MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu.
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu amewaagiza
makamanda wa Polisi kote nchini, kuendesha oparesheni kali ya
kuwachukulia hatua za kisheria, waendesha bodaboda wasiotii sheria za
usalama barabarani.
Ametaja makosa yatakayosababisha waendesha bodaboda hao kukamatwa
kuwa ni pamoja na kubeba abiria zaidi ya mmoja, kupita katika taa
nyekundu na kutovaa kofia ngumu.
IGP Mangu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa wakuu wa
Polisi, wakiwemo makamanda wa Polisi wa mikoa, vikosi na makao makuu
katika kikao kazi kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni ambacho
kilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.
Alisema waendesha bodaboda wamekuwa wakikaidi kufuata sheria za
usalama barabarani, lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka makamanda
wa Polisi wa mikoa kote nchini, kutekeleza maelekezo hayo, ili kuleta
nidhamu kwa bodaboda katika kufuata sheria za usalama barabarani.
IGP Mangu alisema suala la kufuata sheria za usalama barabarani kwa
bodaboda halina mjadala na kila Kamanda ahakikishe kuwa wote wasiofuata
sheria na kukaidi, wanakamatwa bila kuoneana muhali kwa kuwa wamekuwa
wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.
“Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina zote, natoa maelekezo
kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha oparesheni kali dhidi ya bodaboda,
ili kupunguza ajali zinazosababishwa na bodaboda. “Wengi wao hawataki
kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, tusiwaonee muhali maana
maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la msingi ni kusimamia sheria
tu,” alisema IGP Mangu.
Awali akifungua kikaokazi hicho Waziri Kitwanga alilitaka Jeshi la
Polisi kuendelea na mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu, ili
usalama wa raia na mali zao uendelee kuimarika na Watanzania waendelee
na shughuli zao za kujiletea maendeleo bila hofu ya kutendewa uhalifu.
Chanzo HabariLeo.
Friday, 19 February 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment