Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za kushtukiza, baada ya
kutembelea ofisi za Kivukoni Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni
kuangalia mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.
Mashuhuda
waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni wakati Rais anafanya ziara hiyo,
walieleza mtindo alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa kawaida na
vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo wa Rais.
Mfanyabiashara
wa eneo hilo, Sharif Mkamba alisema Rais Magufuli aliingia saa 11 jioni
akiwa na msafara wa magari matatu ya kawaida yaliyokuwa na namba za
kiraia.
“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea bali
ulikuwa ni msafara wa kimya kimya. Aliingia moja kwa moja kwenye zile
ofisi na alitumia kati ya dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema
Mkamba.
Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya
magari matatu alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia kwa kina kwa kuwa
haijazoeleka na walitegemea huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.
“Aliteremka
na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa tulizozipata jana zinadai
hakumkuta huyo bosi, sijui ni meneja au ofisa sisi hatujui,” alisema
Likoko ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo eneo la
kivukoni.
Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya kimya,
Rais Magufuli hakusita kuwasalimia wasafiri waliokuwa wakisubiri kivuko
wakati alipofanya ziara hiyo.
Alieleza kuwa kama wananchi
walifurahishwa na hatua hiyo ya Rais, kwa kuwa watendaji wengi hawafanyi
kazi siku za wikiendi licha ya huduma zake kufanyika siku zote.
Tangu
jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa ikimuonyesha Rais Magufuli
akiwa Kivukoni akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku akishangiliwa
na wasafiri waliokuwa wakingoja kivuko.
Hata hivyo, jitihada za
kutafuta mamlaka husika kueleza kwa undani malengo ya ziara hiyo
ziligonga mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kutopokea
simu.
Ofisa habari wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa)
Theresia Mwami, alitaka utafutwe uongozi wa juu kueleza yaliyojiri
kwenye ziara hiyo kwa kuwa yeye yupo likizo.
Credit;Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment