Maalim Seif Sharif Hamad
Vyama tisa vya siasa kati ya 14 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu Zanzibar
mwaka jana vimeungana na CUF kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa
kufanyika Machi 20, hadi utakapopatikana mwafaka wa kumaliza mgogoro wa
kisiasa.
Mratibu wa umoja wa vyama hivyo, Kassim Bakari Ali
alisema jana kuwa vyama hivyo vilikutana Unguja na
kupitisha maazimio mawili ya kutoshiriki uchaguzi huo.
Vyama hivyo ni
UMD, Jahazi Asilia, Chaumma, UPDP, DP, CCK na ACT Wazalendo. Ushiriki wa
vyama vya ADC na CCK bado una utata kutokana na wagombea wake kutangaza
kushiriki licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti, hali
iliyosababisha wagombea hao kusimamishwa.
Vyama ambavyo
vimetangaza kushiriki marudio hayo hadi sasa ni CCM, Tadea, TLP, Sau na
AFP.
Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea kuwa
kwenye mgogoro wa kisiasa kati ya vyama vikubwa vinavyounda Serikali ya
Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya CUF kususia marudio ya uchaguzi baada ya
ule wa awali kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),
Jecha Salim Jecha.
Akitaja maazimio ya vyama hivyo, Kassim
alisema wamekubaliana kutoshiriki marudio ya uchaguzi huo hadi mgogoro
wa CCM na CUF utakapomalizika na wameunda kamati ya wajumbe 18 ya
wenyeviti na makatibu wa kila chama ili kuanzisha meza ya kutafuta
suluhu ya mvutano uliopo kati ya CCM na CUF.
“Tutaanza kukaa na viongozi
wa vyama hivyo kila upande kujua ni nini hasa hatima ya mvutano huo na
tunajikwamuaje,” alisema.
Ali ambaye pia ni mwenyekiti wa Jahazi
Asilia alisema mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na Wazanzibari wenyewe,
hivyo ni vyema viongozi hao wa kisiasa wakajenga uvumilivu katika
kutafuta mwafaka.
Alisema tatizo la vyama hivyo siyo kushiriki
marudio ya uchaguzi huo tu bali ni kuangalia chanzo na hatima ya mgogoro
huo kwa masilahi ya Wazanzibari.
Mwenyekiti
wa CCK, Constatine Akitanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi
wa kusimamishwa uanachama kwa mgombea wake wa urais, Ali Khatibu Ali,
unakwenda sanjari na kutoshiriki uchaguzi hadi maridhiano ya CUF na CCM
yapatikane.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia AFP, Said Soud
Said alisema jana kwamba, chama hicho kimekubali kurudia uchaguzi huo.
“Lengo la chama chetu ni kushika dola, sasa tusiposhiriki itakuwaje?
Kwanza hatuamini kama CUF haijatendewa haki kwa sababu ni kweli kulikuwa
na udhaifu, mfano vurugu za kituo cha kupigia kura cha Matrekta Wawi,” alisema.
Mwenyekiti
wa TLP, Augustine Mrema alisema kama vyama hivyo viliiamini ZEC katika
uchaguzi uliopita, vinatakiwa kuiamini kwenye marudio hayo kwa kuwa
hakuna mbadala.
“Naomba wakubali kurudia uchaguzi kwani ‘maji
yalishamwagika na kuzoleka haiwezekani... Nani aliyekwenda mahakamani
kupinga? Wanachoogopa kurudia ni kitu gani kama walishinda?” alihoji Mrema.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment