NA HASSAN HAMAD (OMKR), PEMBA
MGOGORO wa uchaguzi visiwani Zanzibar umeingia katika sura nyingine
baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad kusema kuwa watakwenda mahakamani kuzuia kuchaguliwa kwa
wawakilishi na madiwani wengine.
Alisema hawataruhusu viongozi wengine wa ngazi hizi kuchaguliwa tena
kwa vile tayari wawakilishi na madiwani wateule wa CUF wamechaguliwa
kihalali na wananchi na kukabidhiwa hati zao za ushindi baada ya
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif
Sharif Hamad, kwenye viwanja vya Nngoma Hazingwa, mjini Chake Chake,
kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi wa wilaya, majimbo na
jumuiya za chama hicho.
“Tutakwenda mahakamani kutetea nafasi zao na kutoruhusu viongozi
wengine wa ngazi hizi kuchaguliwa tena kwa vile wanavyo vielelezo vyote
vya kuchaguliwa,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni makamu wa kwanza wa
rais wa Zanzibar.
Alisema matokeo ya uchaguzi yaliyobandikwa kwenye vituo vya kupigia
kura na kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, majimbo 18
ya uchaguzi kisiwani Pemba yalichukuliwa na CUF pamoja na wadi zote 32.
Katika hatua nyingine, Maalim Seif aliyegombea urais kwa tiketi ya
CUF, amewapa matumaini wafuasi wa chama hicho kuwa atatangazwa mshindi
wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana na hatimaye kuiongoza Zanzibar.
Alisema kinachofanywa na watawala ni kuchelewesha kumtangaza, lakini hakuna namna yoyote CCM kuendelea kuongoza Zanzibar.
Maalim Seif alisema jumuiya na waangalizi wa kimataifa wote walisema uchaguzi ulikuwa huru, haki na wa uwazi.
Alisema kamwe chama chake hakitashiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20.
Chanzo Mtanzania.
Thursday, 4 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment