Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi ya Agape, John Myola |
MILA potofu mkoani Shinyanga maarufu Samba, imebainika kuhamasisha ndoa za utotoni, ambapo wazazi wamekuwa wakiwatoa watoto wa kike shuleni na kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji kuogeshwa ili wapendwe na vijana wa kiume.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi ya Agape, iliyokuwa ikitekeleza mradi wa kupambana na ndoa za utotoni, John Myola, amesema mila hiyo pia imekuwa ikitumika kuwafanyia watoto ukatili na kuwaambukiza magonjwa.
Kwa mujibu wa Myola, wakati wakitekeleza mradi huo, walibaini katika mkoa huo, ni jambo la kawaida watu wazima wanaume, kushiriki vitendo vya ngono na watoto kati ya miaka minane hadi 13 na kwa kuwa umri wao ni mdogo, inakuwa rahisi kuwashawishi kuliko watoto wa miaka 17 na 18.
“Watoto wa miaka 13 na 14 wanaolewa sana na watoto wenzao au na watu wazima, lakini wale wa kuanzia umri wa miaka 17 na 18 wanawaogopa kwa kuwa akili yao imeshapevuka kidogo. “Mila hiyo imesababisha kuongezeka kwa tatizo la mimba za utotoni kama mlivyosikia kwamba Mkoa wa Shinyanga unaongoza, hii inasababishwa na mila na desturi za mkoa huo ambazo zinaelekeza mtoto anapofika darasa la tano, apelekwe kwa waganga wa kienyeji kuogeshwa dawa ili wanaume waanze kumuona, hii ni changamoto kubwa,” alisema Myola.
Changamoto nyingine waliyokutana nayo kwa mujibu wa Myola, ni msichana anapoolewa, kutakiwa kuandaa wasichana wenzake ambao hawajawahi kukutana na wanaume na mvulana anayeoa na yeye anakuja na vijana wa kiume idadi sawa na ile ya wasichana, wanapofika kwenye sherehe wanaachiwa kuwa pamoja kuanzisha uhusiano.
Alisema shirika lake limekuwa likijitahidi kutoa elimu katika shule mbalimbali mkoani Shinyanga ili watoto wa kike na wa kiume wajitambue na kufahamu haki zao.
Mbali na shuleni, Myola amesema pia wameendelea kukutana na wazee wa mila na wa dini kuweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la ndoa za utotoni pamoja na mimba katika umri mdogo.
“Tunapobaini watu wanaowapa mimba watoto hatuna msamaha nao, tunawafikisha kwenye vyombo vya sheria mara moja ili wachukuliwe hatua, tena mara nyingine tunatoa taarifa tunapewa askari tunakwenda kukamata pamoja,” alisema Myola.
Myola alivitaka vyombo vya habari kutoa ushirikiano mkubwa katika kuandika habari zinazomkandamiza mtoto. Pia aliwataka viongozi wa dini kukemea mila hiyo na vyombo vya dola kutekeleza wajibu wao, ili kumrudishia amani mtoto na tumaini la maisha yake.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment