Friday, 19 February 2016

Tagged Under:

Tunataka fair play Simba na Yanga

By: Unknown On: 23:26
  • Share The Gag

  • MIAMBA ya soka nchini, Yanga na Simba inachuana leo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tayari kila timu imeshacheza michezo minane, hivyo mchezo huo una kila umuhimu kwa timu zote kuhakikisha kila moja inaibuka na ushindi. Tunaamini kila timu imejiandaa vya kutosha na waamuzi wa mchezo huo watachezesha kwa kufuata sheria zinavyotaka.
    Tunatambua fika asiyekubali kushindwa si mshindani, kwani katika soka kuna matokeo ya aina tatu, ambayo ni kushinda, kufungwa au sare. Kwa mazingira hayo, mashabiki wa klabu zote hizo wawe tayari kwa matokeo ya aina yoyote.
    Imezoeleka timu zinapofanya vibaya huwa hazikosi sababu, ambazo si za kitaalamu na zaidi ni kutupiana lawama zisizo na msingi kuanzia uwanjani na hata wengine kutaka kufanya fujo. Wapo watakaokimbilia kulaumu waamuzi na kutaka kufanya vitendo visivyo vya kiungwana na hata wengine kufikia kulaumu wachezaji wao na mambo mengi yasiyo ya kistaarabu.
    Pia hatuna haja ya kunyoosheana vidole, lakini ni wajibu wa waamuzi kuhakikisha wanachezesha kwa kufuata sheria 17 zinazotawala mchezo huo.
    Pamoja na waamuzi, lakini pia kumekuwa na vitendo visivyo vya kiungwana nje ya uwanja na ndani ya uwanja ambavyo huwa haviepukiki sana, lakini tunaamini vinaweza kupungua kama wachezaji wakitumia kauli mbiu ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa) inayosisitiza mchezo wa kiungwana ‘Fair Play’.
    Vitendo visivyo vya kiungwana nje ya uwanja navyo huwa vinatawala sana michezo hii kiasi kwamba wakati mwingine Polisi hulazimika kutumia nguvu kwa baadhi ya mashabiki. Tunaomba wachezaji, viongozi, makocha na mashabiki wajiepushe na vitendo vya aina yoyote visivyo vya kiungwana, ambavyo vinatia doa mchezo huo.
    Vitendo visivyo vya kiungwana nje ya uwanja hivi wahusika wa usalama ni wazi wapo makini na watalifanyia kazi kuhakikisha mechi inachezwa kwa amani. Lakini mashabiki wa klabu hizi watambue kuwa mechi hizi zinaoneshwa ‘live’ hivyo tusijitie doa kwa kuonekana tu wababaishaji.
    Mpira wa miguu si mchezo wa kihuni, ingawa wapo wahuni wanacheza mpira, lakini hiyo si sababu ya kuharibu thamani ya mchezo huo. Ni imani yetu kuwa baada ya dakika 90 wachezaji, mashabiki na hata viongozi watashikana mikono kuashiria kuridhika na matokeo ya uwanjani. Kila la heri.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment