Rais Dkt John Magufuli
RAIS John Magufuli ameombwa kulilinda Shirika la Posta kwa
kuzilazimisha taasisi, wizara na Idara za Serikali kutumia huduma
zinazotolewa na shirika hilo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mtandao wa Simu Nchini (TEWUTA), Pius Makuke
alisema jana kuwa njia hiyo ndiyo pekee itakayoliokoa shirika hilo
lisife.
Alisema kwa sasa taasisi nyingi za Serikali zinatumia mashirika
binafsi hata kusafirisha vifurushi na barua na kuomba hatua alizochukua
Rais Magufuli za kuzuia sukari kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani,
pia atumie mbinu hiyo kuzilazimisha taasisi za Serikali kutumia huduma
za Posta ili lipate mtaji wa kutosha liweze kujiendesha kwa faida.
Alisema wanatoa ombi hilo kwa Rais kwani baada ya Shirika la Posta
kuanzishwa mwaka 1994, Serikali iliahidi kulipatia mtaji, lakini hata
hivyo mtaji huo hadi leo haukupatikana jambo linalofanya lishindwe
kujiendesha.
Aliongeza kuwa Serikali ilipoamua kutenganisha Shirika la Posta na
Kampuni ya Simu (TTCL) mwaka 1994 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa
Shirika la Posta na Simu, Serikali kwa mujibu wa sheria iliyounda
Shirika la Posta iliazimia kutoa mtaji ili lijiendeshe vyema kibiashara.
“Hata hivyo kwa masikitiko makubwa toka mwaka huo wa 1994 hadi leo
Shirika la Posta halijawezeshwa kimtaji na Serikali ambayo ndio mwenye
mali,” alisema Makuke.
Aliongeza kuwa kipimo kizuri cha utendaji kazi hivi sasa ni uwezo wa
mtaji na akaongeza kuwa iwapo kuna mtaji ni rahisi kuwatathmini viongozi
katika ufanisi wao.
“Ombi letu kwa Serikali yetu tunaomba Shirika la Posta kuwezeshwa
mtaji wa kujiendesha katika mwaka huu wa fedha,” alisema mwenyekiti
huyo.
Alisema uwezeshaji wa Shirika la Posta kimtaji unaweza usiwe na fedha
taslimu ili shirika lifikie malengo tarajiwa, ni lazima Serikali itoe
maamuzi mazito na mwongozo kwa taasisi zote za Serikali na Wakala za
Serikali kutumia huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa ajili ya
usafirishaji wa barua, vifurushi na vipeto.
Alisema kwa sasa inasikitisha kuona baadhi ya taasisi za umma
zimekuwa zikitumia kampuni binafsi katika kusafirisha vifurushi, barua
na vipeto jambo ambalo alisema Tewuta inaamini kuwa halifanyiki kwa
maslahi ya Taifa, bali ni kwa maslahi binafsi.
Chanzo HabariLeo.
Sunday, 21 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment