    “Lakini Rais anatambua kuwa ili ailinde sifa hiyo na kuikuza, lazima anyooshe mambo kadhaa ndani ya nchi. Iwapo Tanzania itabaki kuwa maskini, yenye rushwa, ujangili, dawa za kulevya na kadhalika, hiyo sifa nzuri nje ya nchi itaporomoka. “Hivyo ameamua kujipa muda kuimarisha uchumi na maendeleo ndani ya nchi, kupambana na matatizo mengine yanayoharibu sifa yetu, ili iwe rahisi kudumisha sifa ya Tanzania nje ya nchi,” alisema.
    Alisema hatua anazochukua Rais Magufuli kuimarisha mifumo na utendaji wa ndani, umeipa sifa kubwa Tanzania huko nje pamoja na kwamba yeye binafsi hajasafiri kwenda nje ya nchi, tangu achaguliwe kuwa Rais. Kwa hatua hiyo, Balozi Sefue amesema imedhihirisha wazi kuwa mambo ya ndani ya nchi yasiposhughulikiwa ipasavyo, kusafiri tu kwa Rais nje siyo kigezo cha kudumisha heshima na urafiki mwema.
    “Napenda niwahakikishie wananchi wote kuwa dunia inafuatilia yanayotokea nchini na wana shauku ya kuona matokeo yake. Kila kona hivi sasa, nchi zinazungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya siku 100. “Hili ni jambo la kujivunia katika mahusiano yetu na nchi za nje na ni jambo kubwa kidiplomasia. Rais amefanya kazi ya kutangaza Tanzania na kujenga sifa yake bila hata ya kusafiri. Atakapokuwa tayari atasafiri tu,” alisema.
    Maono ya Magufuli Akizungumzia maono ya Rais Magufuli, Balozi Sefue alisema tangu wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais Magufuli aliweka bayana maono ya Tanzania anayotaka kuijenga, na nini kifanyike ili kutimiza azma hiyo. Alisema maono na shauku yake, kama ilivyo kwa watendaji wote, ni kujenga Tanzania mpya yenye uhuru, haki, neema na fursa mbalimbali kwa wananchi wote; amani na utulivu, uchumi imara unaotegemea viwanda na Tanzania ambayo kila mtu ananufaika na rasilimali zilizopo na isiyo na rushwa, ufisadi na dhuluma.
    Katika kutimiza maoni hayo, Balozi Sefue amesema Serikali yake iliahidi kuendeleza misingi imara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii iliyojengwa na awamu zilizotangulia na kuzingatia vipaumbele vifuatavyo. Mosi, Balozi Sefue amesema itakuwa kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa uamuzi na miradi ya Serikali na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wenye maslahi kwa Taifa, hususan katika sekta ya viwanda.
    Pia Serikali imedhamiria kubana matumizi, kwa kupunguza yale ambayo kwa kuzingatia hali yetu ya uchumi kwa sasa, yanaweza kuepukika na kuimarisha huduma za jamii, hasa katika maeneo yenye kero zaidi kwa wananchi. Aidha, rais amedhamiria kuhimiza na kusimamia utii wa sheria, kurejesha nidhamu ya Serikali na uzingatiwaji wa maadili kwa viongozi wa umma na watumishi wote wa Serikali, sekta binafsi na watu wote kwa ujumla.
    Balozi Sefue alisema pia Rais amedhamiria kudumisha ulinzi na usalama, kuendeleza mahusiano mazuri na yenye tija baina ya Tanzania na nchi za nje, mashirika na taasisi za kikanda na kimataifa, pamoja na wabia wengine wa maendeleo. Faraja Katika siku hizo 100 za kwanza za utawala wa Awamu ya Tano, Balozi Sefue amesema Serikali imefarijika kuona wananchi wengi, bila kujali itikadi zao, walivyoonesha imani kubwa kwa Rais na Serikali yake na jinsi wanavyoiunga mkono.
    “Kwa upande mwingine tumeshuhudia jinsi Mheshimiwa Rais na Serikali yake ilivyo karibu na wananchi na namna wananchi wanavyozidi kumfurahia Rais wao. “Wananchi wanafanya hivyo kwa vile wamemkubali kama kiongozi wao na wanamwamini. Hivyo moja ya mafanikio makubwa katika hizi siku 100 ni vile ambavyo Rais ameweza kujijengea imani kubwa miongoni mwa wananchi wenzake, kuwaunganisha katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao bila kuangalia vyama, dini, kabila na rangi zao,” amesema Balozi Sefue.
    Alisema akitakiwa kuelezea kwa maneno machache sana siku 100 za utawala wa Rais Magufuli, atasema, ameiletea nchi aina mpya ya uongozi, unaojenga juu ya msingi wa waliomtangulia, lakini unaoweka Tanzania katika gia mpya kuelekea uchumi wa kipato cha kati ulioahidiwa na Dira ya Maendeleo 2025.

    Chanzo Gazeti La HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment