UFISADI uliofanyika katika uchapaji wa vitabu 2,807,600, vilivyo
tayari kutumika kwa ajili ya darasa la kwanza nchi nzima, umesababisha
wanafunzi hao, ambao mwaka huu udahili wao umeweka historia kwa idadi
kubwa kuwahi kudahiliwa, kulazimika kutumia vitabu vya zamani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Maimuna Tarishi (pichani), alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa
habari ofisini kwake Dar es Salaam. Alifafanua kwamba kasoro kubwa,
zilizobainika katika vitabu hivyo, ambavyo vilishafika katika ghala la
Serikali, zimesababisha Serikali izuie visisambazwe.
Kwa mujibu wa Tarishi, vitabu hivyo vya ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha
Kwanza’ na ‘Najifunza Kusoma Kitabu cha Pili’, vimechapwa na kampuni ya
Yukos Enterprises, ambayo ni moja ya kampuni tatu zilizoshinda zabuni ya
kazi hiyo iliyotangazwa Aprili mwaka jana.
Lakini, alisema kasoro hizo zimesababisha Serikali kuagiza viondolewe
katika ghala lake na udhibiti ufanyike visisambazwe mashuleni.
Upungufu
Kasoro zilizokutwa ni muingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa, picha
moja kuwa na rangi tofauti, ukataji usiozingatia vipimo, baadhi ya
vitabu kufungwa kwa pini moja katikati badala ya mbili, huku vingine
vikikosa pini kabisa na vingine vikifungwa ubavuni.
Kasoro nyingine ni vingine vimekutwa vimechakaa kabla ya matumizi,
hasa kitabu cha ‘Najifunza Kusoma Darasa la Kwanza Kitabu cha Pili’;
vingine vikiwa na mpangilio mbaya wa kurasa, ufifiaji wa maandishi huku
picha katika baadhi ya vitabu na maandishi, vikishindwa kuonekana
kabisa.
Kasoro nyingine kwa mujibu wa Tarishi ni namba za kurasa kutoonekana
kabisa, baadhi ya kurasa kujirudiarudia, baadhi ya kurasa
kutotenganishwa, maandishi ya baadhi ya vitabu kugeuzwa mwelekeo,
majalada kuwa zaidi ya moja na baadhi ya vitabu kukutwa vimedurufiwa
(photocopy).
Katibu Mkuu huyo alisema kasoro hizo, zilibainika baada ya
ufuatiliaji kufanywa na Wizara katika bohari iliyokuwa ikipokea vitabu
hivyo.
“Kutokana na kasoro hizo, ni dhahiri mchapaji Yukos Enterprises Ltd
hakuzingatia vigezo vilivyowekwa na kwa kufanya hivyo amekiuka
makubaliano yaliyo katika mkataba alioingia na Taasisi ya Elimu
Tanzania,” alisema Tarishi.
Athari zake
Kutokana na hali hiyo, Tarishi alisema wanafunzi wa darasa la kwanza
mwaka huu watapungukiwa vitabu vya kujifunza kusoma, kwa kuwa haviwezi
kutumika. Hivyo aliagiza wanafunzi wa darasa la kwanza mwaka huu,
watumie vitabu vya zamani na walimu watatumia ‘Kitabu cha Kiongozi cha
Mwalimu’ ambacho ni kipya.
Kuhusu gharama iliyotumika, Tarishi alisema ni zaidi ya Sh bilioni
mbili, lakini alibainisha kuwa mchapishaji alikuwa amelipwa asilimia 20
tu kwa kutumia dhamana ya benki.
Majipu yatumbuliwa
Kasoro hizo zimemlazimu Katibu Mkuu huyo kuagiza Bodi ya Wakurugenzi
wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuwasimamisha kazi vigogo wa taasisi
hiyo, akiwemo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Vifaa vya Kielimu, Peter
Bandio, Mwanasheria, Pili Magongo na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na
Ugavi, Jackson Mwaigonela.
Hatua hiyo imetakiwa kufuatia uchunguzi katika taasisi hiyo, kuhusu
vipi wameshindwa kusimamia Sheria ya Manunuzi na kazi ya uchapaji wa
vitabu.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 27 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment