Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewahakikishia
Watanzania wote kwamba watapatiwa hati halali ya umiliki wa ardhi,
nyumba na mashamba ili kujinufaisha na mikopo katika taasisi za fedha,
kujikwamua kiuchumi na kuingizia serikali mapato.
Aidha, wawekezaji watakaopatiwa hati na kubainika kutoendeleza
mashamba yao kwa miaka mitatu, watapokonywa na kugawiwa kwa wananchi kwa
ajili ya kuyaendeleza.
Akizungumza katika uzinduzi wa Programu ya Kuwezesha Umilikishwaji
Ardhi (LTSP) Dar es Salaam jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi alisema lengo la programu hiyo ni kupunguza
migogoro ya ardhi iliyokuwepo nchini.
Programu hiyo itaanza kwa mkoa wa Morogoro katika wilaya za Ulanga na
Kilombero, ambayo itadumu kwa miaka mitatu na kugharimu Dola za
Marekani milioni 15.2, ambazo zimefadhiliwa na Washirika wa Maendeleo
zikiwemo nchini za Denmark, Uingereza na Sweden.
Lukuvi alisema kwa sasa ni asilimia 10 ya Watanzania wanaomiliki
ardhi kihalali, hivyo inachangia migogoro ya ardhi kwa kuwa ardhi
iliyokuwepo haijulikani nani mmiliki wake, na kutokana na changamoto
hiyo, ardhi inakosa tija katika kuchangia kupunguza umasikini na
ongezeko la uvamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema programu hiyo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa
kila Mtanzania, itamsaidia kumiliki kihalali ardhi yake kupitia sheria
ya ardhi ikiwemo ya kimila na makazi na kubainisha ni nani anayemiliki
shamba na nyumba.
Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen alisema programu hiyo
itasaidia Watanzania kuona usalama wa ardhi yao na itatoa fursa nyingi
kwa masuala ya kilimo na uwekezaji; na kuwa Watanzania wataweza kuhakiki
taarifa za ardhi na matumizi yake yanahifadhiwa kwa matumizi ya
baadaye.
Chanzo HabariLeo.
Thursday, 18 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment