Na Khelef Nassor, Zanzibar
MWANAMKAKATI wa aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Mohamed Sultan
Mugheiry, maarufu kwa jina la Eddy Riyami, amewekwa ndani na Jeshi la
Polisi mjini Unguja kwa tuhuma za kumtukana Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein.
Eddy Riyami ambaye ni mmoja wa wana mkakati wa timu ya ushindi wa
aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikutwa na
mkasa huo jana baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tuhuma
zinazomkabili.
Riyami ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar,
alikwenda Polisi Makao Makuu kuitikia wito wa Naibu Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, SSP Simon Pasua, huku akiandamana
na Mwanasheria wa CUF, Masoud Faki Masoud.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mwanasheria huyo alisema Riyami anatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya kimtandao.
Alisema licha ya kuzikana tuhuma hizo, lakini Jeshi la Polisi bado lilimshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Ni kweli ameshikiliwa na polisi kwa ajili ya kupitisha uchunguzi na
yupo Polisi Madema, eti Eddy kaambiwa kamtukana Dr. Shein kwenye ‘audio’
ambayo hata si sauti yake, lakini dhamana ipo wazi na tutamchukulia
dhamana,” alisema Masoud.
Akizungumzia kukamatwa kwa Riyami, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na
Makosa ya Jinai, Salum Msangi, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa
huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
“Kitu ninachoweza kuthibitisha ni kuwa tunamshikilia Riyami kwa ajili ya kupitisha uchunguzi,” alisema Naibu Kamishna Msangi.
Februari 17, mwaka huu Ofisi ya Mkurunzi na Makosa ya Jinai,
ilimwandikia Riyami barua ya wito na kumtaka kufika ofisi ya upelelezi
iliyopo Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
Riyami alitii wito huo ambapo wiki iliyopita alikwenda lakini mmoja
wa maofisa wa Jeshi la Polisi aliyemwandikia barua alikuwa nje ya
Zanzibar kwa shughuli za kikazi na kumtaka kwenda jana jumatatu
Riyami si mwanachama wa CUF, lakini mara kadhaa amekuwa akitumiwa na
chama hicho kwa ajili ya mikakati mbalimbali pamoja na ushauri.
Chanzo Mtanzania.
Monday, 22 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment