Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
ameibuka tena na kutangaza kukamilika kwa matayarisho ya uchaguzi wa
marejeo Machi 20, mwaka huu huku akikataa kutoa majina ya wagombea.
Jecha
ambaye tangu afute uchaguzi alionekana hadharani Januari 12, 2016
wakati wa sherehe za Mapinduzi na baadaye kwenye televisheni akitangaza
tarehe ya uchaguzi huo wa marudio, alisema wagombea wote ‘waliojitoa’
watapewa haki zote wanazostahiki kupewa kama wagombea kwa kuwa
hawakufuata taratibu za kisheria za tume hiyo akimaanisha kuwa hakuna
mgombea aliyejitoa kauli ambayo inapingana na msimamo wa CUF ambayo
imetangaza kuwa mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif Hamad
hatagombea.
Kama alivyofanya wakati anatangaza tarehe ya
uchaguzi wa marudio, jana alizungumza kupitia mwandishi wa Televisheni
ya Taifa (TBC), akiwaacha waandishi waliokuwa wameitwa kwa ajili ya
mkutano wake nje ya ofisi hiyo.
Jecha ambaye amekuwa haonekani
hadharani isipokuwa katika matukio machache, alisema tume yake
inawahesabu waliokuwa wagombea katika uchaguzi ulio futwa kuwa ni
halali, licha ya kuandika barua za kujitoa katika tume hiyo.
“Pamoja na
kuwa wagombea wengi, hasa wa CUF, kuandika barua za kujitoa katika ofisi
za ZEC wilaya na makao makuu, hakuna barua hata moja ambayo imefuata
utaratibu wa kisheria na kwa mantiki hiyo, bado tunahesabu wagombea hao
ni halali katika uchaguzi mkuu wa marejeo,” alisema Jecha.
Katika
taarifa hiyo, Jecha alisema vyama vinane vimeshathibitisha ushiriki wake
katika uchaguzi huo vikiwamo Tadea, ACT, ADC, AFP, SAU, TLP na CCM na
utaratibu wa kuwapatia ulinzi wagombea hao umeshaanza.
Jecha alisema
ofisi yake imeshafanya mawasiliano na vyama na wagombea na kuwapa
taarifa mbalimbali za matayarisho ya uchaguzi, ili waanze taratibu za
kupanga mawakala wao.
Alisema baadhi ya vyama vimetoa taarifa
kupitia vyombo vya habari kuwa havitashiriki katika uchaguzi, na
kuwataka wagombea wao kuandika barua za kutoshiriki katika upigaji kura
huo.
“Swala hili naomba nilitolee ufafanuzi kidogo kwa kuwa
kauli za vyama hivyo zimewachanganya baadhi ya wagombea waliodhaminiwa
na vyama hivyo, ambao bado wanataka kugombea katika uchaguzi huo,”
alisema Jecha.
Alisema kila chama cha siasa kilichosajiliwa
kinachokusudia kushiriki uchaguzi wa Rais kitawasilisha jina la mgombea
wake wa urais kwa tume, na ili mtu awe ameteuliwa kihalali kuwa mgombea
urais ni lazima awe amedhaminiwa kwa maandishi na watu wasiopungua 200
ambao wameandikishwa kuwa wapiga kura kutoka kila mkoa wa Zanzibar.
“Kwa
bahati mbaya mpaka tunapowasilisha taarifa hii, hakuna chama hata
kimoja kati ya vyama ambavyo vimejinadi kuwa havitashiriki katika
uchaguzi kilichoiandikia Tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake
kushiriki katika uchaguzi,” alisema Jecha katika taarifa yake.
“La
pili ni kuwa utaratibu wa kujitoa kwa wagombea katika uchaguzi
umefafanuliwa vizuri sana katika kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2015,”
alisema mwenyekiti huyo akisisitiza kuwa haukufuatwa.
Kwa mujibu
wa vifungu hivyo, alisema mgombea wa urais anaweza kujiondoa kwa kutoa
taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa
mwenyekiti si zaidi ya saa 10 jioni siku ya uteuzi.
“Mgombea
uwakilishi na udiwani anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi
aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi si
zaidi ya saa 10 jioni ya siku inayofuatia siku ya uteuzi."
Jecha
alifafanua kuwa tarifa ya kujiondoa chini ya kanuni hizo inatakiwa
iambatanishwe na tamko la kisheria lililotolewa na kutiwa saini na
mgombeya mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa mgombea wa urais na hakimu
kwa mgombea wa uwakilishi au udiwani, mambo ambayo hayakufanyika.
Kuhusu
daftari la wapigakura, Jecha alisema kazi ya uchapishaji wa madaftari
na vituo vya kupigia kura ndani na nje imeshakamilika, na wanatarajia
mwisho wa mwezi huu majina hayo kubandikwa.
Alisema ratiba ya
mafunzo kwa wasaidizi na wasimamizi wa majimbo imeshakamilika, na
mafunzo hayo kwa Unguja na Pemba yataendeshwa Februari 22-28 na
wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo watapewa mafunzo Machi 2 hadi Machi 5.
Alisema mafunzo mengine yatakayotolewa ni ya wasaidizi wa vituo
vya kupigia kuwa ambayo yamepangwa kufanyika Machi 11 -13 na mafunzo ya
mawakala wa uchaguzi siku ya Machi 14 na mafunzo ya walinzi wa vituo
vya kupigia kura Machi 15, 2016.
Jecha alisema kazi ya upangaji
wa vifaa vya kupigia kura kwa ajili ya kusambazwa wilayani tayari
imeanza katika ghala za ZEC za Unguja na Pemba na baada ya kukamilika
kwa kazi hiyo, utaratibu wa kuvisafirisha katika wilaya husika
utaandaliwa.
Kuhusu uchapishaji karatasi za kura, mwenyekiti
huyo alisema matayarisho yamekamilika baada ya tume kumpitisha
mchapishaji wa karatasi hizo.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment